Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 8 kila mwaka ifikapo 2025
Serikali imesema ina imarisha sera za jumla za uchumi na fedha ili kufikia azma hiyo kwa kutengeneza mazingira mazuri ya ufanyaji wa biashara.
- Anakusudia kuufanya uchumi kukua kwa asilimia 8 kila mwaka.
- Kukaa meza moja na sekta binafsi kutatua migogoro ya kibiashara.
- Kuwawezesha wajasiriamali kwa programu za ujuzi na maarifa.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itatekeleza mambo mbalimbali ikiwemo kukuza uchumi kwa wastani wa asilimia 8 kwa mwaka na kutatua migogoro ya kibiashara kati yake na sekta binafsi ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara Tanzania.
Dk Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Novemba 13, 2020) wakati akifungua Bunge la 12 la Tanzania, ameanza awamu ya pili ya uongozi wake wa miaka mitano baada ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Katika hotuba ya Rais aliyowasilisha bungeni ambayo ilikuwa inatoa mwelekeo wa Taifa kwa miaka mitano ijayo, amesema Serikali inalenga kukuza uchumi kwa wastani wa asilimia 8 kwa mwaka na kutengeneza ajira mpya milioni 8.
“Kwenye miaka mitano ijayo tumepanga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na tutahakikisha ukuaji wa uchumi unawanufaisha wananchi hususani kwa kuinua vipato vyao, kupunguza umaskini na tatizo la ajira,” amesema Rais John Magufuli.
Ili kutekeleza azma ya kukuza uchumi na kuongeza ajira, Serikali yake itashughulikia mambo kadhaa ikiwemo kuboresha sera za uchumi jumla na fedha ili ziendane na mahitaji ya wakati huu ambao unatawaliwa na mabadiliko makubwa ya teknolojia.
Aidha, milango itafunguliwa kwa sekta binafsi ya kufanya majadiliano na Serikali kutafuta muafaka wa migogoro ya kibiashara kwa faida ya pande zote mbili ili kuzidi kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini yatakayosaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
“Tunataka mtu yoyote anayetaka kuwekeza asisumbuliwe kwa kuwekewa vikwazo vya aina yoyote. Nataka watanzania wote washiriki kikamilifu kujenga uchumi wa nchi yao. Mimi nataka mwekezaji akija apate kibali ndani ya siku 14,” amesisitiza Rais Magufuli.
Soma zaidi:
Kwa kutambua umuhimu wa sekta binafsi, Rais ametangaza kuhamisha majukumu yote ya uwekezaji ikiwemo ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Ofisi ya Rais.
Serikali hiyo ya awamu ya sita tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi 1992, itakifanya kilimo kuwa cha kibiashara lengo ni kuhakikisha usalama wa chakula, upatikanaji wa malighafi za viwanda na kupata ziada ya kuuza nje.
“Ili kuhakikisha hayo tutahakikisha pembejeo na zana za kilimo ikiwemo mbegu, viwatilifu vinapatikana kwa uhakika na kwa gharama nafuu,” amesema Rais na kuongeza kuwa Serikali inakusudia kununua ndege moja ya mizigo ili kurahisisha usafirishaji ya mazao ya bustani na minofu ya samaki pamoja na nyama.
Fursa za ajira
Ili kutimiza azma ya kutengeneza ajira milioni 8 ifikapo 2025, amesema “tutaendelea kukuza programu za kukuza ujuzi na maarifa ikiwemo maarifa ya ujasiriamali ili kuwapa ujuzi wananchi wetu utakaowawezesha kujiajiri na kuajirika ndani na nje ya nchi.”
Pia uboreshaji wa mazingira ya kufanya biashara kwa wajasiriamali wadogo yaani machinga, baba lishe, mama lishe, waendesha bodaboda, bajaj nao utazingatia ili kuwawezesha kupata ajira na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.
Wakati huo huo, Rais amesema kuwa Serikali inakusudia kuboresha vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo na kuviongezea taarifa muhimu na picha ili wafanyabiashara wavitumie katika shughuli mbalimbali ikiwemo kuombea mikopo katika benki.