October 6, 2024

UNICEF yaonya kuongezeka ndoa za utotoni duniani

huenda kukawa na ndoa za utotoni milioni 10 kabla ya kumalizika kwa muongo huu na hivyo kutishia mstakabali wa elimu ya wasichana duniani.

  • Imeonya kuwa huenda kukawa na ndoa za utotoni milioni 10 kabla ya kumalizika kwa muongo huu.
  • Changamoto za kiuchumi, kuingiliwa kwa huduma, mimba na vifo vya wazazi kutokana na janga la COVID-19 kutachangia ongezeko hilo.
  • UNICEF inataka hatua madhubuti zichukuliwe sasa kabla hali haijawa mbaya zaidi. 

Ripoti ya mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) imeonya kuwa huenda kukawa na ndoa za utotoni milioni 10 kabla ya kumalizika kwa muongo huu na hivyo kutishia mstakabali wa elimu ya wasichana duniani. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyopewa jina “COVID-19: tishio kwa hatua zilizopigwa dhidi ya ndoa za utotoni”, kufungwa kwa shule, changamoto za kiuchumi, kuingiliwa kwa huduma, mimba na vifo vya wazazi kutokana na janga la COVID-19 vinawaweka wasichana walio katika mazingira magumu katika hatari ya ndoa za utotoni. 

Ripoti imesema kuwa hata kabla ya COVID-19 wasichana milioni 100 walikuwa katika hatari ya ndoa za utotoni katika kipindi cha miaka 10 ijayo  licha ya ndoa hizo kupungua kwa kiasi kikubwa katika baadhi ya nchi kwa  miaka ya hivi karibuni, kwa asilimia 15.

Kupungua kwa ndoa hizo ni sawa na ndoa milioni 25 zilizoepushwa, lakini sasa mafanikio hayo yanaweza yasifikiwe kikamilifu.  


Zinazohusiana:


Ripoti hiyo inasema wasichana wengi ambao wanaoolewa utotoni wanakabiliwa na changamoto lukuki za muda mfupi na za muda mrefu na wengi hukumbana na ukatili na pia kukatiza masomo.

Inaelezwa na ripoti hiyo kuwa janga la COVID-19 limezidisha adha ya ndoa hizo na duniani kote inakadiriwa kuwa wanawake na wasichana milioni 650 walio hai leo hii wamepitia ndoa za utotoni na nusu ya ndoa hizo zikitokea Bangladesh, Brazil, Ethiopia, India na Nigeria. 

 Hivyo UNICEF inataka hatua madhubuti zichukuliwe sasa kabla hali haijawa mbaya zaidi.