October 6, 2024

Uganda yawasamehe wafungwa zaidi 800 kuwanusuru na Corona

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewasamehe na kuwachilia huru wafungwa 833 ili kupunguza msongamano magerezani wakati baadhi ya nchi za Ulaya zikilegeza masharti yaliyowekwa kuzuia kusambaa maambukizi ya ugonjwa wa Corona (COVID-19).

  • Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewasamehe na kuwachilia huru wafungwa 833 ili kupunguza msongamano magerezani.
  • Hiyo itasaidia kuwapa nafasi wafungwa kukaa katika maeneo salama dhidi ya maambukizi ya Corona.
  • Baadhi ya nchi za Ulaya zimeanza kulegeza masharti yaliyowekwa kuzuia kusambaa maambukizi  ya ugonjwa wa COVID-19.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewasamehe na kuwachilia huru wafungwa 833 ili kupunguza msongamano magerezani wakati baadhi ya nchi za Ulaya zikilegeza masharti yaliyowekwa kuzuia kusambaa maambukizi  ya ugonjwa wa Corona (COVID-19). 

Awali Jeshi la Magereza nchini humo lilipendekeza zaidi ya wafungwa 2,000 waachiwe ili kupata nafasi ya kumuwezesha kila mfungwa akae katika eneo salama la kutoambukizwa virusi vya corona. 

Miongoni mwa wale walio kwenye orodha ya kuachiwa ni wafungwa wenye makosa madogo na pia wale waliokaribia kukamilisha vifungo vyao. 

Baadhi ya watetezi wa haki za binadamu nchini humo akiwemo Nicholas Opiyo waliwasilisha  ombi kwa serikali kuhakikisha usalama wa wafungwa magerezani ili kuwaepusha kuambukizwa virusi vya COVID-19.

Magereza ni miongoni maeneo yaliyo na mkusanyiko mkubwa wa watu kama vile shule na taasisi za elimu zilizofungwa mwezi Machi.

Mpaka sasa Uganda ina wagonjwa 79 wa Corona.


Zinazohusiana:


Aidha, Baadhi ya mataifa ulimwenguni yameanza kulegeza masharti yaliyowekwa ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya COVID-19, na sasa yanalenga kushughulikia uchumi ulioathiriwa na janga hilo. 

Duru za habari za kimataifa zinaeleza kuwa nchi nyingi za Ulaya zinafungua viwanda pamoja na maeneo ya ujenzi ili kuwaruhusu watu kuendelea na shughuli za uzalishaji.

Nchini New Zealand, watu wataweza kununua vyakula vya kubeba kutoka katika migahawa ambayo itaanza kufunguliwa usiku wa leo. 

Hata hivyo, baadhi ya watu wana wasiwasi kuwa kuanza kulegeza masharti hayo mapema, kunaweza kusababisha virusi vya corona kuanza tena kusambaa kwa kasi.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) jumla ya watu milioni 2.8 ulimwenguni kote wameambukizwa virusi hivyo hadi jana Aprili 26. 

Idadi ya waliokufa kutokana na ugonjwa huo wa COVID-19 ni 193,710.