November 24, 2024

Udanganyifu wa mtihani darasa la saba kujirudia tena mwaka huu?

Maandalizi hafifu yatajwa kuchochea wanafunzi kutumia mbinu zisizo halali kufaulu mtihani.

  • Mwaka 2016 ndiyo ulikuwa na vitendo vingi vya udangajifu wa mitihani ikiwa ni zaidi ya mara 23 ya mwaka 2017.
  • Maandalizi hafifu yatajwa kuchochea wanafunzi kutumia mbinu zisizo halali kufaulu mtihani.
  • NECTA yatoa onyo kwa wasimamizi, walimu, wanafunzi kuzingatia kanuni za mitihani.

Dar es Salaam. Kesho ni siku ambayo wanafunzi wa darasa la saba nchini kote, wanafanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE), ikiwa ni sehemu ya kupima uelewa wao katika kipindi chote walipokuwa shuleni. 

Pia mtihani huo ni daraja la kuwawezesha kwenda elimu ya sekondari ambapo kujiunga kwao hutegemea ufaulu wa mwanafunzi. 

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Msonde, wanafunzi 947,221 wa darasa la saba kutoka shule 17,051 za Tanzania bara wanatarajia kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa siku mbili mfululizo

Wataanza kesho na na kumaliza Alhamisi Septemba 12, 2019 ambapo maandalizi yote yamekamilika tayari kuwawezesha wanafunzi kufanya mtihani huo. 

Kama ilivyo kawaida, kila mwaka  taarifa za vitendo vya udanganyifu  zimekuwa zikiripotiwa katika maeneo mbalimbali ambako mitihani inakofanyika, jambo linaloweza kusababisha wanafunzi kufutiwa matokeo na wahusika wa vitendo hivyo kuchukuliwa hatua za kisheria.

Lakini swali la kujiuliza vitendo vya udangajifu vitajitokeza tena mwaka huu? Kwa kiasi mifumo ya usimamizi wa mitihani iko imeimarishwa kuhakikisha kanuni za mitihani zinazingatiwa na wanafunzi wanapata alama kulingana na walivyojibu mtihani? 

Tukirejea miaka sita nyuma katika matokeo ya darasa la saba yaliyotolewa na NECTA tangu mwaka 2013 hadi 2017, kumekuwa na utofauti wa viwango vya udangajifu wa mitihani na kuleta mashaka kuendelea kwa vitendo hivyo katika mitihani inayokuja.   

Kimsingi udangajifu wa mitihani unahusisha wamiliki na walimu wa shule kuiba mitihani na kuwaandalia wanafunzi majibu, walimu na wasimamizi kuwasaidia wanafunzi kufanya mitihani na wanafunzi kuandika majibu yanayofanana isivyo kawaida au kuandika majibu hayo katika sare au sehemu mbalimbali za miili yao na kuingia nayo katika chumba cha mtihani.

Katika kipindi cha miaka sita, 2016 ndiyo ulikuwa gumzo kwa matukio mengi ya udanganyifu ambapo watahiniwa 238 kutoka shule sita tofauti walifutiwa matokeo kwa vitendo vya ukiukwaji wa kanuni za mitihani. 

Shule hizo ni Tumaini (Mwanza), Mihamakumi (Tabora), Qash (Manyara), St. Getrude (Ruvuma) na Little Flower (Mara). 

Mathalani, katika shule ya Tumaini wilaya ya Sengerema mkoa wa Mwanza, mmiliki wa shule aliandaa majibu ambayo watahiniwa waliandika kwenye sare za shule na kuingia nayo kwenye chumba cha mtihani lakini baadaye walikamatwa na kufutiwa matokeo.

Idadi hiyo ya wanafunzi waliofutiwa matokeo ni zaidi ya mara 23 ya waliofutiwa matokeo mwaka 2017 ambapo walikuwa wanafunzi 10 tu. 

