October 7, 2024

Uthabiti wa Zakia Meghji wachagiza uboreshaji miundombinu ya Chuo Kikuu cha MUST

Ni Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho aliyeteuliwa na Rais John Magufuli Disemba 2018, ambaye amekuwa na uwezo mkubwa kufuatilia uboreshaji wa miundombinu ya maktaba, barabara na mabweni chuoni hapo.

Muonekano wa Chuo Kikuu Cha Sayansi na Teknolojia (MUST). Picha|MUST.


  • Ni Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye aliteuliwa na Rais John Magufuli Disemba 2018.
  • Amekuwa na uwezo mkubwa kufuatilia uboreshaji wa miundombinu ya maktaba, barabara na mabweni chuoni hapo. 

Dar es Salaam. Ikiwa imepita zaidi ya miezi minne tangu Rais John Mgufuli amteue Zakia Meghji kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Cha Sayansi na Teknolojia (MUST), leo ameeleza sababu za kumteua ikiwemo uchapakazi na uwezo mkubwa wa kufuatilia mambo. 

Meghji ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali serikalini ikiwemo Waziri wa Fedha kati ya 2006 na 2008 aliteuliwa kushika nafasi hiyo Disemba 6, 2018 pamoja na Spika mstaafu Pius Msekwa ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa chuo hicho. 

Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza na jumuiya ya chuo hicho leo (Aprili 3, 2019) jijini Mbeya, amesema anamfahamu vizuri Meghji kama mtu aliye thabiti na mwenye maamuzi mazuri katika mipango ya maendeleo.

“Bahati nzuri nimewateulia Mwenyekiti wa Chuo aliyetofauti ninayemfahamu, Zakia Meghji, kwenye mwaka 1995 mimi nilikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, yeye alikuwa Waziri wa Afya, saa zingine nilipokuwa nikikwama mambo yangu, ananiambia bwana mdogo nenda kafanye, alikuwa ana encourage (ananihamasisha), uongo mama Zakia? She was very tough (Alikuwa thabiti),” amesema Rais Magufuli. 

Uzoefu wake wa kukaa Serikalini kwa muda mrefu umemjengea heshima ya kuteuliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi.

“Nguvu za mwili kadiri umri unavyoenda zinapungua lakini She was very tough .Zakia Meghji alikuwa waziri wa fedha wa nchi hii! Na ndio maana nikaamua kumteua kuwa mwenyekiti na kweli ananisumbua kweli,” amesema. 

Kutokana na uongozi wake katika baraza la chuo, Meghji amechagiza miradi mbalimbali ya uboreshaji miundombinu ya chuo hicho ikiwemo ujenzi wa maktaba ya kisasa, mabweni ya wanafunzi na barabara ya lami inayoelekea chuo hapo ambapo mkandarasi ameanza kuijenga.


Zinazohusiana:


Hata hivyo, Rais Magufuli amemtaka mkandarasi wa kampuni ya Chinese Seven Group limited kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara hiyo yenye zaidi ya kilomita mbili kwa sababu ni muhimu kwa jumuiya ya chuo hicho. 

Amesema kwa muda mrefu chuo hicho kimeachwa nyuma katika uboreshaji wa miundmbinu yake, licha ya kuwa kiliasisiwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere.

“Chuo ambacho kilijengwa na baba wa Taifa, tulichelewa kujenga barabara ya lami hapa ni lazima tutubu sisi kama Serikali. Ilitakiwa hiki chuo kilichojengwa na baba wa taifa tuwe tumekijenga kwa lami. Kwa hiyo kwa niaba ya Serikali nawaomba radhi,” amesema Rais. 

Amesema Serikali imetenga Sh10.4 bilioni ambazo zinahusisha baadhi ya barabara katika mkoa wa Mbeya ikiwemo ya chuo cha MUST. 

Chuo hicho kimekuwa sehemu muhimu  ya wahitimu kupata mafunzo, ujuzi katika nyanja mbalimbali za sayansi na teknoloji unaohitajika katika shughuli ukuaji wa uchumi wa viwanda.