October 7, 2024

Unavyoweza kuikaribisha Corona nyumbani pasipo kujua

Ninaposema Corona tunaikaribisha nyumbani namaanisha namna ambavyo tunahusiana na watu ambao wanatupatia huduma tukiwa nyumbani kwa kutuletea bidhaa.

  • Ni wakati kupokea mizigo na bidhaa tunazoletewa nyumbani.
  • Watu wanaokuja nyumbani hatujui walikotoka kama wako salama.
  • Njia rahisi ya kuvunja mnyororo wa maambukizi ni kuvaa barakoa na kutumia kitakasa mikono mara kwa mara. 

Nina majuma kama mawili ndani ya jiji lenye sifa ya kuitwa bandari salama yaani Dar es Salaam. Wazazi wangu wana makazi yao hapa. Hivyo napendelea kupata siha njema toka kwao kwa kuwasalimia kila mara ninapokua ndani ya jiji hili.

Ninaamshwa na hodi mlangoni, ni mama muuza mboga mboga. Huyu mama hupita kila nyumba kila siku na kugonga. Ninamuangalia mama yangu akitoka nje kufungua geti, hajavaa barakoa, hana kitakasa mikono. 

Anamfungulia mama huyu geti, wanatabasamu wote wakiwa na ukaribu, mama huyu nae hajavaa barakoa. 

Inabidi nimuite mama yangu, nimueleze kuhusu uwezekano wa kupata maambukizi ya virusi vya Corona. Ananielewa. Badaye namuona jirani na yeye akipokea mzigo alioagiza toka kwa bodaboda. Kwa mikono na wote hawajavaa barakoa na hapana usalama wala tahadhari wanayoichukua.

Moyo wangu unapata ganzi kwa muda. Napata hamasa ya kuandika hiki ninachosemezana nanyi leo.

Katika kujikinga na Corona watu wengi sasa wameamua kujikarantini na wengine wakiamua kufanyia kazi kutokea nyumbani. Hii ni nyenzo muhimu ya kujikinga kutopata maambukizi. 

Swali la msingi, karantini tunaifanya kwa usahihi? Ugonjwa wa corona huambukizwa kwa matone ya mfumo wa upumuaji. Pia virusi hivi hukaa katika maeneo tofauti kwa muda tofauti. Hivi ni ama nguo, vyuma, fedha na hata vyakula. 

Na hii ndio maana unashauriwa kujitakasa na kuchukua tahadhari kila mara. Kwa lugha rahisi ni kwamba kila mtu anaekuzunguka anaweza kuwa mtu atakayekuambukiza dakika moja ijayo. 


Soma zaidi:


Ninaposema Corona tunaikaribisha nyumbani namaanisha namna ambavyo tunahusiana na watu ambao wanatupatia huduma tukiwa nyumbani kwa kutuletea bidhaa. 

Huduma maarufu hii huitwa “delivery” na sidhani kama kuna biashara isio na mfumo huu wa huduma. Lakini watu hawa wanapotufikia wanachukua tahadhari? Je sisi wapokeaji tunachukua hizo tahadhari pia? 

Watu hawa hushika milango na vitasa vya majumba yetu. Je tunatakasa maeneo haya? Tunapopokea vitu hivi tunakua katika mazingira ya kujilinda sisi na wao? Watu hawa hukutana na watu mbalimbali katika kazi zao. 

Hauwezi kuwa na hakika ni wapi kapata maambukizi. Kama nilivyogusia awali, kila anayekuzunguka au unaekutana naye ni kama amebeba virusi, hatunyanyapaani hasha! bali ni tahadhari. Wahenga walisema “muoga nae ni mtu”

Rai yangu sasa kwa watoa huduma hizi za kufika majumbani, wahakikishe wanavaa barakoa. Pia kuhakikisha wana vitakasa mikono ambavyo wanavitumia kila mara. 

Maana hivi vitu na bidhaa nyingine hupita katika mikono mingi hadi kumfikia mlaji wa mwisho. Na virusi hawa hutofautiana muda na kiwango cha kuwa hai kutokana na mazingira na vitu tofauti. Kwa sababu hakuna namna ambayo hutoacha kumfikishia mlaji na kumpatia ana kwa ana basi utumiaji wa huduma za malipo za kielektroniki vitasaidia kupunguza mnyororo wa maambukizi na kushusha uwezekano huo.

Hakikisha unanawa mikono au unatamia kitakasa mikono baada ya kupokea mzigo. Picha|Mtandao.

Kwa walaji wanaopokea majumbani, ni vyema kuhakikisha kuwa umevaa barakoa kabla hujafika kupokea mzigo wako. Hata kama una haraka vipi, haraka hio isiwe kukikaribia kifo chako na kuwaweka wengine rehani vile vile. 

Pia hakikisha umetakasa mikono yako punde tu baada ya kupokea mzigo wako. Iwapo ni vifaa, ni  vyema kutumia spirit kuvitakasa. Na iwapo ni bidhaa za chakula basi kuviosha kwa maji tirikika kwa walau dakika moja.

Ni muhimu kutakasa mara kwa mara vitasa vya mageti na milango yetu kila mara katika siku nzima. Hii hupunguza uwezekano wa maambukizi kupitia sehemu hizi maana huguswa na watu tofauti baada ya mizunguko kadha wa kadha. Ukate mnyororo huu wa maambukizi kwa kuchukua tahadhari hizi madhubuti.

Kwa leo nadhani nimetoa nyongo hii ilioupa moyo wangu tafakari kuu. Tuendelee kuchukua tahadhari na kutokua na mapuuza. Corona ipo, inaambukiza na inaua usipochukua tahadhari. 

Ulaji wa matunda jamii ya machungwa, mapapai, machenza nk yenye viwango vikubwa vya vitamini C ambayo ni muhimu kwa ajili ya kinga ya mwili. Usikimbilie vidonge iwapo hauna upungufu wa Vitamini C.

 Kwa pamoja tutalivuka hili. Kuwa salama, Epuka Corona, Kata mnyororo wa Corona.

Nipo!

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mazoezi tiba na mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.