Uhaba wa watumishi wazitafuna taasisi 55 za Serikali Tanzania
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amebaini upungufu wa watumishi 9,691 katika taasisi za Serikali zikiwemo wizara tano, jambo linaathiri ufanisi wa kazi na kuwachosha watumishi wachache waliopo katika taasisi hizo.
- Zipo wizara tano na balozi 15 zinazoiwakilisha nchi mbalimbali duniani
- CAG Kichere amesema upungufu wa watumishi unaathiri ufanisi wa kazi na kuwachosha watumishi wachache waliopo katika taasisi hizo.
- Abaini pia uwepo wa taasisi zenye watumishi wengi kuliko mahitaji.
Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amebaini upungufu wa watumishi 9,691 katika taasisi za Serikali zikiwemo wizara tano, jambo linaloathiri ufanisi wa kazi na kuwachosha watumishi wachache waliopo katika taasisi hizo.
Licha ya upungufu huo wa watumishi, katika ukaguzi wake wa mwaka wa fedha wa 2018/2019, Kichere amebaini uwepo wa taasisi za umma zenye watumishi wa ziada kuliko mahitaji yaliyopo.
Katika ripoti ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 kuhusu Serikali Kuu iliyochapishwa hivi karibuni, CAG Kichere ameeleza kuwa katika mapitio yake amegundua upungufu wa watumishi 9,691 katika taasisi za Serikali jambo ambalo linaendelea kuwa kikwazo katika utoaji wa huduma serikalini.
Upungufu huo wa watumishi umejitokeza katika wizara tano, sekretarieti za mikoa (13), tume na taasisi zingine (22) na balozi 15 zinazoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali.
Pamoja na kuwepo upungufu huo, tatizo hilo limeendelea kupungua mfululizo tangu mwaka 2016/2017 kutokana jitihada za Serikali kuajiri watumishi wapya kuongeza ufanisi wa utendaji.
“Katika taarifa yangu ya mwaka 2017, kulikuwa na taasisi 52 zenye upungufu wa watumishi 34,083, mwaka 2018 upungufu wa watumishi ulikuwa 9,755 katika taasisi 61, huku mwaka huu ukisalia upungufu wa watumishi 9,691 katika taasisi 55,” amesema CAG Kichere.
Aidha, CAG Kichere amesema wakati anapitia ikama ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imemuonyesha kuwa kuna watumishi wa ziada 134 baada ya kulinganisha mahitaji ya watumishi 504 na 638 ya waliokuwepo katika orodha ya malipo ya mshahara wa mwezi wa sita mwaka 2019.
“Nikilinganisha na taarifa zangu mbili zinazofuatana na mwaka huu wa ukaguzi inaonekana kuwa suala hili linashughulikiwa, kwani idadi ya taasisi na upungufu wa watumishi unaendelea kupungua taratibu,” amesema Kichere katika ripoti hiyo.
Soma zaidi:
- CAG: HESLB imeshindwa kuwapata wadaiwa wa Sh1.46 trilioni
- Bunge lamtenga rasmi CAG Assad
- CAG hajaiacha salama sekta ya utalii, aibua utofauti wa takwimu za watalii
Amesema kuwepo kwa taasisi zenye watumishi wa ziada na zingine zenye upungufu kunamaanisha kuwa Serikali haijafanya tathmini sahihi ya kuoanisha mahitaji ya watumishi kulingana na shughuli za taasisi hivyo kushindwa kupangilia watumishi kulingana na mahitaji.
Kuendelea kwa tatizo hili kunaendeleza athari ya kutokuwepo kwa ufanisi katika utendaji wa taasisi katika utoaji wa huduma, mlundikano wa kazi na kuchosha watumishi wachache waliokuwepo.
“Bado naendelea kuwashauri maafisa masuuli washirikiane na Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kufanya tathmini ya mahitaji ya watumishi kulingana na shughuli za taasisi kisha upungufu wa watumishi ushughulikiwe,” inasomeka sehemu ya mapendekezo ya CAG Kichere.
Aidha, CAG amesema ukaguzi wa malipo ya mishahara alioufanya katika Jeshi la Polisi ulionyesha kiasi cha Sh196.2 milioni kililipwa kwa watumishi 11 ambao walikwishafariki, kufukuzwa na kustaafu.