Trump kuwania tena Urais wa Marekani mwaka 2024
Amesema anafikiria kufanya hivyo akiwa ndani ya chama cha Republican na siyo kwa kuanzisha chama kipya.
- Amesema anafikiria kufanya hivyo akiwa ndani ya chama cha Republican.
- Hana mpango wa kuanzisha chama kipya.
- Asisitiza kuwa alishinda urais katika uchaguzi mkuu mwaka jana.
Aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump amesema anafikiria kuwania tena urais katika uchaguzi mkuu waTaifa hilo mwaka 2024 huku akisisitiza kuwa alishinda uchaguzi wa Novemba mwaka jana uliompa ushindi Rais Joe Biden.
Trump ambaye ameonekana kwa mara ya kwanza kwa umma tangu aondoke madarakani katika mkutano wa kisiasa wa muungano wa kihafidhina (CPAC) uliofanyika katika jimbo la Florida, amesema huenda akajitosa katika mbio za urais katika uchaguzi mkuu ujao.
“Nani anayejua. Ninaweza kuamua kuwashinda kwa mara ya tatu. Hio ni sawa?,” amenukuliwa mwanachama huyo wa chama cha Republican na vyombo vya habari vya kimataifa wakati akizungumza katika mkutano huo.
Hata hivyo, Trump amepuuza taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ana mpango wa kuanzisha chama chake na kuondoka Republican, akizitaja kama ni habari za uzushi na uongo.
“Tukiwa pamoja katika miaka ijayo, tutaubeba na kuupeleka mbele mwenge wa uhuru wa Marekani. Tutaongoza harakati za kihafidhina na chama cha Republican kurudi kwenye ushindi kamili. Na tumewahi kupata ushindi mkubwa. Msisahau kamwe,” amesema kiongozi huyo anayeishi katika makazi yake ya Mar-a-Lago katika jimbo la Florida.
Soma zaidi:
Trump aliyeiongoza Marekani kwa muhula mmoja kuanzia mwaka 2017 hadi 2021 ameendelea kusisitiza madai yake kuwa alimshinda rais wa sasa Biden katika uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka uliopita.
Amedai kuwa uchaguzi wa mwaka jana ulikumbwa na udanganyifu mkubwa lakini madai yake yalitupiliwa mbali na mahakama nchini humo.
Mkutano huo wa CPAC wa kila mwaka hufanyika mjini Washington lakini ulihamishwa hadi Orlando kutokana na vizuizi vya Covid-19 vilivyowekwa mjini Florida.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa wakosoaji wa Trump hawakuhudhuria mkutano huo.