Ushindani biashara ya chakula mtandaoni wazidi kuibua fursa lukuki Tanzania
Baada ya Jumia Food kufungasha vilago Tanzania, zaidi ya kampuni nne zainyakua fursa ya biashara hiyo mtandaoni
- Inawarahishia wamiliki wa migawaha na hoteli kuwafikia wateja wao kwa haraka.
- Inatengeneza fursa za ajira kwa vijana wabunifu wa teknolojia na wasambazaji wa chakula.
- Wanunuzi nao wanaokoa muda na gharama za kwenda migahawani.
Dar es Salaam. Baada ya kampuni ya Jumia iliyokuwa ikitoa huduma za uagizaji wa vyakula mtandaoni kufungasha vilago Tanzania, biashara ya kuuza na kuagiza vyakula mtandaoni imeshika kasi nchini hasa katika jiji la Dar es Salaam, jambo liliongeza ushindani na kufungua fursa mbalimbali za biashara kwa wamiliki wa migahawa na hoteli.
Biashara hiyo siyo tu inawafaidisha wasambazaji wa vyakula, bali hata wanunuzi ambao ambao huokoa muda na gharama za kufuata chakula kwenye migahawa badala yake kinawafuata popote walipo kwa kutumia programu tumishi (Apps) kwenye simu zao.
Kadri siku zinavyoenda ushindani unazidi kuchachamaa huku kampuni nyingi za vijana zikiwekeza zaidi katika fursa hiyo mpya ya teknolojia.
Baadhi ya programu hizo ni pamoja na Piki iliyoanzishwa takriban mwezi mmoja na nusu uliopita na vijana wa Tanzania inayomwezesha mtu kuagiza chakula mtandaoni na kuletewa mahali popote alipo kwa muda mfupi.
Sambamba na kampuni hiyo kuna kampuni nyingine tatu Yamee, Msosi express na Food Sasa ambazo zinatoa huduma ya chakula kwa kushirikiana na wamiliki wa migahawa na hoteli waliosajiliwa katika programu hizo.
Hata wakati kampuni hizo zikiendelea kuchuana katika soko, ni kampuni moja tu ya Piki iliyofanikiwa kufanya kazi katika zaidi ya mkoa mmoja, ambapo sasa iko Dar es Salaam, Arusha na Mwanza huku zilizobaki zikitoa huduma Dar es Salaam pekee. Msosi Express yenye inafanya kazi Arusha pekee.
Wachambuzi wa masuala ya teknolojia na biashara ya chakula wameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa ongezeko la kampuni zinazotoa huduma ya chakula mtandaoni kunafanya migawaha na hoteli zitafakari njia tofauti na walizozoea kuwafikia wateja wao ili kuendelea kuwepo katika soko la ushindani.
Ukuaji biashara ya chakula mtandaoni ni fursa pia kwa waendesha biashara za vyakula ikiwemo wamiliki wa migahawa. Picha | Mtandao.
“Wateja wa kununua chakula mtandaoni moja kwa moja wanaongezeka kutokana na kampuni hizo kutaka wateja wa kutosha kutoka migahawa mbalimbali nchini,” anasema Paul Madela, Mkuu wa Operesheni na Ufundi wa Kituo cha Ubunifu cha Buni Hub jijini Dar es Salaam.
Madela amesema ushindani huo unaweza kuwafaidisha zaidi wanunuzi kwa sababu bei za vyakula itapungua katika hoteli mbalimbali kutokana na uwepo wa kampuni nyingi zinazotoa huduma hiyo mtandaoni kuongezeka.
Tovuti ya McKinsey & Company katika moja ya makala zake za uuzaji vyakula mtandaoni inaeleza kuwa kuongezeka kwa kampuni zinazouza chakula mtandaoni kunatengeneza fursa nyingi za biashara na ajira kwa watu.
“Ulimwenguni, soko la usambazaji wa chakula linasimama kwa gharama ya Euro bilioni 83 (Sh, au asilimia moja ya soko la jumla la chakula na asilimia 4 ya chakula kinachouzwa kupitia mikahawa na minyororo ya chakula cha haraka.
“Biasharaa hii imekwisha kukomaa katika nchi nyingi na kiwango cha ukuaji wa kila mwaka kinakadiriwa kuwa asilimia 3.5 tu kwa miaka mitano ijayo,” inaeleza sehemu ya makala hiyo.
Hata hivyo, ukuaji biashara ya chakula mtandaoni ni fursa pia kwa waendesha biashara za vyakula ikiwemo wamiliki wa migahawa kwani wana nafasi ya kufikia wateja wengi kwa urahisi na haraka kupitia huduma za uagizaji kwa njia ya mtandao (Online food delivery).
Hii inasaidia kuwaondolea changamoto ya kuwasubiri wateja waende katika maeneo yao. Pia , mbali na kuwanufaisha wafanyabiashara, ni rahisi kupima vizuri ukuaji wa soko kwa kutumia mifumo ya kidijitali.
Unayotakiwa kuzingatia kujiunga na biashara hiyo
Wamiliki wa Apps za chakula wanasema hakuna vigezo vyovyote vigumu anavyotakiwa kuwa navyo mmiliki wa mgahawa ili kujiunga na huduma hizo zaidi ya kukubaliana na masharti ya kampuni husika ikiwemo kuandaa chakula kwa viwango vilivyowekwa na Shirika la viwango Tanzania (TBS).
Sambamba na hilo hakuna gharama zozote anazoweza ingia mmiliki wa mgahawa ili kufanya kazi na kampuni hayo kwani moja ya sababu ya uwepo wa makampuni hayo ni kuhakikisha walaji wanapata huduma za vyakula kulingana uhitaji walionao kwa muda muafaka.
Kwa mujibu wa kampuni hizo, mmiliki mgahawa anatakayejiunga na programu hizo tumishi ataongeza asilimia 15 ya bei ya chakula chake kwa ajili ya kuchangia gharama za uendeshahi wa program hizo tumishi.
- Huyu ndiye muuza biriani kidijitali Dar
- Biashara ya mtandaoni ni tishio kwa maduka makubwa Tanzania?
Wamiliki wengi wa program hizo wanavyotamani kufikia migahawa inayopika vyakula asilia ili kuteka soko la walaji kwani siku zote wateja ni mchanganyiko siyo tu wale wanaotaka kupata huduma za vyakula kutoka mahoteli ya kifahari.
“Kati ya vitu tunavyotamani ni kufikia pia wauzaji wa ‘Local foods’ kwani tunaamini kuna baadhi ya watu wanaohitaji vyakula hivyo na labda inaweza kuwa ngumu kupata kutokanana na muda walionao kutafuta.” amesema Frank.Maston, Meneja Mawasiliano na Masoko wa Yamee.