November 24, 2024

Ukopeshaji sekta binafsi waongezeka zaidi ya mara 10 Tanzania

Waziri wa fedha amesema ukopeshaji huo umepaa kwa asilimia 10.6 katika mwaka ulioshia Aprili 2019 kutoka asilimia 0.8 kipindi kama hicho mwaka 2018.

Sehemu kubwa ya mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuelekezwa katika shughuli binafsi/kaya ambazo zilipata wastani wa asilimia 28.8 ya mikopo yote. Picha|Mtandao.


Waziri wa fedha amesema ukopeshaji huo umepaa kwa asilimia 10.6 katika mwaka ulioshia Aprili 2019 kutoka asilimia 0.8 kipindi kama hicho mwaka 2018.

  • Miongoni mwa hatua zilizochagiza hali hiyo ni udhibiti wa sera za fedha na kupungua kwa kiwango cha mikopo chechefu. 

Dar es Salaam. Serikali imesema kuwa mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka mara 13 ndani ya mwaka mmoja kutokana na hatua mbalimbali inazoendelea kuchukua ikiwemo kupungua kwa mikopo chechefu kwenye benki za biashara nchini.

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango ameliambia Bunge leo jijini Dodoma kuwa mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka kwa wastani wa asilimia 10.6 katika mwaka ulioishia Aprili 2019 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 0.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2018.

“Kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kulichangiwa na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuboresha mazingira ya biashara; usimamizi thabiti wa sera ya fedha; pamoja na kupungua kwa mikopo chechefu kwenye benki za biashara kulikotokana na matumizi ya kanzidata ya taarifa za wakopaji katika kuidhinisha mikopo,” amesema Dk Mpango wakati akiwasilisha taarifa ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Serikali wa mwaka 2019/20.

Dk Mpango amesema mikopo hii imesaidia kuanzisha na kuimarisha shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo biashara, ujenzi na kilimo.


Soma zaidi: 


Bosi huyo wa wizara ya fedha ameeleza kuwa sehemu kubwa ya mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuelekezwa katika shughuli binafsi/kaya ambazo zilipata wastani wa asilimia 28.8 ya mikopo yote ikifuatiwa na shughuli za biashara zilizokuwa na wastani wa asilimia 18.5 na shughuli za uzalishaji viwandani asilimia 11.3.

“Aidha, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha benki za biashara zina ukwasi wa kutosha na kuongeza kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi. 

“Hatua hizo ni pamoja na kuboresha masoko ya fedha na utendaji wa benki, kuboresha mazingira ya kufanya biashara na upatikanaji wa taarifa za wakopaji ili kuongeza uwazi na ufanisi katika utoaji wa mikopo,” amesema.

Wiki iliyopita Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilitoa waraka kwa benki za biashara nchini ukibanisha kushusha kiwango cha fedha kinachotakiwa kushikiliwa na benki kama amana (Statutory minimum reserve (SMR) kutoka asilimia nane hadi saba ili kuongeza ukopeshaji katika sekta binafsi na kuchagiza ukuaji wa uchumi. Kiwango hicho kitaanza kutumika kuanzia Julai mosi mwaka huu.

Mara ya mwisho BoT kushusha kiwango hicho ilikuwa ni Machi 2017 ambapo ilishusha kiwango cha SMR kutoka asilimia 10 hadi nane.