October 7, 2024

Ufanye nini kukabiliana na habari ya kutungwa?

Habari hizo ni zile ambazo hazina ukweli wowote.

  • Habari hizo ni zile ambazo hazina ukweli wowote
  • Mara nyingi hutengenezwa kwa nia ovu ya kupotosha watu.
  • Kuzishinda ni kupata elimu ya uthibitishaji habari.

Dar es Salaam. Kama zipo za kweli, basi na za kutungwa zipo. Kwa nini watu watunge habari? Sababu ziko nyingi ikiwemo kujipatia fedha.

Habari za kutungwa (Fabricate content) ni habari ambayo kwa asilimia 100 ni ya uongo. Hutumika zaidi kudanganya au kusambaza uzushi kuhusu matukio ya kweli yanayotokea likiwemo janga la Corona (COVID-19).

Habari hizo ambazo hutengenezwa na kusambazwa kwa njia mbalimbali ikiwemo akaunti za mitandao ya kijamii, tovuti au hata habari picha au video.

Kitendo hicho hutafsiriwa kama upotoshaji ambapo mtu hubuni habari ambayo haipo au haijaripotiwa kabisa.

Mathalan, kabla Tanzania haijaripoti mgonjwa wa kwanza wa Corona Machi 16, 2020, mtandao wa mcmnt.com ulitunga habari ya uongo na kuichapisha  Machi, 10 2020 kwa lugha ya Kiingereza iliyosema “BREAKING NEWS: Tanzania confirms first case of Coronavirus” (Habari zilizotufikia hivi sasa:Tanzania yathibitisha kupata mgonjwa wa kwanza wa Corona)


Zinazohusiana


Habari hiyo ilikua ni ya uongo kwa sababu Tanzania ilikua bado haijaripoti hata mgonjwa mmoja wa COVID-19 wakati huo.

Wakati mwingine wasambazi wa aina hii ya habari huweza kutengeneza video za uzushi kwa kutumia teknolojia ya ‘deepfake’.

Ni rahisi sana kuzitambua habari za namna hiyo. Kwanza zinaambatana shinikizo la kumtaka mtu kusambaza kwa watu wengine au kufanya jambo fulani ambalo usipifikiria linaweza kumuingiza kwenye matatizo ikiwemo kutapeliwa au kudhurika kiafya.

Zipo jitihada zinazofanywa na mashirika na taasisi mbalimbali kukabiliana na uzushi unaohusu Corona ikiwemo  kampeni ya #NuktaFakti ambayo huthibitisha habari hizo kwa kutumia zana za kidijitali ili kuilinda jamii na madhara.

Kujifunza zaidi kuhusu zana hizo tembelea tovuti ya Nukta Habari (www.nukta.co.tz) au mitanda ya kijamii ya Facebook na Twitter: @NuktaFakti au Instagram: @nuktafakti.