July 8, 2024

Tuzo za mwajiri bora 2020 zafutwa Tanzania

Tuzo za mwajiri bora (EYA) ambazo hutolewa kila mwaka tangu mwaka 2005 zimekuwa chachu kwa waajiri Tanzania kuwawekea mazingira bora ya kazi wafanyakazi wake ili kuwawezesha kupata haki zao.

  • Uongozi wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) umesema tuzo hizo hazitokuwepo kwa mwaka 2020 kufuatia sababu zilizo nje ya uwezo wa chama hicho.
  • Wadau wa chama hicho wameombwa kushiriki katika zoezi la mapitio ya tuzo hizo ambazo zimeanza kutolewa tangu mwaka 2005.

Dar es Salaam. Waajiri waliojipanga kuwania tuzo za mwajiri bora kwa mwaka 2020 hawatapata fursa hiyo mwaka huu kwa sababu waandaji wa tuzo hizo ambao ni Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wamezifuta kutokana sababu zilizo nje ya uwezo wa chama hicho.  

Tuzo za mwajiri bora (EYA) ambazo hutolewa kila mwaka tangu mwaka 2005 zimekuwa chachu kwa waajiri Tanzania kuwawekea mazingira bora ya kazi wafanyakazi wake ili kuwawezesha kupata haki zao. 

Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk Aggrey Mlimuka katika taarifa yake iliyotolewa Septemba 14, 2020, amesema tuzo hizo hazitatolewa mwaka huu kufuatia sababu zilizo nje ya uwezo wa chama hicho ikiwemo mabadiliko yaliyoletwa na COVID-19. 

“Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kinapenda kutoa taarifa kwa wadau wake kuwa, kufuatia sababu zilizo nje ya uwezo wetu, tuzo za mwajiri bora wa mwaka (EYA) kwa mwaka 2020 zimefutwa,” amesema Dk Mlimuka.


Soma zaidi:


Hata hivyo, Dk Mlimuka amesema kufutwa kwa tuzo hizo mwaka huu kunatoa fursa kwa ATE kupitia vigezo, makundi na mfumo mzima wa utoaji wa tuzo ili kuendana na vigezo vya kimataifa vya menejimenti ya rasilimali watu.

Mapitio hayo pia yataangazia mabadiliko yaliyosababishwa na ugonjwa wa Corona ili kuhakikisha tuzo zijazo zinaendana na hali halisi. 

“ATE inachukua nafasi hii kuwaomba wanachama wake walioshiriki tuzo hasa wa mwaka 2019 walioshinda na hata waliosindwa kushiriki katika zoezi la mapitio,” amesema Dk Mlimuka.

Mwaka 2019, tuzo ya mwajiri bora ya mwaka ilichukuliwa na kampuni ya bia Tanzania (TBL) katika nafasi ya kwanza huku nafasi ya pili ikichukuliwa na kampuni ya uchimbaji wa dhahabu ya Geita Gold Mine na nafasi ya tatu ilienda kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).