Ujumbe wa mwisho wa Mengi kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii
Ujumbe huo ulihusu urafiki na biashara aliuandika Aprili 23, 2019 ambapo ndiyo ulikuwa ujumbe wa mwisho kuwekwa katika ukurasa wake wa Twitter mpaka mauti yalipomkuta.
- Ujumbe huo aliandika Aprili 23, 2019 ambapo ndiyo ulikuwa ujumbe wa mwisho kuwekwa katika ukurasa wake wa Twitter mpaka mauti yalipomkuta.
- Unaelezea uhusiano ulipo katika ya biashara na urafiki na kwa kiasi gani unaweza kujenga na kubomoa mahusiano ya watu.
- Mengi alikuwa miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa kwa wafuasi wa Twitter nchini Tanzania.
Dar es Salaam. Mfanyabiashara Reginald Mengi ambaye sasa ni marehemu aliandika ujumbe mzito katika mtandao wa Twitter akielezea uhusiano uliopo kati ya biashara na urafiki ambao uliibua mjadala mpana kwa watumiaji wa mtandao huo.
Ujumbe huo aliandika Aprili 23, 2019 ambapo ndiyo ulikuwa ujumbe wa mwisho kuwekwa katika ukurasa wake mpaka mauti yalipomkuta akiwa Dubai.
Katika ujumbe huo alimnukuu Bilionea wa zamani wa Marekani, John Rockefeller ambapo anabainisha kuwa urafiki unaotokana na biashara zinazowakutanisha watu ni bora kuliko biashara itakayozaliwa kutokana na urafiki wenu.
“Urafiki unaotokana na biashara zenu ni bora kuliko biashara itakayozaliwa kutokana na urafiki wenu”Billionea wa zamani wa Marekani John D,Rockefeller”
— Reginald Mengi (@regmengi) April 23, 2019
Muda mfupi baada ya Mengi ambaye mpaka anafariki alikuwa na umri wa miaka 75 kuweka ujumbe huo, uliibua mawazo tofauti kutoka kwa wafuasi wake huku wengine wakikubaliana naye kwa nukuu aliyochapisha.
Paul Luziga alichangia na kusema, “mara nyingi urafiki wa kibiashara hufa pale panapokosekana mutual benefit (maslahi ya pande mbili).”
Lakini Elinas Peter akaongezea kuwa urafiki unaotokana na biashara ni mbaya kuliko yote.
“Urafiki unaotokana na biashara ni urafiki wa kibiashara tu na siku wewe ukianguka kibiashara hawatokua rafiki zako tena kwa maana hakukuwa na kinachowaunganisha zaidi ya faida za kibiashara. Na nafikiri ndiyo urafiki hatari na mbaya kuliko yote,” ameandika Peter wakati akichangia katika ukurasa wa Twitter.
Godson Chacha amesema ujumbe alioutoa Mengi unapatikana katika kitabu chake cha I can,I Must,I will ambacho amekisoma na kwa kauli yake amepigilia msumari.
Lakini baadhi ya wafuasi wake walimsifu kwa kubadilisha mada kwa sababu kabla ya ujumbe huo, alikuwa anachapicha zaidi jumbe zinazohusu mahusiano hasa ya ndoa yake.
Jumbe hizo ambazo zimejaa mahaba na sifa njema kwa mkewe Jacqueline Ntuyabaliwe-Mengi nazo ziliibua mjadala mpana kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Denny ven deeper akamuuliza Mengi, “Leo vipi mzee haumpost K-lynne (Jacqueline)?? Huku Seth Duguda akisema bora leo mapenzi umeweka pembeni kidogo.
Moja ya ujumbe ulioibua hisia tofauti kwa wafuasi wa mengi ni ule wa, “Ni furaha kuadhimisha ndoa yetu mpenzi wangu. Imekuwa safari iliyojawa na mapenzi na furaha. nakupenda sana.”
Soma zaidi:
- Mengi kuwekeza Sh68 uchimbaji mafuta, gesi Tanzania
- Rais Magufuli, watanzania wamlilia Mengi
- Mengi alivyoacha alama ya uwekezaji katika teknolojia Tanzania
Umaarufu wa Mengi katika mtandao wa Twitter
Mengi amekuwa miongoni mwa watu maarufu Tanzania wenye wafuasi wengi kutokana na aina ya maudhui anayochapisha kwenye mtandao huo ambayo yamewakuwa yakiwagusa wengi hasa vijana wenye ndoto za kufanikiwa katika maisha ya ujasiriamali.
Mpaka kufikia leo, kwa mujibu wa takwimu za Twitter, Mengi ana wafuasi milioni 2.11 katika mtandao huo huku akiwa amechapisha twitti 2,097 tangu ajiunge na mtandao huo Januari 2012
Agosti 2018, www.nukta.co.tz kwa kutumia takwimu za mitandao ya kijamii wa Socialbakers ilibaini kuwa hadi Julai 24 2018, Mengi alikuwa anaongoza kwa wafuasi wengi nchini Tanzania.
Sociabakers hutoa takwimu za watu na mashirika au kampuni mbalimbali zinazotumia mitandao ya kijamii. Takwimu hizo huchukuliwa kwa kutumia mfumo uliounganishwa moja kwa moja na mitandao husika.