October 6, 2024

Utapiamlo kikwazo Tanzania kufika uchumi wa kati 2025

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameutaja utapiamlo kama moja ya vikwazo vitakavyokwamisha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 kama lishe bora haitozingatiwa kwa Watanzania.

  • Utapiamlo unasababisha udumavu wa akili na uwezo kufikiri unaohitajika katika uzalishaji.
  • Ukosefu wa lishe bora unadhoofisha nguvukazi ya Taifa.
  • Wadau washauri lishe bora iwe ajenda ya kitaifa kuelekea uchumi wakati.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameutaja utapiamlo kama moja ya vikwazo vitakavyokwamisha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 kama lishe bora haitozingatiwa kwa Watanzania. 

Majaliwa aliyekuwa akizungumza Oktoba 4, 2019 wakati akifungua mkutano wa mwaka wa wadau wa lishe Jijini Dodoma, amesisitiza lishe bora kwa Watanzania wote kwani afya njema ni muhimu katika kuongeza uwezo wa kuelewa na ubunifu.

“Pamoja na tafiti kuonesha kwamba tumepunguza viwango vya udumavu na upungufu wa damu bado viwango vyake havikubaliki kimataifa. Vilevile, tuna viwango vya utapiamlo ambavyo vimezidi kuongezeka na havikubaliki kimataifa ikiwemo uzito uliozidi kwa wanawake wenye umri wa kuzaa,” amesema Majaliwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, utapiamlo una athari kubwa katika ukuaji wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na hivyo kuathiri ukuaji, elimu na mustakabali wao.

Hata hivyo, Majaliwa amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutoa kipaumbele kwa maeneo ambayo yameathirika zaidi na ambayo yanatekeleza  miradi inayolenga kupunguza udumavu kwa watoto.

Ushirikiano huo pia utaelekezwa kwenye miradi inayopambana na matatizo ya upungufu wa vitamini na madini ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inaleta matokeo chanya katika maeneo hayo.


Zinazohusiana


Majaliwa amewataka wawekezaji na wamiliki wa miradi hiyo  kuitengenezea mikakati thabiti ya utekelezaji ikiwa ni pamoja na kutenga rasilimali za kutosha na kuibua mikakati itakayosaidia kupunguza tatizo la utapiamlo.  

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayesimamia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema bila kuwa na nguvu kazi yenye lishe na afya bora Taifa haliwezi kufanikiwa.

Mhagama ameorodhesha elimu, kilimo na viwanda kuwa baadhi ya sehemu zinazohitaji nguvu kazi yenye lishe ambapo zikikosa nguvu kazi hiyo, jitihada za Serikali za kujenga uchumi wa viwanda zitakwama.

“Juhudi za pamoja zinahitajika ili kuweza kufikia malengo tuliyojiwekea katika Mpango Jumuishi wa Taifa wa Lishe (2016/17 – 2020/21), ambayo ni pamoja na kupunguza udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kufikia asilimia 28 na uzito uliozidi kufikia asilimia 30,” amesema Mhagama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na Wadau wa Lishe baada ya kufungua Mkutano wa  Wadau wa Lishe kwenye Ukumbi wa Kambararage, Hazina jijini Dodoma, Oktoba 3, 2019. Kushoto kwake ni Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda na kulia kwake ni  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, udumavu umepungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2015 na kufikia asilimia 31.5 mwaka huu.

Licha YA kupungua kwa udumavu, changamoto iliyopo sasa ni suala la unyonyeshaji kwa watoto walio na umri wa chini ya miezi sita ambapo wanaonyOnyeshwa ni asilimia 58 tu.

Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda amesema katika jitihada za kupambana na umasikini ni vema elimu ya lishe bora ikatolewa kwa wananchi wote.

Pinda amegusia mila potofu kama moja ya visababishi vya utapiamlo na hivyo amemshauri Majaliwa aibebe agenda ya lishe kama njia ya kutokomeza utapiamlo na kuinua uchumi wa Tanzania.

Amesema katika familia nyingi nchini, vyakula vizuri wanapewa wanaume na vyakula vibovu wanakula wanawake na watoto.