October 6, 2024

Upatikanaji wa ajira kwa vijana bado kitendawili Tanzania

Programu za ujuzi, ufundi stadi zinawaweza kupunguza tatizo la ajira nchini.

  • Vijana wengi wanaomaliza masomo yao katika ngazi mbalimbali za elimu wanahaha kusaka ajira.
  • Programu za ujuzi, ufundi stadi zinawaweza kupunguza tatizo la ajira nchini.

Dar es Salaam. Wakati akihitimu masomo ya elimu ya juu alitarajia kuwa angepata ajira mapema ambayo ingempatia angalau fedha za kujikimu na maisha. 

Zaidi ya miaka mitatu tangu amalize masomo hayo ya elimu ya juu, Jane*, bado anahaha kutafuta kibarua. Ndoto yake ya kupata ajira yenye staha imefifia. 

Jane (siyo jina lake halisi) alisomea Shahada ya mipango ya makazi na miundombinu katika Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) ambayo kipindi anajiunga na masomo alijua itampa dili haraka mara tu baada ya kuhitimu mwaka 2016.  

Kwa kuwa pia ni binti, aliamini kuwa kusingekuwa na ushindani mkubwa sokoni kutokana na ukweli kuwa wanawake ni wachache katika sekta ya ujenzi na miundombinu ikilinganishwa na wanaume. Mipango si matumizi, miaka zaidi ya mitatu sasa ndoto yake haijatimia. 


Safari yake ya kutafuta ajira imekuwa siyo rahisi kwa sababu ametuma maombi mengi ya kazi bila mafanikio na kufikia hatua y
a kukataa tamaa na kukaa tu nyumbani. 

Anawakumbuka marafiki na ndugu zake waliomshauri asomee ualimu wa kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwemo wasioona, lakini muda haumruhusu tena kuwa darasani.

“Nina rafiki yangu ambaye sasa ni mwalimu, ingawa yuko kijijini huko Manyara lakini amefungua miradi mingi inayomuingizia kipato,” anasema Jane.

Hata wakati Jane akisubiri labda siku moja ajira itamdondokea, ameingia mtaani kufanya biashara ya kuuza nguo za wanawake ili kujipatia japo kipato cha kuendesha maisha yake.

Yeye ni miongoni mwa maelfu ya vijana nchini Tanzania ambao wanahaha kusaka ajira kujipatia kipato lakini kwa bahati mbaya fursa za ajira zinazotengenezwa kwa sasa hazilingani na mahitaji. 

Hali hiyo inakuja licha ya jitihada za Serikali na wadau wengine mbalimbali wa maendeleo kufungua fursa mbalimbali za ajira kwa vijana jambo linaloonyesha bado kuna safari ndefu ya kutokomeza ukosefu wa ajira nchini kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya vijana wanaoingia sokoni.


Zinazohusiana:


Vijana ndiyo kundi lenye watu wengi nchini na huchangia kwa sehemu kubwa nguvu kazi ya Taifa inayohitajika katika shughuli za uzalishaji mali ili kuboresha maisha na kukuza uchumi wa nchi. 

Makadirio ya idadi ya watu Tanzania kati ya mwaka 2013 hadi 2035 yaliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), yanaonyesha kuwa  idadi ya vijana walio na umri wa miaka 15-35 mwaka 2019 itakuwa asilimia 34.6 ya watu wote nchini na inataongezeka hadi kufikia asilimia 35.6 mwaka 2025. 

Hii ina maana kwa sasa zaidi ya theluthi moja au mtu mmoja kati ya watu watatu nchini ni kijana mwenye umri kati ya miaka 15 na 35 ambaye ama anamalizia masomo au ameshaingia kwenye soko la ajira kujenga mustakabali wa maisha yake.  

Vijana ni nguvukazi inayohitajika zaidi katika ujenzi wa uchumi ikizingatiwa kuwa Serikali imedhamiria kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati ifikapo mwaka huo wa 2025.

