Uvaaji wa barakoa muda mrefu hausababishi uhaba wa oksijeni mwilini
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema uvaaji wa muda unaweza kuwakera wengi ila hauna madhara kama inavyodaiwa.
- Hakikisha umevaa vizuri barakoa yako kiasi cha kusitiri pua na mdomo.
- WHO imesema uvaaji wa muda unaweza kuwakera wengi ila hauna madhara kama inavyodaiwa.
Dar es Salaam. Miongoni mwa habari unazotakiwa kuzipuuzia kipindi hiki ni pamoja na ile inayosema uvaaji wa barakoa kwa muda mrefu unasababisha ukosefu wa hewa ya oksjeni mwilini na kuongeza sumu kutokana na kuvuta hewa chafu ya dioksidi kaboni (carbon dioxide).
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza kuwa habari hiyo haina ukweli wowote uliothibitishwa kisayansi.
“Uvaaji wa muda mrefu wa barakoa kuna wakati unakera lakini hausababishi madhara kwa kuvuta hewa ya dioksidi kaboni au kusababisha ukosefu wa oksijeni mwilini,” imesema WHO.
Shirika hilo linaeleza kuwa yakupasa uvae vema barakoa yako kwa kuhakikisha unasitiri pua na mdomo wako vizuri kiasi cha kukuwezesha kupumua vema.
“Usitumie zaidi ya mara mbili barakoa inayopaswa kutumika kwa muda mfupi na kutupwa (disposable masks) na jitahidi kuibadilisha mara utakapoona imeshika uchafu au kuwa umefika maeneo hatarishi yenye corona,” limesema shirika hilo ambalo hutoa miongozi ya kiafya ulimwenguni.
Tufuate kwenye mitandao yetu Twitter, Facebook @NuktaFakti na Instagram @nuktafakti kwa taarifa zaidi kuhusu habari sahihi za corona.