October 6, 2024

Twiga hatarini kutoweka duniani

Wadau wa uhifadhi wanyama pori wanafanya mapitio ili kutathmini kama mnyama huyo aingizwe katika orodha ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka duniani.

Twiga amekuwa akiwindwa kwa ajili ya nyama na ngozi ambayo hutumika katika shughuli za kimila.Picha|Mtandao.


  • Wadau wa uhifadhi wanyama pori wanafanya mapitio ili kutathmini kama mnyama huyo aingizwe katika orodha ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka duniani.
  • Inaelezwa kuwa hadi 2016 kulikuwa na Twiga 97,000.
  • Kampeni za mtandaoni kumnusuru mnyama huyo zashika kasi.

Dar es Salaam. Licha ya twiga kuwa sehemu muhimu ya vivutio vya watalii katika mbuga za wanyama, mnyama huyo yuko katika hatari ya kutoweka duniani kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali za kuishi katika mazingira salama. 

Kutokana na hatari hiyo, shirika la Marekani la Huduma za Samaki na Wanyama pori (FWS) limetangaza kuwa litafanya mapitio ya miezi 12 yatakayotathmini kama twiga apewe hadhi ya kuwa miongoni mwa wanyama pori walio katika hatari ya kutoweka duniani.

kwa mujibu wa Muungano wa Kimataifa wa Utunzaji wa Maliasili (IUCN) tangu 1985, idadi ya twiga imepungua kati ya asilimia 30 hadi 40,  ambapo inakadiriwa kuna twiga 97,000 waliobaki mbugani kwa takwimu za mwaka 2016.

Makundi mbalimba nchini Marekani yakiwemo ya ‘Humane Society’ na kituo cha ‘Biological Diversity’ wameanzisha harakati za mtandaoni kuishinikiza Serikali ya Marekani kumuweka twiga katika orodha ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka duniani. 

Makundi hayo yanaamini kuwa hatua hiyo itawasaidia wadau wa utunzaji wa maliasili kuchukua hatua stahiki za kumlinda mnyama huyo aendelee kuishi kama inavyofanyika kwa faru weusi na tembo. 

Katika kile kinachoelezwa kama ”kutoweka kimya kimya” kwa twiga kunakosababishwa na uwindaji haramu na kuongezeka kwa maeneo ya kufanyia kilimo, ujenzi wa barabara na ukuaji wa miji kunachangia kupungua kwa miti ya mshanga (acacia) ambayo ni chanzo kikubwa cha chakula cha  mnyama huyo. 


Zinazohusiana:


Twiga amekuwa akiwindwa kwa ajili ya kitoweo ambapo hutumiwa zaidi na nchi zilizoendelea ikiwemo Marekani. 

Lakini Mfuko wa Wanyama pori wa Afrika (African Wildlife Conservation) unaeleza kuwa watu wanawinda twiga ili kujipatia ngozi na nyama yake ambayo ina thamani kubwa katika mila na tamaduni za Afrika. 

Ngozi na viungo vingine vya mwili wake vimekuwa vikitumika kutengenezea vikuku, nyuzi za kushonea na hata kamba. Ni rahisi kuwauwa twiga kwa ajili ya nyama na ngozi. 

Baada ya FWS kufanya mapitio yake itatoa fursa kwa umma kutoa maoni kabla ya uamuzi wa mwisho kutolewa. 

Hata hivyo, Marekani imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuwalinda wanyama hao  ambapo gazeti la The Independent la nchini humo linaeleza kuwa kati ya mwaka 2006 hadi 2015, zaidi ya twiga 39, 500 (wakiwa hai na waliokufa) waliingizwa nchini humo.