October 7, 2024

Undani kuhusu meli mbili zitakazopeleka ahueni Ziwa Victoria

Kurejea kwa huduma za meli hizo, zilizokarabatiwa kwa Sh27 bilioni, zitapunguza maumivu kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa baada ya tabu ya takriban miaka sita.

  • Kurejea kwa huduma za meli hizo, zilizokarabatiwa kwa Sh27 bilioni, zitapunguza maumivu kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa.
  • Moja ya meli hiyo itakuwa na chumba maalum kwa ajili ya kuwahudumia kina mama na watoto.
  • Meli hizo zinaanza huduma Agosti 16 baada ya kusitisha kwa takriban miaka sita. 

Mwanza. Meli mbili zilizokuwa zimesitisha safari zake kwa takriban miaka sita ndani ya Ziwa Victoria, zinatarajia kurejesha huduma kuanzia Agost 16 mwaka huu huku mamlaka zikianza kutumia mfumo wa tiketi wa kielektroniki kuongeza ufanisi.

Meli hizo mbili za Mv (New) Victoria “Hapa Kazi Tu” na Mv Butiama “Hapa Kazi Tu”, zitakuwa zikifanya safari za kati ya Mwanza-Bukoba na Mwanza – Ukerewe baada ya ukarabati wake kukamilika. Meli zilisitisha huduma mwaka 2014.

Kurejea kwa huduma za meli hizo, zilizokarabatiwa kwa Sh27 bilioni, zitapunguza maumivu kwa wakazi wa maeneo hayo kutokana na kuwapunguzia gharama na kuwaokolea muda kutokana na uhakika wa safari.

Ukarabati wa meli hizo ulihusisha ufungaji wa injini mbili mpya, jenereta kubwa tatu, viti vipya vya kisasa, kubadili mfumo wa umeme na kupaka rangi kwa mujibu wa Mamlaka ya Huduma za Meli nchini (MSCL).

Ofisa Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo Eric Hamissi amesema ukarabati huo ulikamilika toka Aprili mwaka huu na kilichokuwa kikisubiriwa ni kutolewa kwa cheti cha ubora  kutoka Wakala wa Shirika la Meli Tanzania (Tasac) ili zianze kufanya kazi.

“Kwa sasa cheti hicho kimetolewa juzi (Agosti 11) na kuanzia Agost 16 zitaanza kazi kwa safari za Mwanza – Bukoba kwa meli ya Mv Victoria hapa Kazi tu na Mv Butima itahusisha safari za Mwanza- Ukerewe,” amesema Hamissi.

Mwonekano wa meli ya “Mv Victoria Hapa Kazi Tu” baada ya kufanyiwa ukarabati uliogharimu zaidi ya Sh22 bilioni, meli hiyo itarejea kazini kuanzia Agost 16 mwaka huu Kati ya Mwanza-Bukoba. Picha|Mariam John.

Hatua hiyo imekuja baada ya agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mapema Agosti 9 mwaka huu la kuitaka Tasac kutoa vibali vya ubora kwa meli hizo na kuagiza MSCL ndani ya wiki hii.

“Ninaagiza  hizi meli zianze kufanya kazi kwakuwa tayari zishafanyiwa majaribio na kuonekana kuwa zinafaa kuendelea na kazi,” alisema Majaliwa.

Katika maelezo yake, Hamissi anasema meli hizo zilisitisha safari zake Kutokana na uchakavu hali iliyosababisha wakazi wa Bukoba kutumia mabasi na malori kwa ajili ya kusafirisha mizigo.

Ukarabati wa meli hizo umefanywa na Mkandarasi wa ndani Songoro Marine kwa kushirikiana na Kampuni ya KMT CO.LTD kutoka Korea Kusini.  

Kongwe lakini shughuli yake ni ‘balaa’

Meli ya Mv Victoria iliyoundwa mwaka 1959 ina uwezo wa kubeba abiria 1,200 pamoja na Tani 200 za mizigo wakati meli ya Mv Butiama ina uwezo wa kubeba abiria 200 na Tani 100 za mizigo.

“Meli zote zimeboreshwa ndani ya meli kuna baa ambazo zimepewa heshima ya majina ya mbuga za wanyama kama Burigi Chato bar, Serengeti bar, pamoja na Ngorongoro bar, pia viti vyake vimeboreshwa na kuna sehemu kwa ajili ya kuchajia simu,” amesema Hamissi.

