Uhamiaji waeleza sababu za kuendelea kumshikilia Mwanahabari Kabendera
Idara ya Uhamiaji imesema itaendelea kumshikilia na kumuhoji ili ipate taarifa sahihi za uraia wake.
- Idara ya Uhamiaji imesema itaendelea kumshikilia na kumuhoji ili ipate taarifa sahihi za uraia wake.
- Imesema kukamatwa kwa Kabendera siyo jambo geni kwa sababu wanatimizi matakwa ya sheria.
Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji Tanzania imesema bado wanamshikila na kumuhoji Mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera ili wapate taarifa sahihi kuhusu uraia wake.
Kabendera ambaye anaandikia magazeti ya ndani na nje ya nchi alichukuliwa kwa nguvu nyumbani kwake Mbweni Jijini Dar es Salaam Julai 29, 2019 na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi.
Jana, Julai 30, 2019, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema Kabendera hakutekwa lakini anashikilikiwa na polisi akisubiri kukabidhiwa kwa maofisa wa Uhamiaji.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Uraia na Pasipoti wa Idara ya Uhamiaji, Gerald Kihinga amesema Kabendera anashikiliwa na Jeshi la Polisi na Uhamiaji kwa mahojiano zaidi ili kuweza kupata taarifa juu ya uraia wake.
Soma zaidi: Polisi Tanznaia yakiri kumshikilia Mwanahabari Kabendera
Amesema Idara ya Uhamiaji ina dhamana ya kusimamia na kutekeleza Sheria ya Uraia wa Tanzania sura ya 357 rejeo la 2002, inayotoa mamlaka kwa taasisi hiyo kuchunguza na kuthibitisha uraia wa mtu yeyote.
“Idara ya Uhamiaji ni chombo kilichopewa dhamana kubwa ya kutekeleza na kusimamia uraia wa Tanzania, kwa hiyo siyo mara ya kwanza kufanya hivyo, sisi tunamshikilia Kabendera kwa mahojiano kuhusu uraia wake, na siyo yeye tu aliyefanyiwa hivyo, idara ya Uhamiaji inatimiza matakwa ya sheria ya uraia nchini na wala si vinginevyo,” amesema Kamishna Kihinga.
Ameeleza kuwa Idara ya Uhamiaji ilipata taarifa za Kabendera kutoka kwa raia wema na ikaamua kumtafuta ili kufanya naye mahojiano lakini hakuwa tayari kutoa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kukataa kufika ofisi za Uhamiaji, hali iliyopelekea kukamatwa na sasa anaendelea kuhojiwa.
Amesema kumekuwa na ushirikiano baina ya Uhamiaji na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ikwemo Polisi, ili kutekeleza majukumu mbalimbali ya kiusalama kwa nchi hivyo kukamatwa kwa Kabendera siyo jambo geni bali Idara inatimiza majukumu yake yaliyopo kisheria.