July 8, 2024

Utekelezaji bajeti 2019-20 wapunguza presha wizara ya maji

hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu, wizara yake imepokea takriban theluthi tatu ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge la Tanzania katka bajeti ya mwaka 2019/2020 kiwango ambacho ni cha juu kwa utekelezaji ikilinganishwa na mwaka jana.

  • Ilitengewa Sh634.2 bilioni lakini mpaka Machi mwaka huu imepokea Sh470.4 bilioni. 
  • Katika mwaka wa 2020/2021 inapanga kutumia Sh733.3 bilioni. 

Dar es Salaam. Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amesema hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu, wizara yake imepokea takriban theluthi tatu ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge la Tanzania katka bajeti ya mwaka 2019/2020 kiwango ambacho ni cha juu kwa utekelezaji ikilinganishwa na mwaka jana. 

Utekelezaji huo huenda sasa ukapunguza presha kwa viongozi wa wizara hiyo muhimu kwa ustawi wa maendeleo Tanzania.

Katika bajeti ya mwaka 2019/2020 Wizara ya Maji iliidhinishiwa bajeti Sh634.2 bilioni ambapo kati ya fedha hizo Sh610.5 bilioni sawa na asilimia 96.2 zilikuwa ni fedha za maendeleo na kiasi kilichobaki kielekezwa katika matumizi ya kawaida ikiwemo mishahara ya wafanyakazi wa wizara. 

Prof Mbarawa aliwaambia wabunge Aprili 27, 2020 wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kuwa hadi mwezi Machi 2020 wizara hiyo ilikuwa imepokea jumla ya Sh470.4 bilioni ya bajeti yote ya mwaka huu.

Hiyo ni sawa na asilimia 74 au takribani theluthi tatu ya fedha zote za bajeti zilizoidhinishwa mwaka huu wa fedha wa 2019/2020 unaomalizika Juni 30, 2020. 

“Kati ya fedha zilizopokelewa, Sh453.6 bilioni ni za kutekeleza miradi ya maendeleo sawa na asilimia 74 ya bajeti ya fedha za maendeleo,” amesema Waziri huyo.

Kiasi hicho cha fedha ambacho kimepokelewa hadi Machi mwaka huu ni kikubwa ikilinganishwa na asilimia 54.1 zilizokuwa zimepokelewa hadi Aprili 2019 katika bajeti ya mwaka 2018/19.

Katika kipindi hicho, wizara ilikuwa imepokea jumla ya Sh376.7 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida kati ya Sh697.5 bilioni zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge mwaka 2018/2019.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifungua bomba la maji kuashiria uzinduzi wa mradi wa maji Bokwa katika Wilaya ya Kilindi, Mkoani Tanga hivi karibuni. Picha| Wizara ya Maji.

Bajeti ya maji ni moja ya bajeti ambazo huwa na mjadala mzito bungeni kabla ya kupitishwa na hufikia wakati baadhi ya wabunge hutishia kushikilia shilingi ili isipitishwe mpaka mahitaji yao yatakaposikilizwa.

Utekelezaji wa miradi na programu kwa mwaka 2019/20 ulijikita katika maeneo matano ambayo ni usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji; huduma za ubora na usafi wa maji; miradi ya huduma za usambazaji maji vijijini; miradi ya huduma za usambazaji majisafi mijini; na miradi ya usafi wa mazingira.

Hata hivyo, katika mwaka wa 2020/2021 wizara hiyo ya maji inapanga kutumia bajeti ya Sh733.3 bilioni ambapo kati ya fedha hizo, Sh705 bilioni zitatumika katika miradi ya maendeleo.

Kati ya fedha hizo za bajeti, Shilingi 349.5 bilioni sawa na asilimia 49.6 ni fedha za ndani na Shilingi 355.5 bilioni ni fedha za nje.

Fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni sawa asilimia 96.2 ya bajeti yote wizara hiyo, jambo litakalosaidia kuboresha huduma za upatikanaji wa maji safi na salama. 

Bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa 2020/2021 imeongezeka kwa Sh99.1 bilioni ikilinganishwa na ya mwaka huu na ndiyo bajeti kubwa zaidi ikilinganishwa na miaka minne iliyopita.

Mathalan, mwaka 2017/2018 wizara hiyo iliidhinishiwa Sh648 bilioni lakini mwaka uliofuta ikapanda hadi Sh697.5 bilioni kabla ya kushuka tena mwaka 2019/2020. 

Prof. Mbarawa amesema katika mwaka 2020/2021, wizara itaendelea kukamilisha miradi ya maji mijini na vijijini  inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwapatia Watanzania huduma ya maji safi na salama kwa ajili ya maisha yao.


Soma zaidi: Serikali yasema ongezeko la bajeti ya kilimo litategemea mahitaji ya kibajeti ya sekta nyingine


Mbunge wa Singida Kaskazini  Justine Monko akichangia bungeni kuhusu bajeti hiyo amesema licha wizara kutenga bajeti kubwa katika miradi ya maendeleo inatakiwa kuhakikisha fedha zinatoka kwa wakati ili miradi ya maji  iliyopangwa inakamilika kwa wakati.

“Fedha zinachelewa kutoka na hivyo wakandarasi wanashindwa kukamilisha miradi ya maji kwa wakati kwa sababu ya watu wachache wanaotumia muda mrefu kuidhinisha fedha,” amesema Monko.