UN yatoa neno hukumu kifo cha mwanahabari Jamal Khashoggi
Yasema kinachohitajika ni uchunguzi huru ili kuhakikisha uwajibikaji kwa ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa katika kesi hiyo.
- Yasema kinachohitajika ni uchunguzi huru ili kuhakikisha uwajibikaji kwa ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa katika kesi hiyo.
- Watu watano wahukumiwa kifo, watatu wamehukumiwa kifungo cha pamoja cha miaka 24, kutokana na mauji ya mwanahabari huyo mwaka jana.
Umoja wa Mataifa (UN) umeendelea kusisitiza kuwa kinachohitajika baada ya mauaji ya mwandishi wa habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi ni uchunguzi huru, usio na upendeleo ili kuhakikisha uwajibikaji kwa ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa katika kesi hiyo.
Tamko la UN limekuja baada ya jana (Desemba 23, 2019) Mahakama nchini Saudi Arabia kuwahukumu watu watano adhabu ya kifo kwa mauaji ya mwana habari huyo.
Akizungumza jana mjini New York, Marekani kuhusu hukumu hiyo, Msemaji wa umoja huo, Stephane Dujarric amesema bado wanahitaji kuona haki inatendeka lakini wanatofautiana na adhabu ya kifo iliyotolewa kwa watu waliohusika na mauaji hayo.
“Tunazingatia ripoti za leo kwamba watu wanane wamekutwa na hatia na kuhukumiwa na mahakama ya jinai ya Riyadh kuhusu mauaji ya Jamal Khashoggi.
“Katibu Mkuu pia anaendelea kusisitiza ahadi ya Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha uhuru wa kujieleza na ulinzi wa waandishi wa habari, na pia upinzani wetu wa muda mrefu kuhusu adhabu ya kifo,” amesema Dujarric katika taarifa iliyotolewa na UN.
Soma zaidi:
- Polisi Tanznaia yakiri kumshikilia Mwanahabari Kabendera
- Uhamiaji waeleza sababu za kuendelea kumshikilia Mwanahabari Kabendera
- Mwanahabari Erick Kabendera ashitakiwa kwa utakatishaji fedha, uhujumu uchumi
Khashoggi aliyekuwa mwandishi wa habari wa gazeti la Washington Post na mkosaji wa familia ya kifalme ya Saudi Arabia, aliuawa katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul mwaka jana na wanaodaiwa kuwa ni timu ya majasusi wa Saudia.
Mauaji ya Khashoggi yaliishangaza dunia na pia raia wengi wa Saudia, ambao walishtushwa na tukio la raia wa nchi hiyo kuuliwa na mawakala 15 wa serikali ndani ya mojawapo ya balozi za ufalme huo.
Watu wengine watatu wamehukumiwa kifungo cha pamoja cha miaka 24, kwa mujibu wa taarifa ya Mwanasheria Mkuu wa Saudia. Wasaidizi wawili wakuu wa Mwanamfalme, Mohammed bin Salman wamefutiwa mashitaka kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.