Usikose kutazama filamu hizi wikiendi
Wakati “Ip Man” ikikufundisha umuhimu wa kufikiria kabla ya kutenda jambo, “Onward” itawafundisha watoto jinsi ya kujiamini na umuhimu wake.
Hata baada ya kujaribu kumrudisha baba yao, Ian na Barley walimrudisha nusu kiwiliwili. Picha| National review.
- Ni filamu za “Ip Man” na “Onward”zifaazo kwa mapumziko wikiendi.
- Sehemu ya mwisho ya filamu ya Ip Man itakufundisha umakini katika kila kitu unachokifanya
- Filamu ya watoto ya “Onward” siyo ya kukosa kwani watoto wako watajifunza jinsi ya kujiamini na kupigania wanachokipenda.
Dar es Salaam. Kompyuta yako, weka kule. Kalamu na karatasi zako, weka kule! Ni wikiendi na ni wakati wa kupumzika baada ya mvua kubwa, jua kali na mchanganyiko wa kila aina ya vurugu za wiki nzima.
Kama wewe ni mdau wa filamu, kampuni ya Century Cinemax kupitia kumbi zake za kuangalizia filamuzilizopo kwenye maduka makubwa (malls) ina filamu mbili za “Ip Man” na “Onward” kwa ajili yako wikiendi hii.
Kama umewahi kutazama sehemu tatu za filamu hii, tamati yake imefika.
Baada ya Ip Man (Donnie Yen) kufiwa na mke wake, anagundua kuwa ana kansa ya koo ambayo imesababishwa na uvutaji wake wa sigara.
Anaamua kusafiri hadi jiji la San Fransisco lililopo Marekani ambako mwanafunzi wake Bruce Lee amezitibua jamii za “Kung Fu” nchini humo baada ya kufungua shule inayofundisha Wamarekani Kungfu aina ya “Wingchun” au “Wushu” na kuandika kitabu cha Kiingereza kinachofundisha sanaa hiyo ya kupigana kwaajili ya ulinzi binafsi.
Kumbuka kwamba, walimu wa “Kung Fu” wanatakiwa kufundisha wanafunzi wa Kichina tu hivyo anachokifanya Bruce Lee ni makosa.
Hofu ya matumizi mabaya ya sanaa hiyo inatawala kwenye jamii zinazofundisha masomo hayo.
Shuhudia matofali matatu kuvunjika kwa mgumi moja huku kipigo cha mbwa koko kikitembezwa kwenye mitaa ya jiji la San Fransisco. Unakosaje?
Zinazohusiana
- “Just Mercy”: Filamu ya machungu ya walioonewa gerezani
- Unataka kujua kusudi lako la kuishi? Tazama filamu hii
- “Queen and Slim”: Filamu mahususi kwa sikukuu ya wapendanao
Kama siyo mdau wa filamu za ngumi, basi katuni ziko kwa ajili yako na familia yako. Wikiendi hii katika kumbi za sinema hutaikosa filamu ya katuni ya Onward mahsusi kwa watoto.
Wataona nini?
Ian Lightfoot (Tom Holland) ni kijana ambaye ndiyo kwanza ametimiza miaka 16. Hata hivyo, Ian hana imani na mambo yote anayoyatenda na hivyo kukosa uhakika wa kila kitu.
Katika kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa, Ian na kaka yake Barley Lightfoot wanapewa mti wa miujiza ambao ulitengenezwa na baba yao Wilden kabla hajafariki.
Mti huo una uwezo wa kumrudisha Wilden kwa saa 24 duniani hivyo aliubuni mahususi ili aonane na watoto wake.
Katika majaribio ya kumrudisha baba yao kwa saa kadhaa, mambo yanaenda kombo hivyo anarudi kuwa nusu yaani miguu hadi kiuno.
Safari ya kutafuta dhana za kukamilisha mwili wa baba yao inaanza huku mama yao Laurel Lightfoot (Julia Louis-Dreyfus) akiweweseka juu ya kupotea kwao.
Wataweza kuzipata dhana wanazo zitafuta? Kutokujiamini kwa Ian kutasababisha nini? Funga safari na wanao mkatazame filamu hii