October 6, 2024

Uongozi shuleni ulivyochochea ndoto ya kijana wa miaka 19 kuanzisha kampuni ya nafaka

Alianzisha kampuni hiyo kupitia mfuko wa darasa wa kuwasaidia wanafunzi wasiojiweza alioanzisha akiwa shule ya sekondari Mtakatifu Anthoni Mbagala jijini Dar es Salaam.

  • Anasomea masomo ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) akiwa na umri wa miaka 19
  • Alianzisha kampuni hiyo kupitia mfuko wa darasa alioanzisha akiwa shule ya sekondari.

Dar es Salaam. Wakati Serikali na wadau mbalimbali  wakiendelea kusisitiza juu ya vijana kutumia changamoto kutengeneza fursa, baadhi ya vijana kama Richard Caesar hawako nyuma katika  jitihada hizo za kujiari.

Richard (19) ni miongoni mwa vijana waliojiongeza katika suala zima la kuchangamkia fursa kupitia nafasi aliyopata akiwa anasoma shule ya sekondari ya Mtakatifu  Anthony Mbagala jijini Dar es Salaam wakati huo akiwa na umri wa miaka 15 tu.

Akiwa shuleni hapo mwaka 2015 aliamua kugombea Ubunge wa darasa  ambapo aliamua kuja na sera itakayowavutia wanafunzi na kuwaletea mabadiliko endapo angepata nafasi ya kuwaongoza.

Moja ya sera alizokuja nazo Richard ni kuunda mfuko wa darasa ambao ungesaidia wanafunzi wasiojiweza kutatua changamoto zao za kila siku kupitia mikopo midogo midogo na kupata pesa za matumizi wanapokuwa shuleni.

Hata Hivyo, baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari, Richard hakuishia hapo, yeye pamoja na wanafunzi wenzake waliamua kuendeleza mfuko huo ukiwa na kiasi cha Sh4,900  ambapo kupitia mfuko  alifanikiwa   kuanzisha  kampuni ya nafaka iitwayo Nohindu Company Limited.

“Kwa kweli wakati naanzisha ule mfuko sikuwa na lengo jingine zaidi ya kutimiza ahadi zangu kwa watu walionichagua. Sikujua kama ningekuja miaka miwili baadaye kuwa na kampuni nje ya mfuko,” amesema Caesar.


Zinazohusiana:


Nohindu ni kampuni inayosambaza bidhaa za nafaka na chakula kama mchele, dagaa, maharage, mahindi pamoja na mbogamboga za kila aina. Mteja huweza kupata huduma hiyo kwa kutembelea mitandao ya kijamii ya kampuni hiyo na kuchagua bidhaa anayotaka na kisha kufikishiwa popote alipo.

Mpaka sasa Nohindu imeweza kufikia maduka yasiyopungua matano katika soko eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam na wateja wengine kwenye  maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam.

Richard anayechukua masomo yake ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) akiwa ndiyo kwanza amejiunga mwaka huu  lakini bado kampuni inaendelea kwani ameajiri wafanyakazi wengine wanaendelea kufanya shughuli za usambazaji bidhaa huku akiwasimamia kupitia mawasiliano ya simu. 

“Sasa hivi kila kitu ni rahisi, kwa sababu ya simu na teknolojia. Kila kitu watakachofanya wenzangu lazima kipitie kwangu kwanza licha ya kuwa mbali,” amesema Caesar.

Changamoto kubwa anayokumbana nayo katika uendeshaji wa kampuni ni ukosefu wa mtaji wa kuhudumia wateja wakubwa kama hoteli.

Richard ameimbia Nukta kuwa amewahi kupata tenda nyingi za hoteli kutaka huduma za nafaka, lakini ameshindwa kuwasambazia kutokana na kuwa na mtaji mdogo wa kutoa huduma hiyo.

Pamoja na kampuni hiyo kufikia hatua iliyopo bado ana matamanio na malengo makubwa ya kupata wawekezaji watakaowekeza katika kampuni hiyo, ili izidi kukuwa na kufika mahali fulani pazuri zaidi ya ilipo hivi sasa. 

“Natamani sana tupate wawekezaji, ili malengo makubwa zaidi yaweze kutimia kwa ufasaha. Kuna wateja wengi wanatamani kupata huduma zetu lakini kutokana na kuwa na  uzalishaji mdogo inatuwia ngumu kuwahudumia,” amesema Caesar. .

Bado Richard ana kazi kubwa ya kutatua changamoto hiyo, na kuhakikisha ana uwezo wa kuhudumia wateja wote wenye uhitaji na kufika lile lengo analotamani kulifikia kwa miaka ijayo.