Unafanyia kazi nyumbani? Fanya haya kuboresha afya yako
Wataalam wa masuala ya kazi na afya wameeleza mambo mbalimbali yanayoweza kuwasaidia watu wanaofanyia kazi nyumbani kuongeza ufanisi na kuhakikisha afya zao zinakuwa bora wakati wote ikiwemo kufanya mazoezi.
- Pata muda wa kufanya mazoezi na kucheza na watoto wako.
- Kunywa maji ya kutosha na mlo kamili huku ukiepuka kutumia vyakula vya wanga kwa wingi.
- Pata muda wa kupumzika na kujumuika na familia yako.
Dar es Salaam. “Nilikuwa na mpango chakula (diet) lakini sasa hivi umevurugika. Ninajihisi kuongezeka uzito,” Amesema Gamariel Mrema ambaye ni mwanasheria anayelazimika kufanyia kazi nyumbani kwa sasa kutokana kusambaa kwa ugonjwa wa Corona.
“Ninaweza nisinywe maji kabisa. Kwa kifupi kufanyia kazi nyumbani kwangu siyo salama kiafya kabisa,” amesema Mrema ambaye anabainisha itamchukua muda mrefu kuzoea kufanyia kazi nyumbani.
Huenda Mrema anawakilisha watu wengi ambao wanafanyia kazi wakiwa nyumbani kwa sasa, ambao wako katika hatari ya kupata changamoto za kiafya ikiwemo kuongezeka uzito, kupata magonjwa yasiyoambukiza na kupungua kwa ufanisi wa utendaji wa afya akili na mwili.
Hata hivyo, hakuna linashindakana chini ya uso wa dunia. Wataalam wa masuala ya kazi na afya wameeleza mambo mbalimbali yanayoweza kuwasaidia watu wanaofanyia kazi nyumbani kuongeza ufanisi na kuhakikisha afya zao zinakuwa bora wakati wote.
Meneja rasilimali watu na mwandishi wa vitabu (The color of life), Ritha Tarimo amesema kufanyia kazi nyumbani kunamfanya afanye kazi kwa muda mwingi kuliko awali lakini bado anajitahidi kuendana na mazingira.
Ritha ambaye ameandika kitabu cha “The Color of Life”, amependekeza kwa ambao wana watoto watenge muda kufurahia na familia zao hasa kucheza na watoto wao ambayo pia ni mazoezi.
“Sipo na harakati nyingi kama awali lakini ninatenga muda kutembea na kufanya mazoezi ya kunyoosha viungo (yoga) na ninacheza na mwanangu. Graham mwenye miaka saba ana harakati nyingi na hiyo inanisaidia sana,” amesema Tarimo.
Amesema kucheza kunampatia furaha ya kukaa karibu na familia yake lakini kunachangamsha akili yake na kumuwezesha kukamilisha majukumu ya kazini kwa ufanisi mkubwa.
Hata hivyo, amekiri kuwa wakati mwingine kufanyia kazi nyumbani inapunguza utulivu na ufuatiliaji wa kazi wa kiwango kinachohitajika.
Siyo lazima uite mwalimu wa mazoezi. Unaweza kufanya mazoezi ya kawaida kama Push_up na ukawa kwenye hali nzuri. Picha| Giphy
Mshauri wa masuala ya afya na mtindo wa maisha, Dk Joshua Sultan amesema jambo muhimu la kuzingatia kwa sasa ni kufanya mazoezi na kunywa maji ya kutosha.
“Ukinywa maji utajikuta unaruti (safari) za kwenda chooni na hiyo itakusaidia kutokukaa kwenye kiti chako kwa muda mrefu. Hata haihitaji sayansi.” amesema mtaalamu huyo.
Sultan pia amesema mtu anaweza kufanya mazoezi rahisi ambayo yanafanyika nyumbani yakiwemo kuruka kamba, kujinyoosha ambayo hayahitaji maelekezo ya mwalimu wa mazoezi.
“Siku hizi mambo mengi yapo mtandaoni. Kupitia simu yako, unaweza ukaona jinsi mazoezi haya yanafanyika kwa ufasaha,” amesema Dk Sultan.
Zinazohusiana
- Njia rahisi za kukabiliana na ongezeko la joto mwilini
- Fanya haya kulinda afya kazini
- Jinsi unavyoweza kuishinda sonona isiharibu maisha binafsi, kazi
Naye Daktari kutoka kituo cha Afya cha Ngarenanyuki kilichopo mkoani Arusha Jonas Kaguo amesema kipindi hiki ambacho watu wako nyumbani wanashauriwa kula chakula chenye virutubisho vya kutosha.
Daktari huyo amesema Kaguo kwa sababu watu hukaa muda mrefu nyumbani ni muhimu waepuke kula vyakula vya wanga kwa wingi kwani vinaweza kuongeza uzito mwilini kwa sababu hazitumiki.
Daktari huyo ameshauri ulaji wa matunda hasa yenye rangi rangi.
“Penda kutumia matunda kwani yenyewe hayahitaji nguvu nyingi kumeng’enywa. Kwanini ujishindilie ugali mkubwa wakati hauna popote pa kuenda?” amehoji Dk Kaguo.
Amebainisha kuwa shughuli za nyumbani kama kulima bustani, kusafisha nyumba na kucheza na wanafamilia kunaweza kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa mtu.
Unachukua hatua gani kuimarisha afya yako ukiwa nyumbani? Tuambie