October 6, 2024

Uhamiaji kuanza kutoa vibali vya ukaazi vya kielektroniki

Hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa vibali hivyo kwa raia wa kigeni na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi nchini.

  • Hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa vibali hivyo kwa raia wa kigeni na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi.
  • Idara ya Uhamiaji inatarajia kuanza kutoa huduma tajwa kwa raia wa kigeni muda wowote kuanzia sasa ambapo raia wa kigeni wataweza kuomba vibali hivyo kwa njia ya kielektroniki wakati wowote na mahali popote walipo.
  • Matumizi ya mifumo hiyo itaongeza ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa kuwa mteja ataweza kulipia huduma hizo mwenyewe moja kwa moja pasipo kupitia kwa mawakala au mtu yeyote.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua huduma za viza na vibali vya ukaazi vya kielektroniki na amewataka watu wote watakaopewa vibali hivyo kutii sheria kwa kufanya shughuli ambazo wameelekezwa kwa mujibu wa vibali vyao na si vinginevyo.

Amesema utoaji wa huduma hizo ni miongoni mwa jitihada za Serikali katika kuvutia uwekezaji, hususan katika sekta ya viwanda kwani hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa vibali hivyo kwa raia wa kigeni na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi.

Majaliwa aesema hayo Novemba 26, 2028 wakati akizindua huduma za viza na vibali vya ukaazi vya kielektroniki katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam ambapo hatua hiyo itasaidia kuondoa urasimu na ucheleweshwaji wa huduma pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.

Idara ya Uhamiaji inatarajia kuanza kutoa huduma tajwa kwa raia wa kigeni muda wowote kuanzia sasa na kwa kupitia huduma hiyo, raia wa kigeni wataweza kuomba vibali hivyo kwa njia ya kielektroniki wakati wowote na mahali popote walipo.

Majaliwa amesema watakaopewa vibali hivyo wanatakiwa kufanya shughuli zao kwa mujibu wa vibali vyao kwa sababu kufanya shughuli tofauti na ilivyoainishwa kwenye kibali ni kosa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Uhamiaji.


Zinazohusiana: Teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi wa matibabu Muhimbili


Amesema matumizi ya mtandao katika utoaji wa huduma za viza na vibali vya ukaazi ni hatua ya mfano, kwani inakwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na sera ya Serikali ya matumizi ya TEHAMA katika shughuli za Serikali (e-government).

Matumizi ya mifumo hiyo itaongeza ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa kuwa mteja ataweza kulipia huduma hizo mwenyewe moja kwa moja pasipo kupitia kwa mawakala au mtu yeyote.

“Natoa wito kwa Maafisa, Askari pamoja na Watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji kuhakikisha kuwa mifumo hiyo inatunzwa pamoja na kuendeleza miundombinu yote ya kiutendaji,” amesema Majaliwa.

Amesema mfumo wa huduma hizo utaunganishwa na mifumo mingine ya Serikali, ambayo inatoa huduma kwa wananchi na wageni kama vile mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Idara ya Kazi – Ofisi ya Waziri Mkuu, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mfumo wa Malipo ya Serikali Kimtandao (GePG).