November 24, 2024

Ujue umuhimu wa kuchukua likizo kazini

Ni muda mzuri wa kuangalia fursa zingine zitakazosaidia kuboresha maisha nje ya kazi unayofanya.

  • Mtu anapata muda mzuri wa kujishughulisha na masuala mbalimbali nje ya kazi.
  • Zinasaidia kuongeza ufanisi wa mtu anaporudi kazini.
  • Ni muda mzuri wa kuangalia fursa zingine zitakazosaidia kuboresha maisha. 

Dar es Salaam. Baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu, mapumziko ni moja ya vitu muhimu kwa kila mfanyakazi ili kumpa fursa ya kuongeza ufanisi wake anaporejea kazini.

Mapumziko yanaweza kuwa katika mfumo wa likizo fupi au ndefu kulingana na eneo analofanya mtu kazi.

Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004, inaeleza kuwa mwajiri anatakiwa kumpa mwajiriwa likizo ya siku 28 mfululizo katika kila mwaka yaani kipindi cha miezi 12 katika mzunguko wa ajira. Ifahamike kuwa siku za likizo zinaweza kupungua endapo mwajiriwa alishawahi kuomba likizo za dharura mbalimbali katika mwaka husika.

Licha ya kuwa zipo likizo mbalimbali zinazotambulika kisheria ikiwemo ya ugonjwa na huruma. Leo tunazungumzia likizo ya kila mwaka ambayo mfanyakazi anatakiwa kuipata ili apumzike na kuachana kabisa na shughuli za ofisi kwa kipindi fulani.

Watu huchukua likizo siyo tu kukaa nyumbani lakini pia hujihusisha na mambo mbalimbali ya kijamii ambayo husaidia kubadili wanavyofikiri dhana nzima ya maisha.Hata hivyo, bado wafanyakazi wengi hawajui uwepo wa haki hii na umuhimu wake. Na wakati mwingine baadhi ya waajiri hutumia udhaifu huo kuwadhulumu wafanyakazi wao haki hii ili kujinufaisha.

Hizi ndizo sababu ya kwanini uchukue likizo unapokuwa kazini:


Inaongeza ufanisi wa mtu kazini

Mtu anapochukua likizo anapata muda mrefu wa kupumzika, kupanga mambo yake kwa ufasaha na kujipanga vizuri kwa ajili ya nyakati atakapokuwa anarudi kazini.

Mwili na akili huchoka na huhitaji mapumziko katika kipindi fulani ili kujihuisha tena (reboot). Wakati mwingine tunafanya kazi muda mwingi na kukosa mapumziko, matokeo yake ufanisi unapungua na tunashindwa kutimiza malengo tuliyowekewa.  


Zinazohusiana


Mahusiano mazuri kati ya kampuni na mwajiriwa

Kampuni zina utaratibu wa kuruhusu wafanyakazi kuchukua likizo mara baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu. Uwezo wa kampuni kuhamasisha wafanyakazi kuchukua likizo ni moja ya mafanikio kwa kampuni kwani inaonesha hali ya kujali kwa wafanyakazi ili kukamilisha sheria zilizopo ndani ya kampuni.

Kampuni iliyofanikiwa inatarajia kuona wafanyakazi wake wanafanikiwa na kuboresha maisha yao ikiwemo afya. Likizo inawasaidia wafanyakazi kuipenda zaidi kampuni na kuona ni mahali salama kutumia taaluma na ujuzi wao kutoa huduma kwa umma.

Pata muda wa kumpumzika baada ya kazi. Picha| Leio McLaren (@leiomclaren)/Unsplash.

Muda wa kujipanga zaidi na maisha nje ya kazi

Muda wa likizo pia ni wakati muafaka ambapo mtu anaweza kujipanga na vitu mbalimbali anavyoweza kufanya nje ya maisha ya kazi kama kutafuta biashara anayoweza kumwingizia kiasi fulani cha pesa pamoja na familia wakati akiendelea na kazi za kila siku.

Inaweza kuwa ni fursa kuwatembelea ndugu na marafiki ili kuimarisha mahusiano ya kifamilia. Lakini ni wakati pia wa kukaa na familia kutafakari walikotoka na wanakokwenda.

Wengine hutumia kipindi hiki kusafiri katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kupumzika na kujifunza vitu vipya ambavyo haviko katika maeneo yao. Hii huwasaidia kuboresha uwezo wa kuelewa mambo na hata kupata mawazo ya kibunifu yanayoweza kuchangia maendeleo ya kampuni. 

Likizo inaweza kutumika katika shughuli za kijamii ikiwemo kujitolea kuwasaidia watu wenye uhitaji ikiwa ni sehemu ya kuboresha maisha ya watu.