July 8, 2024

Ujenzi bandari kuimarisha biashara ya uvuvi Tanzania

Serikali ya Tanzania inakusudia kujenga bandari moja ya uvuvi itakayosaidia kuongeza kasi ya uvuvi wa kisasa na biashara ya samaki ili kujipatia mapato na kuboresha maisha ya wananchi wanaotegemea sekta hiyo.

  • Bandari hiyo itakuwa inapokea meli za uvuvi na kuchagiza biashara ya samaki nchini.
  • Itajengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Korea Kusini. 
  • Inaweza kujengwa Bagamoyo, Kilwa Masoko au katika bandari ya Lindi.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inakusudia kujenga bandari moja ya uvuvi itakayosaidia kuongeza kasi ya uvuvi wa kisasa na biashara ya samaki ili kujipatia mapato na kuboresha maisha ya wananchi wanaotegemea sekta hiyo. 

Takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi za mwaka 2020 zinaonyesha kuwa wingi wa samaki katika maji ya Tanzania umefikia tani milioni 3.3 mwaka 2019/2020 kutoka tani milioni 2.8 za mwaka 2018/2019. 

Licha ya wingi wa rasilimali hiyo muhimu, bado kiwango cha samaki wanaovunwa kila mwaka hakifiki hata robo ya samaki waliopo majini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo matumizi ya teknolojia duni. 

Mathalan, mwaka huu wa 2019/2020 ni tani 392,933 za samaki zenye thamani ya Sh1.85 trilioni ndiyo zilivuliwa na wavuvi. 

Hali hiyo inaweza kubadilika baada ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luaga Mpina kueleza kuwa Serikali iko katika mchakato wa kujenga bandari ya uvuvi ambayo itakuwa inaruhusu meli kubwa za uvuvi kutia nanga. 

“Wizara inaendelea kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya uvuvi kupitia mtaalam mwelekezi ambaye ni kampuni ya M/S Sering Ingegneria ya chini Italia kwa gharama ya Sh1.5 bilioni,” amesema Mpina Alhamis hii wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2020/2021.


Zinazohusiana:


Amesema maeneo matatu ya Mbegani- Bagamoyo, Kilwa Masoko na Bandari ya Lindi yamependekezwa ambapo eneo moja kati ya hayo litachaguliwa kwa ajili ya ujenzi. 

“Mazungumzo yanaendelea baina ya Serikali ya Tanzania na Korea ya Kusini kwa ajili ya kupata ufadhili wa ujenzi wa bandari ya uvuvi katika eneo litakalopendekezwa,” amesema waziri huyo.Katika mwaka 2020/2021, Serikali itakamilisha upembuzi wa kina na kuanza ujenzi wa bandari hiyo katika eneo litakalochaguliwa.

Sambamba na hilo Serikali inakusudia kutekeleza mradi wa uvuvi utakaojumuisha ujenzi wa meli ya uvuvi wa Mishipi (Longliner), meli ya uvuvi wavu wa kuzungusha (Purse Seiner), na meli ya uvuvi wa maji ya ndani (Territorial Waters Fishing Vessel) ambazo zitatumika kuvua samaki baharini.

Mpina amesema kuwepo kwa bandari ya uvuvi kutawezesha ukuaji wa biashara ya mazao ya uvuvi, kuongeza ajira, kuchochea uwekezaji na ujenzi wa viwanda, kuongeza fedha za kigeni, kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la Taifa na hivyo kuiwezesha nchi kunufaika kikamilifu na rasilimali za uvuvi. 

Mwaka 2019, sekta ya uvuvi ilichangia asilimia 1.7 ya pato la Taifa na ilikua kwa asilimia 1.5, chini ya wastani wa ukuaji wa uchumi wa Taifa wa wastani wa asilimia saba. 

Sekta ya Uvuvi huchangia katika kuwapatia wananchi uhakika wa chakula, lishe, kuongeza kipato, fedha za kigeni na kupunguza umaskini huku makadirio ni kuwa zaidi ya Watanzania milioni 4.5 wanategemea shughuli zinazohusiana na uvuvi.