October 6, 2024

Utata kifo cha mzee anayedaiwa kufariki dunia akihojiwa na polisi Mwanza

Giza limetanda kwenye familia ya mzee Malila Njiga (65), mkazi wa Nansio wilayani Ukerewe katika Mkoa wa Mwanza anayedaiwa kufariki dunia wakati akifanyiwa mahojiano ndani ya kituo cha polisi.

  • Ni Malila Njiga mkazi wa Nansio wilayani Ukerewe katika Mkoa wa Mwanza.
  • Inadaiwa alifariki dunia wakati akifanyiwa mahojiano ndani ya kituo cha polisi Nansio.
  • Ndugu na familia wagoma kuzika mwili wake  wataka uchunguzi ufanyike. 

Mwanza. Giza limetanda kwenye familia ya  mzee Malila Njiga (65), mkazi wa Nansio wilayani Ukerewe katika Mkoa wa Mwanza anayedaiwa kufariki dunia wakati akifanyiwa mahojiano ndani ya kituo cha polisi.   

Wakizungumzia tukio hilo Ndugu wa marehemu wamesema Njiga alikuwa buheri wa afya wakati anachukuliwa na diwani wa kata ya Nkilizya Fotunatus Mahatane kwenda kituoni cha polisi Nansio kwa mahojiano kufuatia kuwepo kwa madai ya tuhuma za uwizi wa simu zilizomkabili.

 Akizungumza na Nukta habari mwenyekiti wa Muungano wa jamii Tanzania (Mujata), Mathayo Makoba amesema tukio hilo lilitokea April 18 mwaka huu majira ya saa 5 asubuhi. 

“Marehemu alifuatwa nyumbani kwake majira ya saa 5 na diwani huyo na kumpakia kwenye usafiri binafsi  pasipo ndugu kupewa taarifa,  ambapo siku inayofuata baada ya kufahamika kuwa Njinga yupo kituo cha Polisi,  mke wa marehemu alimpelekea kifungua kinywa ndipo alipoelezwa kuwa mumewe alifariki wakati akifanyiwa mahojiano,” amesema Makoba.

Taarifa za kifo cha mzee huyo zimezua taharuki kwenye jamii na ndugu wa marehemu ambao wanahoji kwanini polisi hawakutoa taarifa ya ndugu yao kukamatwa na badala yake wanapewa taarifa baada kifo kutokea na tena ikiwa ni baada ya mke wa marehemu kufika kituoni siku moja baadaye.

Ndugu wa marehemu wamekataa kuchukua mwili wake na kwenda kuuzika wakitaka wapewe maelezo kuhusu kifo hicho.  


 Zinazohusiana: 


Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza,  Jumanne Muliro amemwagiza Mkuu wa Polisi wilayani humo kuhakikisha anafuatilia sakata hilo na kushirikiana na familia ili kufikia suluhu. 

Aidha, taarifa za ndani zinaeleza kuwa marehemu baada ya kuzuka kwa sintofahamu baina ya familia, na mamlaka wilayani  humo, vikao kadhaa viliketi vikihusisha pande zote ambapo maazimio yaliyofikiwa ilikua ni kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu ili kubaini chanzo cha kifo hicho.

Kwa mujibu wa chanzo ambacho hakikutaka jina lake kiwekwe hadharani, kimeiambia Nukta habari kuwa mnamo April 19, 2021 siku moja baada ya kifo cha Njinga mwili ulifanyiwa uchunguzi kwenye hospitali ya Wilaya ya Ukerewe  chini ya usimamizi wa polisi na ndugu wa marehemu.

Ilibainika kuwa marehemu alifariki dunia kutokana na ulevi wa kupindukia ambapo vipimo  vilionyesha mapafu yaliharibika kutokana na unywaji wa pombe kali.

Hadi habari hili linawekwa mtandaoni bado hakuna muafaka wa maziko ya marehemu Njinga huku  familia ikiendelea na msimamo wake  ikimtaka Diwani Mahatane au polisi kuchangia shughuli za msiba na jeneza.