October 6, 2024

UN yawalilia waliofariki katika shambulizi la studio ya vikaragosi Japan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesema ameshtushwa sana vifo vya watu takriban 33 ndani ya studio. Hiyo.

Jengo la studio ya vikaragosi (Kyoto Animation-KyoAni) lililoshambuliwa Alhamisi asubuhi na kuua watu takriban 33. Picha|Mtandao.


  • Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesema ameshtushwa sana vifo vya watu takriban 33 ndani ya studio. Hiyo.
  • Amesema katika kipindi hiki, UN inashikamana na Serikali ya Japan.
  • Shambulio hilo lilitekelezwa Alhamisi asubuhi na mtu mmoja aliyedai studio hiyo iliiba kazi zake. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesema ameshtushwa sana na vifo vya watu takriban 33 ndani ya studio maarufu ya vikaragosi mjini Tokyo, Japan vilivyosababishwa na shambulio la makusudi la moto lililotekelezwa Alhamisi asubuhi. 

Shambulizi hilo limeelezwa kuwa ni moja ya mashambulizi mabaya zaidi lililoua watu wengi katika historia ya Japan.

Kwa mujibu wa UN, Polisi nchini Japan tayari wamembaini mtu anayeshukiwa kufanya shambulio hilo ambaye ameripotiwa kuingia katika jengo la studio hiyo ya vikaragosi (Kyoto Animation-KyoAni) kuwa ni Shinji Aoba akiwa amebeba makopo ya bidhaa za majimaji za mlipuko ambayo aliyamwaga katika sehemu tofauti za studio hiyo kabla ya kuwasha moto.

Duru za Habari zinaeleza kuwa watu walioshuhudia mtu huyo akikamatwa wamesema alisikika akidai kuwa kampuni hiyo ya vikaragosi iliiba baadhi ya mawazo yake ya ubunifu.


Soma zaidi: Mabilionea kulijenga upya kanisa la Notre Dame Ufaransa 


Takriban watu 70 walikuwa ndani ya jengo hilo wakati moto mkubwa ulipolipuka na watu zaidi ya 30 walikimbizwa hospitali na wengi wa waliokufa wanadaiwa kukutwa kwenye ngazi wakijaribu kukimbia moto huo.

“Katibu Mkuu ameshtushwa sana na kupotea kwa maisha ya watu kutokana na shambulio la moto mjini Kyoto,” imesema taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Msemaji wake ambapo ametuma salamu za rambirambi kwa waathirika, watu na serikali ya Japan huku akiwatakia ahuweni ya haraka majeruhi wote. 

“Katika kipindi hiki cha janga kubwa, Umoja wa Mataifa unashikamana na serikali na watu wa Japan,” amesema Guterres. 

Watu wengi walijitokeza jana nje jengo hilo na kuonyesha heshima zao kwa kuweka maua na kusali.

Kampuni hiyo ya vikaragosi imeshatengeneza picha nyingi za video ikiwemo sinema ya hivi karibuni ya ‘Violet Evergarden’ ambapo imechukuliwa na warusha vipindi wengi duniani kwenye mtandao na kuonyeshwa na kampuni ya Netflix.

KyoAni ilianzishwa mwaka 1981 na imetengeneza vipindi vingi vya video za vikaragosi ambavyo vimekuwa vikurushwa katika runinga mbalimbali duniani. Umaarufu wake unatokana na ubunifu wa wafanyakazi wake kutengeneza kazi za sanaa zenye ubora na zilizo tofauti na wengine.