Wakati udanganyifu huo ukitokea mwaka 2016, ilikuwa kipindi ambacho Serikali ilianza kutekeleza sera ya elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari ambapo iliongeza idadi kubwa ya wanafunzi shuleni na kuibua changamoto kadhaa ikiwemo mgawanyo usio sawa walimu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Hali hiyo ni tofauti na miaka iliyotangulia ambapo 2013 ni wanafunzi 13 pekee walifutiwa matokeo na mwaka uliofuata wa 2014 vitendo vya udanganyifu vilidhibitiwa zaidi na alipatikana  mwanafunzi mmoja tu .

Mtihani ni kipimo cha uelewa wa masomo kwa mwanafunzi. Picha| News Ghana

Hata hivyo, huenda vitendo vya udanganyifu vinaendelea kutokea bila kuripotiwa ikizingatiwa kuwa wanafunzi na walimu wanabuni njia mpya kila siku ili kutimiza malengo yao yaliyo kinyume na miongozo ya mitihani.

Zipo sababu mbalimbali ambazo zinachagiza wanafunzi na walimu kujiingiza katika udanganyifu ikiwemo wanafunzi kukosa maarifa ya msingi na maandalizi hafifu kuwawezesha kujibu mtihani na hivyo kutafuta njia ya mkato kufikia mafanikio ya elimu.

Kwa mujibu wa utafiti wa taasisi ya Hakielimu kwa mwaka 2012, jumla ya wanafunzi 5,200 walibainika kufaulu kujiunga kidato cha kwanza bila kujua kusoma wala kuandika.

Idadi hiyo iligundulika baada ya udanganyifu uliokuwa umejitokeza katika mtihani wa darasa la saba na kusababisha watoto 9,736 kufutiwa matokeo.

Kutokana na hali hiyo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliamuru wanafunzi wote wanaoripoti shuleni kwa kipindi hicho kupewa mtihani wa majaribio wa kupima uwezo wao wa kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).


Zinazohusiana:


Nayo ripoti ya taasisi ya Uwezo iliyo chini ya Twaweza ya mwaka 2015, inabainisha kuwa asilimia 16 ya watoto wa darasa la saba mwaka 2014 walihitimu bila kuwa na uwezo wa kusoma mafunzo ya hadithi rahisi ya Kiswahili ya darasa la pili.

Ripoti hiyo inaonyesha pia kuwa asilimia 23 ya wanafunzi waliohitimu darasa la saba hawakuwa na uwezo wa kufanya hesabu rahisi za kiwango cha darasa la pili.

Serikali  kukabiliana na vitendo vya udangajifu wa mitihani

Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limeonya kuhusu vitendo vyovyote vya udanganyifu na kwamba yeyote atakayegundulika atachukuliwa hatua kali.

NECTA imewaasa wasimamizi, watahiniwa, walimu, wamiliki wa shule na wananchi wote  kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu  na kwamba watahiniwa watakaobainika watafutiwa matokeo yao.

Pia kuwa haitasita kukifuta kituo chochote cha mtihani endapo itajiridhisha kuwa kuwapo kwake kunahatarisha usalama wa mitihani ya taifa.

“Kamati zote za mitihani za mikoa, halmashauri na manispaa nchini zinatakiwa kuhakikisha kwamba taratibu zote zinazohusika na uendeshaji wa mitihani ya Taifa zinazingatiwa ipasavyo. 

“Kamati zote zinaagizwa kuhakikisha mazingira yote ya vituo vya mitihani yako salama, tulivu kuwawezesha watoto wetu kufanya mitihani kwa amani kabisa,” amesema Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Charles Msonde.

Dk Msonde amesema tahadhari hiyo inatoa  matarajio kwamba wanaohusika, wakiwamo wanafunzi, walimu, wasimamizi na vituo, watazingatia misingi ya iliyowekwa na NECTA hivyo kamati zihakikishe mazingira ya mitihani hayaruhusu udangajifu wowote kutokea.