October 6, 2024

Unayotakiwa kufahamu kupata wazo bora la biashara 2020

Fanya tathmini ya mwenendo wa sasa biashara na angalia fursa zilizopo mbele yako huku ukikubali mabadiliko ya teknolojia na achana na mifumo ya zamani ya biashara.

  • Fanya tathmini ya mwenendo wa sasa biashara na angalia fursa zilizopo mbele yako.
  • Kubali mabadiliko ya teknolojia na achana na mifumo ya zamani ya biashara.

Ni mwaka mwingine wa 2020 ambao kila mtu amejiwekea malengo yake ambayo atayatekeleza. Wapo ambao wanawaza kuanzisha au kuendeleza biashara ili wapate faida kuboresha maisha yao. 

Pamoja na kujiwekea malengo ya kibiashara, bado una kila sababu ya kuwa na mawazo mapya na chanya ili biashara yako ipate soko hasa katika zama hizi ambazo teknolojia inabadilika kwa kasi.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ushauri wa uwekezaji ya SSC Capital, Salum Awadh anaeleza kwa undani ni jinsi gani mjasiriamali anaweza kuwa na wazo bora na tofauti ambalo linaweza kumtoa mwaka 2020. 

Katika ujumbe aliouweka jana (Januari 5, 2020) katika ukurasa wake wa Twitter, Awadh ambaye pia ni mtaalam wa masuala ya mitaji ya kampuni ameeleza baadhi ya mambo ya kupata wazo bora na la kipekee la biashara (unique business idea) ikiwemo kutumia ujuzi maarifa na kipi kinawasumbua watu wengi ili kukibadilisha kiwe fursa:

Tabiri nini kinafuata

Wakati ukijipanga kuwa na wazo bora la biashara ambalo utalifanyia kazi mwaka huu, Awadh anakuambia angalia na tathmini mwenendo wa biashara wa sasa ili kujua nini kinafuata mbeleni.

Hii itakupa fursa ya kupata mawazo ya biashara yanayoweza kukutoa mwaka huu, kuliko kuanza kufanya biashara yoyote iliyopo mbele yako.

Dunia inabadilika kila siku, teknolojia na njia za kufanya biashara zinabadilika. Ni vema kuzingatia mabadiliko yaliyopo katika eneo lako la biashara ili uendelee kuwepo katika soko la ushindani.

Kama usipozingatia mambo yanayotokea kwenye ulimwengu wa biashara, utajikuta ukiwekwa pembeni na mabadiliko hayo na biashara yako itaanguka. Picha|Helloquence/Unsplash.

Geuza changamoto kuwa fursa

Wazo la biashara litakuwa la tofauti na wengine kama litajielekeza kutathmini kwa kina matatizo au changamoto walizonazo watu kwenye jamii.

Awadh anaeleza kuwa hiyo ni fursa kwako kutoa suluhisho hasa kwa tatizo linalowatatiza watu wengi. Unaweza kuleta suluhisho la teknolojia rahisi ili kuwarahisishia maisha watu wengine wanaotaka kuboresha hali zao.

Pata muda wa kutafakari, ni mambo gani yanayohitaji msaada wako ili uyatatue na kupata kipato. 


Soma zaidi:


Achana na mambo yaliyopitwa na wakati

Utendaji wa biashara unabadilika kila siku kutokana na kuvumbuliwa kwa mifumo ya kidijitali ambayo inaongeza ufanisi kwa watumiaji. 

Awadh anakushauri wewe mmiliki wa biashara au unayetarajia kutekeleza wazo lako kuwa tathmini mambo ambayo unaona hayawezi tena kukuletea matokeo katika kipindi hiki na uachane nayo.

Kama usipozingatia mambo yanayotokea kwenye ulimwengu wa biashara, utajikuta ukiwekwa pembeni na mabadiliko hayo na biashara yako itaanguka.

Mwandishi wa vitabu na Kiongozi wa taasisi ya Global Thought Leadership ya Marekani, John Sviokla katika makala yake iliyochapishwa katika tovuti ya Strategy+Business, ametaja mambo matano ambayo yanaweza kukupa ishara kuwa mabadiliko yanatokea kwenye aina ya biashara unayofanya ikiwemo kubadilika kwa tabia za wateja wako ambao wataanza kutaka vitu vipya zaidi ya walivyovizoea.

Mabadiliko mengine ni kuvumbuliwa kwa teknolojia mpya za uzalishaji kwa muda mfupi; kuongezeka kwa ushindani; mabadiliko ya sera, sheria na kanuni za Serikali zinazosimamia biashara; ujio wa mifumo mipya ya uzambazaji bidhaa na huduma; na kampuni kongwe kujiboresha kuyafikia masoko mapya. 

Kipaji chako ukikitumia vizuri kinaweza kuwa wesehemu ya kukutengenea biashara inayolipa. Picha|Kyle Wong/Unsplash.

Badilisha kipaji chako kuwa biashara

Kama bado hujagundua kipaji, ujuzi au maarifa uliyonayo, basi mwaka 2020 utumie kujitathmini kile ulichonacho ambacho ni cha kipekee ambacho unafikiri ukikitumia vizuri kitaleta manufaa.

Kama una kipaji cha kuimba, basi wekeza nguvu zako katika kuimba kibiashara. Mfano unaweza ukaingia mkataba na baadhi ya hoteli kubwa jijini Dar es Salaam ukawa unatumbuiza siku za wikiendi kwa muziki ambao utaleta matokeo kwa wanaokusikiliza.

Wakati mwingine kile tulichokisomea darasani kinaweza kisiwe na mchango mkubwa katika mafanikio yetu lakini vipaji tulivyopewa na Mungu ambavyo vikinolewa vizuri vinaweza kuwa biashara kubwa inayolipa.

Pamoja na yote haya, utekelezaji wa wazo lako la biashara unategemea zaidi ulivyojipanga kutumia rasilimali zako vizuri hususan kutafuta mtaji ili ukusaidie kupata kile unachokitaka mwisho wa mwaka wa 2020.