October 6, 2024

Ujumbe wa Waziri wa Zanzibar kwa vijana wa Tanzania

Amewataka vijana kutumia zaidi vipaji vyao kujiingizia vipato na kuacha kulalama juu ya ukosefu wa ajira unaoendelea kuliandama Taifa.

  • Amewataka vijana kutumia zaidi vipaji vyao kujiingizia vipato na kuacha kulalama juu ya ukosefu wa ajira unaoendelea kuliandama Taifa.
  • Amewakumbusha Watanzania waishio ughaibuni wenye vipaji vya namna hiyo kushirikiana na wenzao wenye vipaji kama vyao waliopo nchini katika kutumia zaidi fursa zilizopo.

Zanzibar. Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Moudline Castico amewataka vijana kutumia zaidi vipaji vyao kujiingizia vipato na kuacha kulalama juu ya ukosefu wa ajira.

Mbali na ushauri huo, Castico amewakumbusha Watanzania waishio ughaibuni wenye vipaji vya namna hiyo kushirikiana na wenzao wenye vipaji kama vyao waliopo nchini katika kutumia zaidi fursa zilizopo.

Castico, aliyekuwa akizungumza katika maonyesho ya mitindo yaliyofanyika Zanzibar yakiongozana na mashindano ya warembaji yaliyofanyika Machi 3 mwaka huu, amesema badala ya watu kukaa bila ajira ni vizuri kutumia vipaji vyao kujiingizia kipato.

“Kila mtu anaweza kujiajiri kwa kutumia vipaji vyao,” amesema.

Mmoja wa waasisi wa maonyesho hayo ya Zanzibar Glamr, Maitham Mohammed amesema kusudi la maonyesho hayo ni kuibua vipaji vilivyojificha nchini hasa vya vijana wanaoshiriki katika urembo na ubunifu wa mavazi.

“Mashindano ya warembaji yamefanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania na tumeyafanya ili kuendeleza vipaji vya vijana wakizanzibari,” amesema.


Soma zaidi:


Amesema ni jambo la kusikitisha kuona wiki kadhaa zilizopita moja ya harusi iliyofanyika visiwani Zanzibar  iliwalazimu waandaaji kuajiri mrembaji kutoka nchi za nje licha kuwa kuna Wazanzibari wenye vipaji kama hivyo.

Aysha Ally, ambaye ni mmoja wa wabunifu walioonyesha mavazi yao na pia mshindi wa tuzo za ubunifu za nchini Uingereza, amesema maonyesho hayo ni jukwaa zuri la kuanzia kwa vijana wabunifu wa kizanzibari na warembaji.

“Vijana wakizanzibari wamepata sehemu kwa ajili ya kuonyesha vipaji vyao. Ni njia kuelekea kutimiza ndoto zao,” amesema Aysha.

Maonyesho ya mitindo na mashindano ya warembaji ya Zanzibar Glamr yamefanyika kwa mara ya kwanza Zanzibar yakiwa yamesheheni wabunifu na warembaji kutokea Zanzibar.