Unaogopa kutofautiana na familia yako? Tazama filamu ya Mulan
Wakati wenzake wakicheza mdako, Mulan alikuwa akikimbiza kuku huku akipaa naye hadi juu ya paa na mafunzo ya Tai Chi kwake ilikuwa ni kitu cha kawaida sana.
- Inamhusu binti aliyelazimika kuingia vitani kwa kuigiza kuwa ni mwanamume.
- Siri yake inapofichuka, analazimika kupigana vilivyo ili arudi uwanjani.
- Je, atafanikiwa? Atakubalika? Atapona na kurudisha heshima ya familia yake?
Dar es Salaam. Ulingoni… Baada ya kikosi chao kuzidiwa na kunasa katika mtego wa adui Bori Khan, ni mpiganaji mmoja tu ndiyo hajanasa katika mtego huo.
Ni Hua Mulan ambaye mahesabu yake yanamuonyesha kuwa dakika chache zijazo, wenzake wote watarudishwa nyumbani ndani ya majeneza.
Anachokifanya Mulan ni kuokota kofia za wenzake walioaga dunia kwenye mapigano hayo na kuzipanga kwenye mawe. Kisha anaelekeza mshale kwa maadui zake nao wanahisi kuwa wanashambuliwa na kundi la watu waliojificha nyuma yao.
Pale wanapoingia katika mtego wa Mulan na kuamua kuhamisha mwelekeo wa mizinga yao, wanajikuta wanapigana na wanajeshi hewa na kuupiga mlima uliojaa barafu na hivyo kusababisha tetemeko linalowasomba wote na kuwafunika na theruji.
Subiri kwanza! Huo ni utamu tu. picha linaanza hivi; tangu akiwa mdogo, Mulan alikuwa anapenda kujifunza mapigano ya Tai Chi.
Tai Chi au Tai Chi Chuan, ni sanaa ya jadi ya kijeshi ya China ambayo inafundisha kupigana kwa ajili ya ulinzi binafsi na utulivu wa moyo.
Turudi huku… Tofauti na wasichana wengine ambao walikuwa wakifanya shughuli za nyumbani, Mulan alitumia muda wake mwingi milimani akijifunza mapigo hayo.
Wakati wenzake wakicheza mdako, Mulan alikuwa akikimbiza kuku huku akipaa naye hadi juu ya paa.
“Hakuna mwanaume atakayeoa binti anayekimbizana juu ya paa na kuku,” ni maneno ya mama Mulan (Rosalind Chao) ambaye anamwambia mume wake (Hua Zhou).
“Ni muda wa wewe kukificha kipaji chako,” ni maneno yanayorarua moyo wa Mulan hasa kwa kuwa yametoka kwa baba yake aliyekuwa akimuunga mkono kwa kila kitu.
Baada ya kuchoka kuishi na uongo, Mulan anaamua kuonyesha uhalisia wa jinsia yake. Picha| Variety.
Lakini Zhou anabadilika baada ya mke wake kumkumbusha tamaduni za jamii yake kuwa Mulan anatakiwa kuleta heshima kwa familia yake kwa kuolewa.
Filamu inakolea sukari baada ya ufalme kuvamiwa na kundi linaloongozwa na Bori Khan ambaye anasadiwa na mchawi Xianniang.
Baada ya kila familia kutakiwa kuchangia kijana mmoja kwa ajili ya kupigwa msasa kujiandaa na vita, Baba Mulan ambaye ni mlemavu anajitolea kwani familia yake ina mabinti tu.
Kunapopambazuka, baba Mulan anakuta mavazi yake ya vita na upanga havipo huku Mulan ambaye amekimbia kuchukua nafasi ya baba yake haonekani nyumbani.
Soma zaidi
- Zingatia haya kabla ya kuchagua rangi ya nyumba yako
- Mabinti Watanzania wang’ara kwa kubuni teknolojia ya kupambana na ukame
- Tafakari haya kabla ya kuingia kwenye ujasiriamali
Ndiyo! Mulan huyo huyo aliyeokoa kundi la wanajeshi waliokuwa mbioni kuaga dunia, ni mtoto wa kike ambaye hapaswi kuwa ulingoni. Siri yake itadumu kwa muda gani?
Kushindwa kuoga kwa siku tatu, kuona ya sirini ni kati ya mambo mengi utakayokutana nayo ukiitazama filamu hii.
Baada ya Mulan kutambulika siyo mwanaume ataruhusiwa kuendelea na vita? Itazame filamu hii kupitia kumbi za kuangalizia filamu zikiwemo Century Cinemax Mlimani City na Aura Mall jijini Dar es Salaam kwa gharama ya Sh10,000.
Kama filamu siyo fungu lako, unaweza kusikiliza muziki, kufanya mazoezi na hata kutalii ili kuupumzisha ubongo wako na shughuli za wiki nzima.