Mbali na hayo pia amebainisha kuwa ndani ya meli hiyo ya New Victoria kuna chumba maalum kwa ajili ya wazazi kwa maana ya mama na watoto wao pamoja na wajawazito (Martenity room).

 

Ahueni tena Ziwa Victoria

Baada ya meli ya Mv Victoria kusitisha safari zake abiria wengi walilazimika kutumia mabasi huku wakilazimika kulipa nauli kubwa ya mizigo iliyochangia kuongeza gharama za kufanya biashara.

Nauli ya mabasi kutoka Mwanza hadi Bukoba inakadiriwa kuwa wastani wa Sh20,000 kwa safari.

“Kwa mfano wafanyabiashara walilazimika kutumia Sh100, 000 kusafirishia tani moja ya mizigo lakini kwa sasa watalazimika kutumia Sh27,000 kwa tani hiyo hiyo moja ya mizigo kwenye meli,” anasema Hamissi.

Nauli kwa daraja la uchumi abiria atatozwa kiasi cha Sh16,000 wakati daraja la biashara 30,000 na daraja la kwanza atalazimika kulipia Sh45,000 huku watoto chini ya miaka 18 wakitozwa nusu ya nauli ya mtu mzima.

Abiria watakaokuwa wakisafiri na meli ya Mv Butima watalazimika kulipia ShSh10,000 kwa daraja la kwanza na Sh8,000 kwa daraja la pili.

 

Unachotakiwa kufahamu kuhusu safari

Meli ya New Victoria itatumia saa sita kwenda Bukoba na itakuwa inasafiri mara tatu kwa wiki kwa maana ya Jumatatu na itaandoka saa tatu usiku ikipitia kisiwa Cha Kemondo na kufika Bukoba  saa 11 alfajiri ya Jumanne.

Meli ya Mv Butiama itakuwa ikiondoka saa 9 alasiri kila siku na itatumia saa mbili kufika Nansio visiwani Ukerewe. Meli hii itakuwa inaanzia Ukerewe saa 2 asubuhi kwenda Mwanza ambapo itafika saa 4 asubuhi na kurudi Ukerewe saa 9 alasiri.


Zinazohusiana: 


Sahau risiti, sasa tiketi ni kielektroniki 

Tofauti na kabla hazijasitiza huduma za usafiri, ukataji wa tiketi utakuwa wa kielektroniki, jambo linalotarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma hizo.

Kaimu Meneja Idara ya Masoko wa MSCL, Filemon Bagambilaga amesema upatikanaji wa tiketi utakuwa wa aina mbili moja ni katika bandari za Mwanza Kaskazini, Kemondo na Bukoba na nyingine kwa njia ya mtandao.

“Mteja atalazimika kuingia kwenye website (tovuti) yetu na ataweza kufanya manunuzi ya tiketi kwa njia hiyo,” amesema Bagambilaga.

 

Vipi kuhusu kukuza utalii ndani ya Ziwa Victoria? 

Wadau wa utalii wanatarajia kurejeshwa kwa safari za meli hizo kutangia kukuza utalii katika kanda ya ziwa hasa baada ya sekta hiyo kuathiriwa na janga la ugonjwa wa virusi vya corona.

Mkuu wa bodi ya utalii Kanda ya Ziwa Gloria Milambo anasema kurejea kwa safari hizo pia kutasaidia kufufua maeneo ya utalii katika visiwa mbalimbali vilivyopo ndani ya Ziwa Victoria.

“Asilimia 50 ya watalii wanaoingia jijini Mwanza hupenda kutembelea Kisiwa cha Nansio kushuhudia jiwe linalocheza na wakati mwingine kwenda kusikiliza nyimbo za asili , ngoma na namna kabila la Wakerewe wanavyodumisha mila zao,” anasema Gloria.

Mbali na kutembelea maeneo, anasema watalii hupenda pia kutumia usafiri wa meli kutalii kati ya kisiwa na kisiwa, kuangalia uvuvi wa asili na mapori yaliyopaishwa hadhi mfano Burigi Chato.

Anasema watalii wengi wanaokuja hutokea Uganda hivyo kukosekana kwa meli ndani ya kipindi hicho kulipunguza idadi yao. Hata hivyo, Milambo hakutaja takwimu kamili ya watalii waliopungua kipindi hicho.