October 6, 2024

Uhamiaji waeleza chanzo cha kuwakamata wafanyakazi wa CPJ

Idara ya uhamiaji imesema wafanyakazi hao walikuwa nchini kwa ajili ya matembezi lakini walianza kufanya mikutano na wanahabari “kinyume na sheria.”

  • Uhamiaji wameeleza kuwa wafanyakazi hao wa CPJ walikuwa wakifanya mikutano na wanahabari kinyume na sababu za wao kuingia nchini.
  • Imesema kuwa Quintal na Mumo wamerejeshewa pasi zao za kusafiria 

Dar es Salaam. Idara ya uhamiaji nchini imesema imewarudishia pasi za kusafiria wafanyakazi wawili wa Kamati ya Kutetea Wanahabari Duniani (CPJ) baada ya kuwashikilia kwa muda “kutokana na kuvunja sheria za uhamiaji.”

Mratibu wa Programu wa Afrika Angela Quintal na Mwakilishi wa kamati hiyo ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, Muthoki Mumo walikamatwa jana jioni wakiwa hotelini walikofikia na kunyang’anywa pasi za kusafiria, CPJ wameeleza katika taarifa yao.

Msemaji Mkuu wa idara hiyo, Ali Mtanda ameiambia Nukta kuwa baada ya kufuatilia kwa kina wamebaini kuwa Quintal na Mumo walikamatwa jana Saa mbili usiku kutokana na kufanya mikutano na wanahabari kinyume na masharti ya vibali vyao vya kuwapo nchini.

Mtanda amesema wafanyakazi hao wa CPJ ambao pia ni wanahabari walikuwa na kibali cha siku 90 cha matembezi kinachoisha Januari 2019 lakini hakikuwa kikiruhusu mikutano.

“Baada ya mahojiano na maofisa wetu baadaye walieleza kuwa lengo lao jingine ni kufanya mikutano na wanahabari. Sasa hivyo ilikuwa kinyume na sheria ya uhamiaji sura ya 54 ambayo hairuhusu kubadilisha ‘status’ ya kazi uliyojia.

“Pia, ‘profession’ (taaluma) yao ya uanahabari ilikuwa inataka wafuate taratibu nyingine za nchi kama kwenda Habari Maelezo na kupata ‘press cards’ (vitambulisho vya wanahabari)…lakini hawakufanya hivyo,” amesema Mtanda.


Zinazohusiana: CPJ wadai wafanyakazi wao wawili wanashikiliwa Tanzania


Baada ya mahojiano hayo, Mtanda amesema Mumo na Quintal waliachiwa huru lakini pasi zao za kusafiria zilishikiliwa kwa muda kwa ajili ya uchunguzi wa nia halisi ya kuingia nchini na iwapo walifahamu ukiukwaji huo wa sheria ama la.

Hata hivyo, amesema leo wamewapatia elimu ya namna walivyotakiwa kufanya ikiwemo kufuata sheria na taratibu za nchi kabla ya kufanya mikutano hiyo.

“Tumewapa elimu na kuwarudishia ‘passport’ zao mbele ya mabalozi wa nchi zao,” amesema Mtanda na kuongeza “kama wanataka kubaki nchini kuongea na wanahabari ni juu yao kwa kuwa bado wana siku nyingi za kuwepo nchini ila wafuate taratibu zinazotakiwa ikiwemo kupata vibali vya kufanya hivyo.”

Katika taarifa yao, CPJ wameeleza kuwa Mumo ambaye ni raia wa Kenya na Quintal kutoka Afrika Kusini walikuwa nchini kikazi na waliingia kihalali.