July 5, 2024

Unavyoweza kuepuka changamoto za usafiri wa ndege

Chagua siti na shirika la ndege lenye huduma za uhakika.

  • Ni pamoja na kuhakikisha unaandaa vitu vyako mapema na kubeba zana muhimu. 
  • Beba kitabu na vifaa vya kusikilizia muziki au filamu ukiwa ndani ya ndege.
  • Chagua siti na shirika la ndege lenye huduma za uhakika.

Dar es Salaam. Siku yako ya kwanza kusafiri angani maarufu kukwea pipa (ndege) ilikuwaje? Huenda ilikuwa ni siku yenye bashasha kiasi cha kushindwa kutambua changamoto ambazo huambatana na usafiri huo.

Muda mrefu wa kusubiri kabla ya kuingia ndani ya ndege, mitikisiko ya angani, kukaa kwenye siti moja bila kutembea kwa muda mrefu ni baadhi ya changamoto wanazokutana nazo wasafiri wanaotumia ndege.

Hata hivyo, kwa kila changamoto ipo ahueni ambayo mtu anaweza kuipata. Tovuti ya safari ya Travel Leisure imeeleza baadhi ya vitu ambavyo mtu anaweza kuzingatia ii afurahie safari yake wakati wote anapotumia usafiri wa ndege. Ni vitu gani hivyo?


Chagua shirika la ndege unaloliamini

Kila shirika la ndege limejizolea umaarufu wake kutokana na huduma ambazo linatoa. Mbali na kupewa viburudisho ukiwa safarini, vipo vitu vya muhimu vya kuangalia ikiwa ni pamoja na historia ya safari za shirika hilo.

Baadhi ya mashirika huduma zake siyo za kuridhisha ikiwemo kuahirisha safari mara kwa mara. Kama hutaki changamoto hiyo ikupate, basi chagua shirika la ndege linaloaminika.

Baadhi ya mashirika huduma zake siyo za kuridhisha ikiwemo kuahirisha safari mara kwa mara. Picha| Mtandao.

Chagua siti inayokufaa 

Kuna mambo mengi unayoweza kuyapata kwa kuchagua siti ya ndege inyokufaa. Unapochagua siti ya dirishani, unaweza kufurahia mandhari ya juu ya anga ikiwemo mawingu na hata udogo wa nyumba na miundombinu. 

Pia, kuchagua siti kutakusaidia kufurahia safari yako kwa kuwa na uhuru.


Hakikisha unabeba nyenzo sahihi za safari

Wapo watu ambao hupenda kulala wanapokuwa safarini lakini kelele, baridi inayotokana na kiyoyozi na mwanga ndani ya ndege vinaweza kukukera na kusitisha furaha yao. 

Kama wewe ni kati ya watu hao, hakikisha unabeba sweta lenye kofia (hoodie) na viziba masikio. Kwa njia hiyo, itakuwezesha kupata usingizi wako bila shida.


Beba kitabu, filamu na muziki uupendao

Endapo utasafiri kwa saa nyingi, huenda kulala pekee isiwe suluhisho la kuimaliza safari yako. Pale usingizi unapokuisha, unaweza kusoma kitabu, kusikiliza muziki na pia kutazama filamu ili kuiburudisha akili yako.

Pia, unapokuwa umevalia spika za masikioni kwa ajili ya kusikiliza muziki au kutazama filamu, ni muhimu kuhakikisha unasikiliza kwa sauti ya wastani ili pale matangazo yanapotolewa, yasikupite.


Soma zaidi:


Valia mavazi ambayo hayatokusumbua

Ule mchakato wa kuvua mkanda na viatu ambazo hufanyika katika sehemu ya ukaguzi, huenda zinawakera baadhi ya watu lakini hazina budi kufanyika kwa ajili ya usalama wa kila abiria.

Kama siyo muhimu kuvaa mkanda na viatu vya kamba, unaweza kuachana na mavazi hayo na kuvaa mavazi ambayo hayatokusumbua hasa wakati wa ukaguzi na pia pale hali ya hewa inapobadilika.

Zaidi ya hayo, penda kuandaa vitu vyako mapema ili kuepuka kusahau kabla ya kuanza safari. 

Mfano, unaweza kuandaa orodha ya vitu muhimu utakavyovihitaji ukiwa safarini ili uviandae mapema kuepuka gharama za kununua vitu vipya.