July 8, 2024

Uhaba wa mbegu unavyokwamisha kilimo cha mkonge Tanzania

Huenda mkakati wa Serikali kufufua zao la mkonge ukatumia muda mrefu kukamilika, baada ya uzalishaji wa mbegu bora kutoendana na mahitaji ya wakulima ambao wanawekeza katika zao hilo la biashara.

  • Mahitaji halisi kwa mwaka ni mbegu milioni 1.6 lakini uwezo wa uzalishaji ni mbegu 500,000.
  • Serikali yasema itakiongezea nguvu kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) cha Mlingano mkoani Tanga kuzalisha mbegu nyingi.
  • Wakulima watakiwa kuchangamkia fursa ya kilimo hicho. 

Dar es Salaam. Huenda mkakati wa Serikali kufufua zao la mkonge ukatumia muda mrefu kukamilika, baada ya uzalishaji wa mbegu bora kutoendana na mahitaji ya wakulima ambao wanawekeza katika zao hilo la biashara. 

Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, mkonge ni miongoni mwa mazao ya mkakati ambayo Serikali ya awamu ya tano ilianza kuyatilia mkazo ili kuimarisha uzalishaji wake, upatikanaji wa pembejeo na masoko ya ndani na kimataifa. 

Mkuu wa kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) cha Mlingano kilichopo Muheza mkoani Tanga Dk Catherine Senkoro amesema uzalishaji wa mbegu mpya za mkonge zenye uwezo mkubwa wa mavuno umefikia mbegu 500,000 kati mahitaji ya wakulima ya mbegu milioni 1.6 kwa mwaka.

Hiyo ina maana kuwa kuna upungufu wa uzalishaji mbegu milioni 1.1 au theruthi mbili ya mahitaji jambo linaloweza kuwaletea changamoto wakulima wanaotaka kuwekeza katika zao hilo. 

Hata hivyo, Dk Senkoro amesema kwa sasa wana mkakati wa kuzalisha mbegu bora za mkonge kwa kutumia teknolojia ya maabara na vipando itakayosaidia kuongeza idadi ya mbegu na kuweza kufikia lengo la kuzalisha mbegu milioni 2 ifikiapo mwaka 2021.

Dk Senkoro alikuwa akitoa taarifa ya uzalishaji wa mbegu za mkonge Aprili 27, 2020 mbele ya  Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipoongea na watumishi wa TARI na wale wa Chuo cha Mafunzo  Kilimo (MATI) wilayani Muheza Mkoa wa Tanga.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya akipata maelezo ya namna mbegu bora za mkonge zinavyozalishwa kwenye vitalu kwa njia ya maabara.Kulia ni Mtafiti wa zao la mkonge Gelleson Mkongwe wa kituo cha TARI Mlingano akitoa maelezo. Picha| Wizara ya Kilimo. 

Kwa mujibu wa Dk Senkoro kwa sasa ekari moja inazalisha tani moja ya mkonge wakati China wanazalisha tani tano kwa ekari, mara tano zaidi ya uwezo wa ekari moja Tanzania.

Mtaalamu huyo amesema kuwa taasisi hiyo inahitaji kuongezewa nguvu ili izalishe mbegu bora zenye kutoa matokeo makubwa kwa wakulima.


Zinazohusiana:


Kusaya ameitaka TARI kuhakikisha inazalisha mbegu 5,000,000 kwa mwaka na kuwa wizara yake itatoa fedha za kuwezesha utafiti na uboreshaji maabara ya kupima afya ya udongo na ile ya kuzalisha mbegu bora za mkonge.

“Wizara ya Kilimo ipo tayari kusaidia kituo hiki kupata fedha za kutosha ili kuzalisha mbegu bora za mkonge na kuwafikia wakulima wengi zaidi kama alivyoagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati alipotembelea kituo hiki Machi mwaka huu” amesema Kusaya katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Kilimo.

Kusaya alisema ni wakati muafaka sasa watafiti wa zao la mkonge kujikita katika kutoa matokeo chanya ya mbegu kwani kuna maeneo mengi nchini kama wilaya za Kahama, Kishapu, Kilosa na Geita wameonesha nia ya kuanzisha mashamba ya mkonge.

Hata hivyo, kuna matumaini makubwa katika zao hilo, ikizingatiwa kuwa uzalishaji wake unaongezeka kila mwaka, ikiwa wakulima watapata mbegu bora, teknolojia ya kisasa na masoko ya uhakika.  

Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018, kinaeleza kuwa uzalishaji wa zao uliongezeka kwa asilimia 11.2 hadi tani 40,635 mwaka juzi kutoka tani 36,533 mwaka 2017.