July 5, 2024

Umaarufu wa Dk Shika ulivyoibuka ghafla mwaka 2017

• Takwimu za Google trends zinaonyesha kuwa mvuto wake waanza kuporomoka

maoni@nukta.co.tz

Dar es Salaam. Hakuwa anafahamika hata kidogo. Hata kwenye mtandao wa Google ilikuwa ni vigumu kulipata jina lake hadi Oktoba, 2017.

Lakini ndani ya saa chache Novemba 9, Dk Luis Shika alianza kuteka mitandao ya kijamii. Uamuzi wake wa kushiriki mnada wa nyumba za Bilionea Said Lugumi na kutangaza dau la juu ndiyo uliomuibua.

Hata hivyo, huenda asingekuwa maarufu kwa kujitokeza tu kununua nyumba hizo zilizopo Mbweni na Upanga katika mnada huo uliosimamiwa na kampuni maarufu ya udalali ya Yono Auction Mart.

Watu wengi wameshajitokeza kununua nyumba zinazopigwa mnada na benki au taasisi za kifedha lakini hawajawahi kuwa maarufu kiasi cha kufikia nafasi ya Dk Shika.

Ili kujiridhisha Dk Shika alikuwa maarufu kwa kiwango gani mwaka 2017, tumetumia takwimu za mtandao wa Google Trends unaorekodi taarifa zinazotafutwa au kutumiwa zaidi mtandaoni ambao unaweza kuhifadhi taarifa za kila nchi ulimwenguni.

Kuhakikisha tunapunguza mapungufu ya kitakwimu ambayo yanaweza kutokea wakati wa kuchambua umaarufu wa Dk Shika, tulitumia maneno ambayo yanayotumika zaidi mtandaoni ya “Dk Shika” na “Dk Luis Shika”. Tulitafuta takwimu za maneno hayo kwa pamoja na kuzifananisha ili kupata picha kamili ya namna watu walivyovutiwa naye.

Uchambuzi wa kitakwimu uliofanywa na nukta.co.tz kutoka Google trends unaonyesha kuwa umaarufu wa Dk Shika ulianza kurekodiwa mtandaoni Novemba 9 na kipindi chote cha nyuma hakukuwa na taarifa za kutosha kuonyesha umaarufu wake.

Hata hivyo, umaarufu ulipaa zaidi Novemba 18 baada ya neno “Dk Shika” kupata alama zote 100 ikiwa na maana kuwa lilikuwa maarufu zaidi kwa wakati wote huku lile la “Dk Luis Shika” likipata alama 58 ikiwa ni juu ya kiwango cha nusu ya umaarufu. Novemba 18, ndiyo siku ambayo alitangaza kuwa ameshalipia Dola za Kimarekani 100 (Sh220,000) kwa ajili ya bima ya kuletewa fedha zake kutoka Urusi.

Tangu wakati huo umaarufu ulishuka na kubaki katika wastani wa juu ya alama 25 kabla ya kupaa tena Desemba 9, shukran kwa waliokuwa wakifananisha umaarufu wake na wa kina Babu Seya na Papii Kocha baada ya kutolewa gerezani kwa msamaha wa Rais John Magufuli. 

Iwapo uchambuzi utafanywa kati ya wiki ya katikati ya Novemba hadi sasa, mvuto Dk Shika umeanza kuporomoka na huenda akapotea kabisa iwapo asipoendelea kualikwa katika matamasha ya kijamii na burudani au kushirikishwa kwenye matangazo ya biashara kama walivyofanya hivi karibuni.

Kwanini Dk Shika alikuwa maarufu?

Umaarufu wa Dk Shika ulipanda kwa sababu nyingi lakini kuna mambo makubwa matatu. Mosi, ni matumizi ya lugha rahisi ya “900 itapendeza” katika kufanya manunuzi ya nyumba zenye thamani kubwa za mamilioni na mabilioni. Kwa kipato cha mtanzania wa kawaida, ilikuwa kama ni kejeli kurahisisha malipo ya Sh900 milioni kwa kusema tu “900 itapendeza”.

Kauli hiyo nayo huenda isingekuwa maarufu kama Dk Shika angeweza kununua nyumba hizo tatu za kifahari zenye thamani ya zaidi ya Sh3 bilioni zikiwemo mbili za Mbweni.

Kushindwa kwake kutoa asilimia 25 ya gharama yote ndani ya muda inayotakiwa kulifanya watu wavutiwe kumfahamu zaidi. Kitendo hicho kilifanya polisi wamshikilie kituo kikuu cha polisi (Central) kwa tuhuma za kuvuruga mnada.

Upepo wa umaarufu wa Dk Shika kama bilionea aliyenunua nyumba zilizokuwa zimeshindikana awali ulibadilika na kuonekana ni tapeli. Ilibainika zaidi kuwa ‘bilionea’ huwa anaishi katika nyumba ya kawaida huko Tabata jijini hapa na aliwahi pata misukosuko huko Urusi iliyofanywa akatwe vidole vya mikononi.

Hata baada ya kutoka polisi, Dk Shika ameendelea kusisitiza kuwa na uwezo wa kununua nyumba hizo na ameshaalikwa katika mikutano mbalimbali na kufanya matangazo ya biashara likiwemo la mchezo wa kubahatisha la Sokabet.

Pamoja na umaarufu wake wa mtandaoni, bado kuna maswali lukuki yamesalia. Je, kulikuwa na sababu ya kumpa Dk Shika umaarufu kiasi hicho. Umaarufu huo umeleta tija gani kwa taifa?

Je, Dk Shika ataendelea kuwa maarufu mwaka 2018? Unafikiri ni vitu gani vilimfanya awe maarufu? Tuambie kupitia mitandao ya kijamii ya Facebook: @NuktaTanzania, Twitter: @NuktaTanzania.