November 24, 2024

Tusipoteze muda na wasioamini katika mabadiliko ya tabianchi-Kabudi

Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba John Kabudi ameitaka jumuiya ya kimataifa kuwajibika na isipoteze muda na watu wasioamini katika uharibifu wa mazingira unaosababisha mabadiliko ya tabianchi

  • Waziri huyo Mambo ya Nje ameitaka jumuiya ya kimataifa kuwajibika na  isipoteze muda na watu wasioamini katika uharibifu wa mazingira.
  • Amesema nchi zilizoendelea kiviwanda zina wajibu wa kufanya kupunguza hewa ukaa.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Profesa Palamagamba John Kabudi ameitaka jumuiya ya kimataifa kuwajibika na  isipoteze muda na watu wasioamini katika uharibifu wa mazingira unaosababisha mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame na ongezeko la joto. 

Prof. Kabudi amezengumzia hatua hiyo wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kabla ya kuhutubia mkutano wa baraza kuu la UN na kusema kila nchi itakiwa kuwajibika kwa kuwekeza fedha ili kuokoa mazingira. 

“Wako ambao wanakana kwamba tatizo hilo halipo, hao tusipoteze muda wetu sana, lakini wale wanaokiri kwamba tatizo hilo lipo wajue kuwa wanapotoa fedha zao kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kushughulikia tatizo hilo katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania hawafanyi hivyo kwa hisani bali wanatimiza wajibu wao,” amesema Kabudi. 

Amesema waliochafua mazingira lakini sasa wana mali za kutosha, wana wajibu wa kutoa fedha, teknolojia ya kupambana na  hali hiyo na nchi zilizobaki zina wajibu wa kushiriki katika miradi hiyo ili kunusuru na kuikoa dunia isiangamie mapema kuliko inavyotarajiwa.


Soma zaidi: Maoni: 


Aidha, amesema Tanzania inaungana na Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guaterres katika kuhakikisha kwamba nchi zinazoendelea zinasaidiwa kupata maendeleo na wakati huo huo kuhifadhi mazingira. 

“Na maana yake wote tuna wajibu wa pamoja wa kulinda mazingira, lakini kila mtu ana wajibu ulio tofauti,” amesisitiza Kabudi. 

Tanzania imetenga asilimia 32 ya eneo la nchi kama hifadhi ya misitu ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.