November 24, 2024

Ujenzi reli ya kisasa kupaisha utalii Morogoro

Rais Magufuli amesema reli ya kisasa inayojengwa kati ya jiji la Dar es Salaam na Jiji la Dodoma itavutia watu wengi kutembelea kwa matukio mbalimbali ikiwemo kupiga picha.

  • Rais Magufuli amesema reli hiyo itavutia watu wengi kutembelea kwa matukio mbalimbali ikiwemo kupiga picha. 
  • Awataka Watanzania kujenga hoteli na kuanzisha shughuli za utalii katika maeneo hayo. 
  • Ameagiza Wizara ya Ardhi ishirikiane na viongozi wa mkoa huo kuanzisha korido za kiuchumi kuvutia wawekezaji. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewataka viongozi na wananchi wa Mkoa wa Morogoro kutumia vizuri miradi ya kimkakati ikiwemo reli ya kisasa mkoani humo kuendeleza shughuli za utalii ili kujipatia mapato. 

Kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) kutoka jijini Dar es Salaam hadi jijini Dodoma na baadaye itaunganisha nchi za Rwanda na Burundi. 

Moja ya miundombinu ya reli inayojengwa ni mahandaki manne yaliyopo kati ya Morogoro na Makutupora jijini Dodoma ambayo yakitumika vizuri yanaweza kuinua sekta ya utalii Tanzania. 

Dk Magufuli akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mahandaki hayo na uzinduzi wa barabara ya lami ya Rudewa – Kilosa mkoani Morogoro amesema miundombinu hiyo ni rasilimali muhimu kwa ukuaji wa sekta ya utalii.

“Wapo watu watakuja kupiga picha hapa hasa watani zangu wa Morogoro. Wapo watu wa kila aina watakuja hapa. Kwa hiyo Wilaya ya Morogoro, Wilaya ya Kilosa, tumefungua fursa ya utalii.” amesema Rais Magufuli.


Zinazohusiana:


Kiongozi huyo wa nchi amewasihi wakazi wa mkoa huo kuitumia miradi ya reli kujiletea maendeleo kwa kuanzisha huduma za utalii kwa sababu watu watakaotembelea katika maeneo hayo watapeleka pesa.

“Muanze kutengeneza mianya ya kuvuta hizo pesa, mwenye uwezo wa kujenga hoteli, ajenge,” amesisitiza Rais Magufuli.

Aidha, Rais ameiagiza  Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wizara zinazohusika kushirikiana na viongozi wa Morogoro kuanzisha korido za kiuchumi ili kuvutia wawekezaji mkoani humo.

“Kama ni mashamba yafunguliwe mengi ya kutosha. Mtalima matunda, yatasafirishwa mpaka Ulaya… Viongozi wote wanaohusishwa na migogoro ya mashamba muitatue kwa kumtanguliza Mungu mbele,” amesema Rais Magufuli


Awaonya wakandarasi 

Kwa upande wa barabara ya inayounganisha Kilosa na Dumila yenye urefu wa kilometa 24, Dk Magufuli amesema hafurahishwi na kazi ya wakandarasi wa eneo hilo “hata kidogo,” 

“Haiwezekani mtu mpewe kilometa 24, mpaka sasa ni zaidi ya mwaka hata kama wanajifunza, maana yake si wameshindwa kujifunza, fukuza uweke wengine wanaofanya kazi.

“Nataka sasa huu mradi ubadilike na nina wapa mwezi mmoja, kazi zianze kufanyika. Wafanye kazi usiku na mchana,” ameagiza Rais.