July 8, 2024

Unayoweza kuyafanya usichukiwe na watu kupita kiasi

Watu wengi wanawachukia watu wanaojisifia kwa kila jambo.

  • Mitandao ya kijamii inaweza ikasababisha watu wakuchukie kutokana na masuala unayochapisha mara kwa mara.
  • Watu wengi wanachukia watu wanaojisifia kwa kila jambo.
  • Kuficha hisia zako katika mambo mbalimbali inaongeza watu wasiokupenda.

Mwanamitindo mahiri wa Marekani Paris Hilton aliwahi kusema kuwa “wakati watu wasiokufahamu wakikuchukia jua kwamba wewe ni zaidi yao.” 

Hata hivyo, swali muhimu la kujiuliza ni kwamba wanaokuchukia au wasiokupenda wameamua kufanya hivyo kwa sababu gani? 

Japo kila mtu anaweza akawa ana sababu zake za kukuchukia lakini kuna baadhi ya masuala ambayo wewe uyatendayo yanayochochea watu kutokukupenda. 

Fahamu mambo matano ambayo unayoyafanya au usiyoyafanya yanayoweza kusababisha watu wasikupende. 

Kuchapisha picha nyingi katika mitandao ya kijamii 

Uraibu wa kutumia mitandao ya kijamii imefanya baadhi yetu kutuma picha za maisha yetu kuanzia zile za familia, marafiki au kazini. Hapa unaweza kutuma picha za jinsi maisha yako yalivyo watu wakakuchukia kwa sababu wakatamani kuwa na maisha kama yako. Wengine wataona kama unajionyesha au kujitapa na mfumo wa maisha ambao hawajabahatika kuwa nao.

Unashauriwa kuweka baadhi ya mambo yako binafsi nje ya mtandao, itakuepusha pia na watu wasiopenda maendeleo yako na wanaoweza kutumia udhaifu wako katika kukurudisha nyuma kimaendeleo. 

Kujipiga picha ‘Selfie’ na kuziweka mtandaoni siyo vibaya lakini kuzichapisha kwa wingi kwenye mitandao ya kijamii kunawafanya baadhi ya watu kuona ni kero licha ya ukweli kuwa picha hizo haziwahusu. Picha| Africa Rising.

Kutaja majina ya watu maarufu unaowafahamu katika kila mazungumzo ya kawaida na watu

Ni dhahiri kuwa unaweza ukawa na ndugu au marafiki maarufu waliokaribu sana na wewe. Hata hivyo, wapo baadhi ya watu ambao katika stori zao za kila siku na watu lazima ataje mtu maarufu kumuonyesha kwamba anafahamika na watu. 

“Mimi nilikuwa naishi nyumba moja na …”, “Juzi tulikuwa na mheshimiwa…” kauli hizi zinafanya baadhi ya watu kukuchukia na kuona kuwa hauko sawa na wao na wataanza kukuepuka katika mazungumzo yao.

Pia, tabia hiyo inakufanya uonekane kama mtu uliyetegemezi kwa watu hao unawatajataja. Watu hawakawii kukuona mtu unayedandiadandia fursa za watu maarufu.

Kujisifia kwa nia njema 

Binadamu tumeumbwa kusifia hatua njema za maisha tulizofikia. Hii ni njia sahihi pia ya kujipa nguvu katika kuendelea na mapambano na maisha. Katika kusherehekea mafanikio hayo, wapo watu ambao wanatumia muda mwingi katika mazungumzo na wenzao katika kuonyesha wao ni bora kwa kueleza mazuri yake kila mtakapokuwa mnaiongea mada fulani. 

Busara ni kuwa baada ya baadhi ya watu kujua uliyoyafanya unaweza kuendelea kujikita kufanya vitu zaidi na uache wengine wakuzungumzie wenyewe.

Achana na kauli za “yaani nimefanya kazi sana mpaka nimefanikiwa” au “nimewasaidia watu wengi sana kufanya jambo fulani.” Kauli kama hizi zinafanya baadhi ya watu waanze kukuchukia wakihofia siku moja ukiwasaidia huenda ukawatangaza kama unavyofanya kwa wengine.

Kuficha hisia zako

Binadamu hutawaliwa na hisia ziwe furaha au huzuni. Hivyo kuficha hisia zako kwa kila jambo linalotokea kunaweza kukufanya watu wasikupende. 

Unaweza kuwa ni mtu ambaye hawezi kuonyesha huzuni, mshangao, furaha au kukasirika. Inashauriwa kuwa muwazi kwa kueleza hisia zako ili mtu asihisi kama haujali pale anapokuwa na jambo la furaha au huzuni.

Kutokutabasamu

Siyo wote tumejaliwa hulka ya kutabasamu kwa kila jambo zuri linalotokea mbele yetu lakini ni wachache wanaweza kuficha hisia zao za jambo la furaha. Tabasamu ni matokeo ya kufurahia jambo achana na lile ambalo kwetu Uswahili huita ‘tabasamu la kinafiki’ ambalo mtu hutabasamu aonekane anakufarahia jambo hajaridhishwa na jambo husika.

Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa watu waliwekewa picha kati ya mtu aliyenuna na aliyetabasamu wengi walichagua mtu aliyetabasamu kuliko aliyenuna. Hii inaashiria kuwa watu wasiotabasamu hupoteza mvuto wa kupendwa.

Hii ni moja ya sababu ya watu wengi kama wanasiasa hutabasamu sana wakiwa mbele za watu katika kampeni au majukwaani ili kuwafanya watu waweze kuwasikiliza na kuvutiwa nao.