October 6, 2024

Uhamisho wa wanyamapori unavyoweza kuzifaidisha hifadhi za wanyama Tanzania

Wataalam wasema lengo la kuhamisha wanyamapori kwenda sehemu nyingine ni kuendeleza vizazi vya wanyama hao ili waendelee kuishi na kuleta faida kwa mazingira na Taifa hasa katika sekta ya utalii.

Kuendelea kuishi kwa wanyamapori katika mazingira mapya waliyohamishiwa kunategemea mambo mbalimbali ikiwemo mazingira waliyozoea kuishi awali. Picha|Mtandao.


  • Wataalam wasema wakihamishwa kwa kuzingatia taratibu nzuri watasaidia uhifadhi wao kuwa endelevu.
  • Mnyama anaweza kufa katika mazingira mapya kama atakosa furaha ya wanafamilia.
  • Wengine wabainisha kuwa uhamisho wanyamapori uzingatie utunzaji wa mazingira.

Dar es Salaam. Kufuatia uhamisho wa wanyamapori kutoka hifadhi moja kwenda nyingine unaofanywa na Serikali, wataalam wa wanyamapori wameeleza kuwa jambo hilo siyo baya lakini yapo mambo ya msingi yanayotakiwa kuzingatiwa ikiwemo tabia za viumbe hao ili kuviwezesha kuendelea kuishi katika mazingira mapya. 

Mapema Februari mwaka huu simba 17 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti walihamishiwa hadi katika hifadhi mpya ya Taifa ya Burigi-Chato ambayo ilianzishwa mwaka 2019.

Huo ni muendelezo wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) kuwapeleka wanyama katika hifadhi hiyo ili kuiongezea vivutio vitakavyochagiza sekta ya utalii kanda ya Ziwa hasa mkoa wa Geita. 

Mtaalam wa wanyamapori kutoka Idara ya Ziolojia na Uhifadhi Wanyamapori ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) Dk Elikana Kalumanga ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa lengo la kuhamisha wanyamapori kwenda sehemu nyingine ni kuendeleza vizazi vya wanyama hao ili waendelee kuishi na kuleta faida kwa mazingira na Taifa hasa katika sekta ya utalii.

Amesema kuendelea kuishi kwa wanyamapori katika mazingira mapya waliyohamishiwa kunategemea mambo mbalimbali ikiwemo mazingira waliyozoea kuishi awali. 

“Kwa mfano ukimtoa mnyama aliyezoea kuishi kwenye misitu minene kama Selous (hifadhi ya Taifa) halafu ukampeleka kwenye hali ya hewa ya kitropiki (Savannah) ambako kuna hali ya ukame, anaweza akafariki,” amesema Dk Kalumanga wakati wa mafunzo ya wanahabari kuripoti habari za wanyamapori na utalii jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Mafunzo hayo maalum yaliandaliwa na Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) wakishirikiana na USAID-Protect yanalenga kuwezesha uzalishaji wa habari zinazohusu wanyama pori na utalii, zenye mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa na vyombo vya habari husika.

Mtaalam huyo amesema wanaohamisha wanyamapori ni muhimu wasome tabia na hisia za wanyama hao kama zinazendana na mazingira mapya watakayoishi muda uliobaki.

Kwa mujibu wa Dk Kalumanga ambaye pia ni mshauri wa masuala ya wanyamapori, kinachoweza kumuua mnyama katika mazingira mapya ni kukosa furaha na kampani ya wenzake. 

“Ukimpeleka katika mazingira mapya, wanyama wengine watamuona ni mgeni na watamkimbia. Kwa hiyo utajisikia huzuni na kukosa furaha aliyoizoea,” amesema.

Ili kuhakikisha wanyama hao wanaishi vizuri katika mazingira mapya, amesema inashauriwa wahamishwe familia yote na siyo mnyama mmoja mmoja, jambo litakalowasaidia kujiona bado wako wamoja na wanaweza kuendelea kuzaliana. 


Soma zaidi: 


Tathmini ya upatikanaji wa chakula kule wanakopelekwa nayo inatakiwa ifanyike kwa sababu vipo baadhi ya vyakula ambavyo mnyama anakiwa avipate ili aendelee kuishi.

Kalumanga amesema baadhi ya wanyama kama tembo wamezoea kula udongo ambao unawasaidia kupata madini joto na “calcium” ambapo wakihamishiwa kwenye eneo ambalo hayapatikani wanaweza kurudi walikotoka hata kama ni mbali. 

“Wanyama nao wanapata magonjwa, katika mazingira mapya lazima uangalie uwezo wa mnyama unayemwamisha kustahimili magonjwa ambayo yamekuwa hatari katika eneo husika,” amesisitiza Dk Kalumanga.

Wanyamapori wamekuwa sehemu muhimu ya uhifadhi wa mazingira na ukuaji wa sekta ya utalii kwa sababu wageni kutoka nje wamekuwa wakitembelea hifadhi za Taifa kujionea fahari ya Tanzania. 

Ripoti ya utafiti wa wageni wa nje ya nchi mwaka 2017 (International Visitors’ Exit Survey Report 2017) inaonyesha kuwa mbuga za wanyama na fukwe ndiyo zinaongozwa kwa kutembelewa zaidi na watalii wanaokuja Tanzania.

Maeneo hayo mawili yanachukua asilimia 58.2 ya maeneo yote yaliyotembelewa na watalii nchini mwaka 2017, jambo ambalo linafungua milango kwa wadau kuweka mikakati thabiti ya kuboresha sekta ya wanyamapori.

Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) Dk Ellen Otaru ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz)  uhifadhi wa wanyamapori hautafanikiwa nakuleta tija kwa Taifa ikiwa wadau mbalimbali hawataunganishwa nguvu na kufanya kazi kwa pamoja ili kubaini changamoto zilizopo.

Amesema changamoto kubwa zinazokwamishwa uhifadhi endelevu wa wanyamapori ni mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame, ongezeko la idadi ya watu, shughuli za ujenzi wa miundombinu na uelewa mdogo wa jamii kuhusu mahusiano ya binadamu na wanyamapori katika kuendeleza mazingira.

Aidha, amesema suluhisho ni kuondoa pengo la utendaji wa taasisi za Serikali kwa sababu mazingira na wanyamapori vinagusa wizara mbalimbali ambazo zinahitaji kuwa na mawasiliano mazuri ya utekelezaji wa shughuli zao ili zisiathiri ustawi wa wanyama hao.