October 8, 2024

Unavyoweza kuzungumza na watoto kuhusu Corona

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) limetoa vidokezo vinavyoweza kukusaidia kuwapatia majibu sahihi ya ugonjwa huo na jinsi ya kujilinda nao.

  • Iwapo bado ni wadogo na hawajasikia juu ya ugonjwa huo, huenda hautahitaji kuibua suala hilo.
  • Tumia muda wako kuwakumbusha juu ya tabia nzuri za usafi bila kuibua hofu mpya.
  • Ni muhimu kuhakikisha watoto wako hawanyanyapaliwi na wala hawasababishi uonevu kwa watu wenye ugonjwa huo. 

Mapambano ya ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) yanaendelea duniani note kila nchi ikichukua tahadhari kuwalinda raia wake.

Lakini jitihada zinahitajika zaidi kuwakinga wazee na watoto.

Ni wazi kuwa watoto wanapata mashaka hasa wanapoona taarifa kwenye mitandao na vyombo vya habari au kusikia kutoka kwa watu kuhusu janga hili.

Je utazungumza nao vipi kama mzazi au mlezi? Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) limetoa  vidokezo vinavyoweza kukusaidia kuwapatia majibu sahihi ya ugonjwa huo na jinsi ya kujilinda nao:

Uliza maswali ya kufikirisha na sikiliza

 Zungumza na watoto wako juu ya virusi vya Corona. Tafiti kiwango cha uelewa wao na fuata mwongozo wao.

Iwapo bado ni wadogo na hawajasikia juu ya ugonjwa huo, huenda hautahitaji kuibua suala hilo – chukua nafasi hiyo kuwakumbusha juu ya tabia nzuri za usafi bila kuibua hofu mpya.

“Hakikisha uko katika mazingira salama na umruhusu mtoto wako azungumze kwa uhuru. Michoro, hadithi na shughuli zingine zinaweza kusaidia kufungua mjadala,” inaeleza sehemu ya vidokezo vya UNICEF.

Hakikisha unatambua hisia zao na kuwahakikishia kuwa ni kawaida kuhofia mambo hayo. Onyesha kuwa unasiliza kwa makini na hakikisha wanaelewa kuwa wanaweza kuzungumza nawe na walimu wao wakati wowote ule wanaopenda.

Mfanye mtoto kuwa rafiki yako, ongea naye kuhusu jinsi ya kujikinga na Corona. Picha|Mtandao.

Eleza ukweli kwa njia ya kirafiki na watoto

Watoto wana haki ya kupata habari za ukweli juu ya kile kinachotokea katika ulimwengu, lakini watu wazima pia wana jukumu la kuwalinda salama dhidi ya taarifa potofu.

UNICEF inaeleza kuwa tumia lugha inayoendana na umri wao, angalia wanavyopokea taarifa hizo na kuwa mwangalifu na kiwango chao cha wasiwasi.

Usikisie iwapo huwezi kujibu maswali yao. Tumia hali hiyo kama fursa ya kutafiti majibu kwa pamoja.

Tovuti za mashirika ya kimataifa kama shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) na lile la afya (WHO) ni vyanzo vikubwa vya habari.

“Wafafanulie ya kwamba baadhi ya taarifa kwenye mtandao si sahihi na kwamba ni bora kuwaamini wataalam,” vinaeleza vidokezo hivyo.

Waonyeshe jinsi ya kujilinda na marafiki wao

Njia moja bora zaidi ya kuwalinda watoto dhidi ya virusi vya Corona na magonjwa mengine ni kuhamasisha unawaji wa  mikono.

Unaweza kutumia njia mbalimbali kuwafahamisha jambo hilo ikiwemo nyimbo na michezo ili kuwavutia watoto.

 Pia unaweza kuonyesha watoto jinsi ya kujifunika na kiwiko cha mkono pindi unapokohoa au kupiga chafya.

Waeleze kuwa ni bora kutokuwa karibu na watu wenye dalili za ugonjwa wa virusi vya Corona na waombe wakueleze pindi tu watakapoanza kuhisi kama wana homa, kikohozi au shida ya kupumua.


Zinazohusiana


Wapatie hakikisho

Watoto wanaweza kushindwa kutofautisha kati ya picha za kwenye televisheni na hali yao ya binafsi, na wanaweza kuamini kuwa wako katika hatari kubwa. 

Unaweza kusaidia watoto wako kukabiliana na mfadhaiko na taharuki ya Corona kwa kuwapatia fursa ya kucheza na kupumzika, inapowezekana.  

Iwapo kuna mlipuko kwenye eneo lako, wakumbushe watoto wako ya kwamba wanaweza wasipate ugonjwa, na kwamba watu wengi wanaoambukizwa COVID-19 hawaugui sana. .

 

Angalia iwapo wanakabiliwa na unyanyapaa

Mlipuko wa COVID-19 umeleta ripoti nyingi za ubaguzi wa rangi kote ulimwenguni, kwa hivyo ni muhimu kuhakikisha watoto wako hawanyanyapaliwi na wala hawasababishi uonevu.

“Fafanua kwamba virusi vya Corona havina uhusiano wowote na muonekano wa mtu, anakotoka au lugha anayozungumza. Ikiwa wamepachikwa majina majina au wameonewa shuleni, wanapaswa kujisikia huru kumweleza mtu mzima ambaye wanamwamini,” imesema UNICEF. 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akifurahia jambo na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mnyigumba mkoani Iringa mara baada ya ziara yake Shuleni hapo kuangalia masuala ya Lishe. Picha| Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Wakumbushe watoto kusaidiana

Ni muhimu kwa watoto kufahamu kuwa watu wanasaidiana kwa matendo ya fadhila na ukarimu.

Wapatie watoto simulizi za wahudmu wa afya, wanasaynsi na vijana, miongoni mwa mifano michache, ambao wanafanya kazi kuzuia mlipuko na kuweka jamii salama. Inaweza kuwa faraja kubwa kufahamu kwamba watu wenye huruma wanachukua hatua.

Hitimisha mazungumzo kwa uangalifu

Ni muhimu kutambua kuwa huwaachi watoto katika hali ya mkanganyiko. Mazungumzo yanapokaribia kufikia tamati, jaribu kupima kiwango cha wasiwasi kwa kutazama lugha ya mwili wao, ukizingatia kama wanatumia sauti yao ya kawaida na pima kauli zao kwa kusikiliza pumzi zao.

Wakumbushe watoto wako kuwa wanaweza kuwa na mazungumzo mengine magumu na wewe wakati wowote. Wakumbushe kwamba unajali, unasikiliza na kwamba unapatikana kila wanapohisi kuwa na wasiwasi.