Hata hivyo, hali ya mtaani bado siyo nzuri sana, kwa sababu vijana wengi wanaomaliza masomo yao katika ngazi mbalimbali hawana kazi kutokana na kasi ya uzalishaji wa ajira kutoshabihiana na mahitaji ya ajira nchini. 

Ripoti ya Takwimu Muhimu za Tanzania (Tanzania in Figure 2018) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kiwango cha watu wasio na ajira Tanzania mwaka 2018 kilikuwa ni asilimia 9.7 ikiwa imepungua kidogo kutoka asilimia 10.1 mwaka 2015.

Hii inamaanisha kuwa kwa kila watu 10 wenye uwezo wa kufanya kazi basi takriban mtu mmoja hana ajira nchini. 

Pia kufanya kazi kwenye sekta isiyo rasmi au kujiajiri kwa kufanya biashara imekuwa ni vigumu kutokana changamoto za kupata mitaji, nyenzo na mahali pa kufanyia kazi zao.

Benki ya Dunia (WB) inakadiria vijana wapatao 800,000 huingia katika soko la ajira Tanzania kila mwaka lakini ni takriban asilimia 10 tu ndiyo hufanikiwa kupata kazi. 

Suala la ongezeko la vijana wasio na ajira ni jambo linaloumiza vichwa vya wengi wakiwemo viongozi wa Serikali na jamii kwa ujumla, licha ya sera na sheria mbalimbali kuainisha kupata kazi kama haki muhimu kwa vijana.

Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 inaeleza kuwa kijana ana haki ya kupata kazi na ujira wa haki ili kumudu maisha yake kwa sababu jamii inategemea kumuona akishiriki katika shughuli za maendeleo na kuanza kujitegemea kwa kiasi fulani.

Sehemu ya waombaji zaidi ya 10,000 wa nafasi ya Mkaguzi Msaidizi, Idara ya Uhamiaji wakifanya usaili wa awali wa kuandika ulioandaliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ajili ya kujaza nafasi 70 za kazi ambazo zinahitajika katika Idara hiyo.Picha |

Tatizo ni kubwa zaidi kwa wasomi

Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana inaeleza kuwa vijana walio wengi, asilimia 60 ya wale wote wasio na ajira rasmi hawana kazi maalum. Hali hii imekuwa na matokeo tofauti kwa vijana na wengine kupoteza kabisa mustakabali wa maisha yao.

Baadhi hujiingiza katika vitendo viovu kama vile wizi, ujambazi, uzururaji, uvutaji bangi, utumiaji wa madawa ya kulevya, umalaya n.k,” inaeleza sehemu ya sera hiyo.

Aidha, baadhi ya vijana hasa wasomi wa vyuo vikuu wameendelea kuwa tegemezi kwa wazazi wao hasa katika maeneo ya mijini. 

Pia ukosefu wa ajira kwa vijana ni moja ya changamoto kubwa ya usalama nchini Tanzania, ikizingatiwa kuwa ni rahisi vijana wasio na mweleko kujiingiza katika uhalifu.

Serikali, wadau wanatafuna mfupa mdogo mdogo

Hata wakati, ukosefu wa ajira kuwa kilio kikubwa kwa vijana, Serikali na wadau wa maendeleo ikiwemo sekta binafsi wameendelea kutoa fursa mbalimbali za ajira ili kupunguza tatizo hilo kwenye jamii.

Katika siku za hivi karibuni, Serikali imekuwa ikitumia miradi mikubwa kama ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), majengo ya Serikali jijini Dodoma kutengeneza ajira mpya. 

Kwa mujibu wa ripoti ya Takwimu Muhimu za Tanzania (Tanzania in Figure 2018)  jumla ya ajira 552,063 zilizozalishwa nchini mwaka 2017/18 kulikuwa ikilinganishwa na ajira 453,466 kwa mwaka 2016/17. 

Kati ya ajira zilizozalishwa mwaka 2017/18, asilimia 75 zilikuwa ni ajira kutoka Serikalini; zikijumuisha ajira 18,000 kutoka Serikali Kuu na ajira 397,009 kutoka katika miradi ya maendeleo kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 hadi 2020/21. 

