November 24, 2024

Uwanja wa ndege Marekani wajipanga kuzuia matumizi ya chupa za maji za plastiki

Hatua hiyo ni kuendeleza jitihada za utunzaji wa mazingira na kuokoa viumbe vya baharini.

  • Hatua hiyo ni kuendeleza jitihada za utunzaji wa mazingira na kuokoa viumbe vya baharini. 
  • Watumiaji wa uwanja huo wamepinga hatua hiyo kwa madai kuwa haina tija.
  • Wanywaji wa soda, juisi zinazohifadhiwa katika chupa za plastiki haiwahusu.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa San Francisco uliopo Marekani unakusudia kuanza kutekeleza marufuku ya matumizi ya chupa za maji za plastiki zinazotumika na watumiaji wa uwanja huo kuanzia Agosti 20, 2019. 

Duru za kimataifa zinaeleza kuwa upigaji marufuku wa chupa hizo za maji ni sehemu ya mpango wa miaka mitano wa kupunguza uchafuzi wa mazingira ikiwemo taka za plastiki kwenye vyanzo vya maji. 

“Sisi ni “Airport’ (kiwanja cha ndege) ya kwanza kutekeleza mabadiliko haya,” amesema Msemaji wa uwanja huo,  Doug Takel wakati akizungumza na Wanahabari. 

Hata hivyo,  marufuku hiyo hazihusu chupa plastiki za juisi au soda bali chupa zenye maji.

Pia migahawa, maduka na wachuuzi wote hawaruhusiwa kuuza bidhaa hiyo katika uwanja huo, licha ya kuwa ndege zinazotumia uwanja huo zitaendelea kutumia chupa hizo kwa wateja wake. 

Wasafari wanaotumia uwanja huo wamekuwa na maoni tofauti kuhusu marufuku hiyo itakayoanza siku saba zijazo ambapo baadhi wamesema hawaoni marufuku hiyo kama ina maana yoyote kwa sababu haijahusisha vinywaji vingine vinavyotumia chupa za plastiki. 

Wengine wamesema hiyo ni njia ya uongozi wa uwanja huo kuwalazimisha watu kunywa soda badala ya maji na kuwa huenda marufuku hiyo isilete matokeo yaliyokusudiwa. 


Soma zaidi: 


Hatua kama hizo za zimechukuliwa na Tanzania ambapo kwa sasa wananchi wote hawaruhusiwi kutumia mifuko ya plastiki, licha ya kuwa bado chupa za maji zinatumika kama kawaida. 

Kwa sasa wageni wanaotumia mipaka na viwanja vya ndege hawaruhusiwi kuingia na mifuko ya plastiki, jambo ambalo linatajwa kuwa litasaidia kulinda mazingira kwa kuhimiza matumizi ya mifuko mbadala. 

Airport ya San Francisco inajinasibu kama kama “kiongozi wa mabadiliko endelevu” kwa kutumia umemejua na kuwataka watoa huduma katika uwanja huo kutumia teknolojia rahisi inayohifadhi mazingira.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa San Francisco uliopo Marekani. Picha|Mtandao.

Airport za Dubai na India nazo zimetangaza kupiga marufuku ya chupa za maji za plastiki lakini mpaka sasa bado hazijaanza kutekeleza kwa vitendo. 

Jiji la San Francisco lilizuia uuzaji wa chupa za maji za plastiki tangu mwaka 2014, lakini ilijipa muda na kuchelewa ili kuweka mambo sawa. 

Inaelezwa kuwa uzalishaji wa plastiki duniani umeongezeka kwa viwango vya juu ambapo kila mwaka tani milioni 400 zinazalishwa.

Kila mwaka mamilioni ya ndege na viumbe wa baharini zaidi 100,000 duniani kote wanajeruliwa na kufa kwa kumeza plastiki katika mifumo yao ya chakula.  

 Canada na Umoja wa Ulaya unakusudia kuipiga marufuku ya matumizi ya plastiki kuanzia 2021.