Usiyoyajua kuhusu shule iliyoshika nafasi 10 kidato cha nne
Imeingia kumi bora kwa shule zilizo na wanafunzi zaidi ya 40 kwa mara ya kwanza toka ilipoanzishwa.
- Imeingia kumi bora kwa shule zilizo na wanafunzi zaidi ya 40 kwa mara ya kwanza toka ilipoanzishwa.
- Imetoa mchuano mkali hasa kufaulisha wanafunzi daraja la kwanza la alama saba.
- Nidhamu, ushirikiana na kufuata ratiba vyaibeba shule hiyo.
Dar es Salaam. Shule ya Wavulana ya Musabe inawezekana ni jina geni masikioni mwa Watanzania wengi baada ya kusikika katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2019, baada ya kuingia katika orodha ya shule 10 bora kitaifa.
Hata hivyo, shule hiyo iliyopo jijini Mwanza ilianza kufanya vizuri muda mrefu, japo haikufikia hatua ya kuingia10 bora kitaifa.
Upekee wa shule hii ni kuwa imeweza kuchauna vikali na shule kongwe hasa zile zinazomilikiwa na watu binafsi ambazo zimekuwa zikitawala orodha hiyo ya dhahabu, licha ya kuwa ilikuwa na wanafunzi wengi waliohitimu kidato cha nne mwaka jana.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), shule hiyo ilikuwa na watahiniwa 118 kati yao wanafunzi 108 walipata daraja la kwanza na waliobaki wamepata daraja la pili.
Kama hiyo haitoshi, kati ya wanafunzi waliopata daraja la kwanza, 14 walipata daraja la kwanza la alama saba wakichuana vikali na shule za Kemebos na St. Francis ambazo zote ziko kwenye 10 bora kitaifa.
Kuibuka kwa shule hiyo, ndio kumeacha maswali mengi kwa watu ambao wamezoea kuziona shule zile zile kila mwaka kwenye 10 bora. Mwaka 2018 ilikuwa ya 31 kitaifa lakini mwaka jana ikapanda zaidi hadi katika nafasi ya 10.
Matokeo hayo sio haba ukilinganisha na matokeo yao ya huko nyuma licha ya kuwa iliwahii kuingia 10 bora mwaka 2016 kwa upande wa shule zilizo na wanafunzi chini ya 40 ambapo ilishika nafasi ya sita kitaifa.
Musabe isiyosikika sana kwa wengi lakini imekuwa ni shule ambayo inafaulisha wanafunzi wake vizuri kwa miaka minne mfululizo sasa ambapo wanafunzi wake wamekuwa wakifaulu kwa mwendo wa daraja la I na II.
Mwaka 2017 shule hiyo ilishika nafasi 14 kitaifa ikiwa na wanafunzi 50. 30 kati yao walipata daraja la kwanza na 17 daraja la pili. Mwaka uliofuata ufaulu ulishuka kidogo ikiwa na 31 kitaifa huku waliopata daraja la kwanza walikuwa 22 kati ya wanafunzi 81 waliofanya mtihani huo.
Zinazohusiana.
- Walichokisema wadau wa elimu ufaulu matokeo kidato cha nne.
- St. Francis yavunja rekodi yake yenyewe kidato cha nne 2019.
Nini kimeibeba shule hiyo?
Meneja wa Shule ya Sekondari ya Musabe, Daniel Damian ameimbia www.nukta.co.tz kuwa siri ya mafanikio ya shule yao ni uwekezaji mzuri uliofanya katika shule hiyo.
Amesema jitihada za shule za kuhakikisha wanapatikana walimu wa kutosha na wazuri wa kufundisha wanafunzi ni mmoja ya siri ya kufanya vizuri.
‘’Kama shule binafsi tumewekeza katika kupata walimu walio bora na wazuri, pia tunafuatilia kuhakikisha kila mwanafunzi anafanya jitihada katika kujifunza.’’amesema Damian.
Pia amesema msingi mwingine ni nidhamu kwa wanafunzi pamoja na kufuata ratiba kwa katika kila jambo lililopangwa kwa wakati shuleni hapo.
“Kama ni wakati wa michezo au kusoma mwanafunzi anatakiwa kuwa katika eneo hilo kwa muda uliopangwa,” amesisitiza Meneja huyo.
Musabe itaendeleza ubabe wake wa kuchuana na shule zilizojiimarisha kwa muda mrefu katika orodha ya 10 bora na hata kushika nafasi ya kwanza kitaifa mwaka 2020?