“Hali hii inatokana na ukweli kuwa wananchi wengi huajiriwa kwenye miradi ya kimkakati ya maendeleo inayoendelea hapa nchini ambapo Serikali imejikita kwa dhati kuitekeleza kwa ajili ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na kupunguza umaskini,” inaeleza sehemu ya taarifa ya NBS kuhusu ripoti ya Tanzania in Figure 2018.

Kwa upande wa sekta binafsi, mwaka 2017/18 ilizalisha ajira 137,054 sawa na asilimia 25 ya ajira zote zilizozalishwa. Hata hivyo, ajira zilizozalishwa na sekta hiyo inayotegemewa zaidi kutoa ajira ulimwenguni zilipungua kutoka ajira 239,017 zilizozalishwa mwaka 2016/17.

Nini kifanyike kuokoa jahazi?

Katika kipindi hiki cha ukosefu wa ajira, bado vijana na sehemu ya kufanya kuzitatua changamoto zinazowakabili ili kuboresha maisha yao.

Vijana wametakiwa kuangalia fursa nyingine za kujiajiri na kuwa huru kufanya shughuli za ujasirimali ambazo zitawasaidia kuinuana kuliko kusubiri ajira za serikalini na sekta binafsi ambazo hazitoshelezi mahitaji yao ikizingatiwa kuwa idadi yao inaongezeka kila mwaka. 

“Wanatakiwa wajiongeze, wajiajiri wenyewe kwa aina moja au nyingine ikiwemo kuanzisha biashara yako mwenyewe ambayo inaweza kuajiri watu wengi ili kuongeza ajira zaidi,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Ekihya, Lilian Madeje ambaye ni mdau wa masuala ya vijana.

Katika kujiajiri, vijana wanaweza kutumia vipaji na ujuzi walivyonavyo kubaini na kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii. Mfano wanaweza kutumia changamoto ya mabadiliko ya tabianchi kutoa suluhisho la uharibifu wa mazingira katika maeneo yao. 

Pia mashirika ya kijamii nayo yamekuwa yakianzisha programu mbalimbali za kuwaongezea ujuzi na maarifa vijana ili kujiajiri katika shughuli za ufundi na ujasiriamali kupunguza ukali wa maisha. 

Pamoja na jitihada hizo, bado idadi ya vijana wasiofikiwa na fursa za ajira ni kubwa ikizingatiwa kuwa idadi yao inaongezeka kwa kasi, ikilinganishwa na jitihada zinazochukuliwa kuboresha maisha yao. 

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hususan waajiri na wafanyakazi, sekta binafsi, washirika wa maendeleo pamoja na vyama vya kiraia inaendelea kutekeleza programu zinazowezesha kuibua fursa zaidi za ajira. 

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshugulikia Maendeleo ya Jamii Dk John Jingu amesema kuwa dhana ya uanagenzi inaweza kuwa suluhisho la kuhakikisha mifumo yetu ya elimu inazalisha wataalamu mahiri wenye ujuzi au stadi zinazohitajika katika soko la ajira.

Amesema kuwa Serikali imeona umuhimu wa kushughulikia changamoto ya kuzalisha wahitimu wasioajirika kwenye sekta rasmi na isiyo rasmi kwa kuanzisha dhana ya uanagenzi kwenye taasisi na vyuo vya maendeleo ya jamii itakayosaidia kupata wataalam wenye ubora unaohitajika.

Dkt. Jingu amesisitiza kupitia mifano ya nchi za Ujerumani na Rwanda ikionesha kuwa uanagenzi umewezesha kutoa matokeo chanya. 

Ujerumani waliingiza dhana hii katika mfumo wa elimu ambapo imesaidia asilimia 60 ya wanafunzi wanaomaliza vyuo kuweza kujiajiri wenyewe kutokana na ujuzi na uzoefu wa kazi wanaoupata wakiwa masomoni kwa kupitia njia hiyo.