Utegemee nini unapoenda hospitali?
Siyo kila ugonjwa au tatizo linahitaji dawa na Daktari kukuuliza kuhusu historia ya ugonjwa wako.
Daktari ni rafiki yako, ukionana naye uwe huru kumueleza yanayokusibu ili upate tiba kamili. Picha|Mtandao.
- Siyo kila ugonjwa au tatizo linahitaji dawa.
- Daktari kukuuliza kuhusu historia ya ugonjwa wako.
- Baadhi ya matatizo hayahitaji uchunguzi wa kimaabara bali kufanyiwa uchunguzi katika sehemu za mwili wako.
Hospitali siyo sehemu ambayo watu hupendelea kwenda. Na hii ni kwa sababu mara nyingi kimachompeleka mtu hospitali ni ugonjwa au kuwa na dalili za ugonjwa. Ni mara chache hasa katika tamaduni za kiafrika mtu kuelekea hospitali pasipo kuumwa.
Kwenda hospitali hakuepukiki kwa mtu yeyote yule kwa sababu hujui ni lini utaumwa au ndugu na rafiki watalazwa na wewe utatakiwa kwenda kuwafariji na kuwatia moyo.
Kufahamu mambo kadhaa utakayokutana nayo utakapoenda hospitali itakusaidia wewe kujiandaa kisaikolojia lakini pia kujua ni mambo gani unayoweza kukutana nayo ukiwa huko.
Ni vizuri kutambua kuwa ijapokuwa daktari ni mtaalamu wa fani hiyo, au nesi au mfamasia, lakini wote ni binadamu na hivyo moja ya siha kubwa ni urafiki.
Tambua ya kuwa mtu anayekuhudumia ni kama rafiki yako wa karibu, hivyo ili akupe huduma stahiki ni vyema kuwa muwazi na kujisikia huru. Tuangazie mambo machache ambayo ukiyafahamu yatasaidia ziara yako ya hospitali kuwa murua:
Daktari kukuuliza kuhusu historia ya ugonjwa wako. Utakapomueleza daktari wako kuhusu kuumwa kwako, atapenda kujua historia ya ugonjwa wako. Yaani ulianza lini, ulianzaje nk.
Pia katika kuchukua historia yako anaweza kukuuliza maswali yanayohusiana na aidha kabila lako, historia ya familia, historia ya zamani ya ugonjwa au upasuaji nk. Yote haya ni ili kupata uhusiano wa tatizo lako na yeye kuweza kukuhudumia kwa ufanisi zaidi.
Soma zaidi:
- Viliba tumbo bado vyawatesa watanzania
- Teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi matibabu ya figo Muhimbili
- MOI kuanza upasuaji wa ubongo kwa teknolojia ya kisasa
Kuna uwezekano tatizo lako likahitaji vipimo au la. Vipimo hivi vyaweza kuwa vya kimaabara au kiuchunguzi katika mifumo ya kawaida au ukaguzi wa sehemu ya mwili.
Baadhi ya matatizo hayahitaji uchunguzi wa kimaabara bali hufanyiwa “physical assessment” hivyo usishangae kwenda hospitali na kutopimwa kitu maabara.
Si kila ugonjwa au tatizo linahitaji dawa. Kwa utaalamu alionao daktari tambua ya kuwa sio kila tatizo linahitaji dawa. Kupitia utaalamu wa kitabibu daktari anaweza kukushauri ama kupumzika au kunywa maji ya kutosha na kupata usingizi.
Usidharau au kuona hujahudumiwa, ni vyema ukielewa kuwa ametumia sababu nyingi kufanya hivyo na tatizo linalokusumbua halihitaji tiba ya vidonge au sindano.
Ni vizuri kuwa na taarifa zako za nyuma mfano aina ya dawa uliowahi tumia, vipimo nk. Iwapo umetibiwa katika hospitali tofauti na ya mwanzo, daktari wako anaweza kukuuliza kuhusu dawa ulizowahi kutumia awali.
Pia anahitaji kujua iwapo kuna dawa unatumia kwa wakati huo. Kuwa huru kumueleza na ikiwezekana ambatana na dawa hizo uendapo kumuona.
Usiogope kwenda hospitali! Ni sehemu salama ya kupata uponyaji. Afya bora ndiyo msingi wa mafanikio yako.
Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.