November 24, 2024

Unavyoweza kuzungumza na watoto kuhusu ugonjwa wa Corona

Wape taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huo kulingana na umri wao na wafundishe jinsi ya kujikinga na kuwalinda wenzao dhidi ya Corona

  • Wape taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huo kulingana na umri wao.
  • Wafundishe jinsi ya kujikinga na kuwalinda wenzao dhidi ya Corona.

Dar es Salaam. Wakati ugonjwa wa virusi vya Corona ukiendelea kutafutiwa chanjo na dawa ili kuutokomeza, wazazi na walezi bado wanajukumu la kuwalinda watoto wao kwa namna mbalimbali dhidi ya ugonjwa huo. 

Njia mojawapo ni kuzungumza nao kuhusu ugonjwa huo na namna wanavyoweza kujikinga ili wawe salama na kuendelea masomo kutimiza ndoto zao za elimu.

Utazungumza nao vipi? Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, (UNICEF) linakupatia vidokezo mbalimbali vitavyokusaidia katika mazungumzo hayo.

Mpe nafasi ya kuzungumzia ugonjwa huo

Mwambie akuambie anafahamu nini kuhusu virusi vya Corona. Tafiti kiwango cha uelewa wake na kama bado ni wadogo na hawajasikia juu ya mlipuko, huenda hautahitaji kuibua suala hilo. 

Wakumbushe juu ya tabia nzuri ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabauni bila kuibua hofu mpya.

“Hakikisha uko katika mazingira salama na umruhusu mtoto wako azungumze kwa uhuru. Michoro, hadithi na shughuli zingine zinaweza kusaidia kufungua mjadala,” imeeleza UNICEF.

Onyesha kuwa unasikiliza kwa kuwa makini na hakikisha wanaelewa kuwa wanaweza kuzungumza nawe na walimu wao wakati wowote ule wanaopenda.


Zinazohusiana.


Waeleze kwa utulivu kuhusu ugonjwa huo

Watoto wana haki ya kupata habari za ukweli kuhusu COVID-19 lakini watu wazazi, walezi na walimu pia wana jukumu la kuwalinda salama dhidi ya mkanganyiko unaoweza kutokea. 

Hapa tumia lugha inayoendana na umri wao, angalia wanavyopokea taarifa hizo na kuwa mwangalifu na kiwango chao cha wasiwasi huku ukijibu maswali yao kwa usahihi kama zinavyotolewa na wataalam wa afya. 

Tumia taarifa za Wizara ya Afya, Shirika la Afya Duniani (WHO) na taarifa rasmi za Serikali kuhusu maendeleo ya ugonjwa huo. 

 

Wahakikishie usalama wao

Wakati mwingine watoto wanaweza kushindwa kutofautisha kati ya taarifa wanazosikia na hali yao kuhusu ugonjwa huo na wanaweza kuamini kuwa wako katika hatari kubwa. 

UNICEF inaeleza kuwa katika mazingira haya wasaidie watoto wako kukabiliana na mfadhaiko kwa kuwapatia fursa ya kucheza, ratiba ya shughuli zao na kupumzika. 

 “Iwapo kuna mlipuko kwenye eneo lenu, kumbusha watoto wako ya kwamba wanaweza wasipate ugonjwa, na kwamba watu wengi wanaoambukizwa COVID-19 hawaugui sana,” inasomeka sehemu ya vidikezo vya shirika hilo.

Wafundishe watoto kwa upole na upendo kuhusu COVID-19. Picha| Mtandao.

Waepushe naunyanyapaa na ukatili

Mlipuko wa COVID-19 umeleta ripoti nyingi za ubaguzi wa rangi kote ulimwenguni, ni muhimu kuwalinda watoto wako kuhakikisha hawanyanyapaliwi na wala hawasababishi uonevu.

Waeleze kuwa virusi vya Corona havina uhusiano wowote na muonekano wa mtu, anakotoka au lugha anayozungumza. 

“Wakumbushe watoto wako kuwa kila mtu ana haki ya kuwa salama shuleni. Uonevu shuleni ni kosa na kla mmoja anapaswa kuchukua hatua kueneza ukarimu na kusaidiana,” imesema UNICEF. 

Onyesha kielelezo

Utaweza kusaidia watoto wako vizuri zaidi iwapo utakuwa mstari wa mbele kufuata maelekezo ya wataalam wa afya kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kuvaa barakoa na kunawa mikono. 

Watoto wataangalia ni vipi unachukua hatua kutokana na habari zinazotangazwa. Hii inasaidia wao kutambua iwapo unahimili hali ilivyo na unatulia. Hiyo itawapa hamasa wao kuondokana na wasiwasi kuhusu Corona.

Wakumbushe watoto kuwa wako huru kukuuliza au kujadiliana na wewe jambo lolote kuhusu Corona.