October 6, 2024

Udahili wa shahada ya uzamili washuka vyuo vikuu Tanzania

Huenda elimu ya juu nchini Tanzania ikachukua mkondo mpya, baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere kubaini kuwa udahili wa wanafunzi wanaosoma shahada za uzamili katika baadhi ya vyuo vikuu vya umma unashuka kila mwaka

  • Ripoti ya CAG yabaini udahili wa shahada hiyo unashuka kila mwaka tangu mwaka 2016/2017. 
  • Vyuo ambavyo udahili umeshuka ni Chuo Kikuu cha Mzumbe,  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA). 
  • Kutokuwepo matangazo na bajeti kwatajwa kama sababu ya kushuka kwa udahili.

Dar es Salaam. Huenda elimu ya juu nchini Tanzania ikachukua mkondo mpya, baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere kubaini kuwa udahili wa wanafunzi wanaosoma shahada za uzamili katika baadhi ya vyuo vikuu vya umma unashuka kila mwaka. 

CAG Kichere katika ripoti yake kuhusu mashirika ya umma kwa mwaka 2018/2019 iliyotolewa hivi karibuni amesema ukaguzi wake umebaini udahili wa wanafunzi wa shahada hizo umeshuka katika Chuo Kikuu cha Mzumbe,  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).

Ripoti hiyo imesema kutokana na mipango-mkakati ya Chuo Kikuu cha Mzumbe na SUA ya mwaka 2017/2018-2021/2022, Chuo Kikuu cha Mzumbe kiliweka mkakati wa kuongeza udahili wa wanafunzi wa shahada za uzamili kwa asilimia tisa ifikapo mwezi Juni mwaka 2022.

Pia Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kilipanga kuongeza udahili wa wanafunzi wa shahada za uzamili kutoka )wanafunzi 751 mwaka 2015 hadi wanafunzi 2,000 mwaka 2021.


Soma zaidi:


Hata hivyo, CAG amebaini kupungua kwa udahili wa wanafunzi SUA kutoka wanafunzi 813 mwaka 2016/2017 hadi wanafunzi 576 mwaka 2018/19 sawa na upungufu wa asilimia 29.2 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. 

“Aidha, nilibaini kupungua kwa udahili wa wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe kutoka wanafunzi 1,592 mwaka 2014/2015 hadi wanafunzi 730 mwaka 2018/2019,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

CAG Kichere amesema Chuo Kikuu cha Mzumbe kiliweka mipango ya kupanua kozi zilizokuwepo na kusajili kozi nyingine mpya zinazohitajika zaidi sokoni ambazo zingechangia kuongeza idadi ya wadahiliwa. 

Licha ya mipango mizuri iliyokuwepo, chuo hakikutenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa mikakati hiyo.

Katika hatua nyingine, CAG amebaini kuwa udahili wa wanafunzi katika shahada za uzamili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ulishuka mfululizo kwa miaka mitatu hadi wanafunzi 729 walioripotiwa mwaka 2018/2019.

 Ripoti hiyo imeeleza kuwa kutokuwekeza vya kutosha kwenye matangazo ya shahada ya uzamili na kunaweza kusababisha kutofikiwa kwa malengo yaliyokuwepo kwenye mpango-mkakati wa kuongeza wanafunzi wa shahada za uzamili na inaweza kuleta madhara kwenye upatikanaji wa mapato ya ndani. 

Vyuo husika vimeshauriwa kuongeza wigo wa matangazo wa kozi kwa kutumia njia mseto za mitandao ya kijamii na vipeperushi ili kufikia malengo yake.