October 6, 2024

Uwekezaji miradi mipya washuka Tanzania

Kuondolewa kwa vivutio vya kifedha kumeshusha usajili wa miradi mipya ya uwekezaji kwa asilimia 37.7 ndani ya mwaka mmoja.

  • Kuondolewa kwa vivutio vya kifedha kumeshusha usajili wa miradi mipya ya uwekezaji kwa asilimia 37.7 ndani ya mwaka mmoja. 
  • Thamani ya miradi mipya nayo yashuka kwa asilimia 44.4.
  • Dar yaongoza kusajili miradi mingi huku sekta ya viwanda ikiongoza kuwa na miradi mingi ya uwekezaji. 

Dar es Salaam. Huenda Serikali ikawa na kibarua kigumu cha kuvutia wawekezaji nchini baada ripoti mpya ya hali ya uchumi wa Taifa kuonyesha idadi ya miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita imeporomoka kwa asilimia 37.7. 

Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018 kilichotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Juni mwaka huu, kinaeleza kuwa Mwaka 2018, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilisajili miradi 215 ikilinganishwa na miradi 345 mwaka 2017. 

Hiyo ni sawa na upungufu wa asilimia 37.7 au upungufu wa miradi  130 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. 

“Upungufu huo ulitokana na kuondolewa kwa vivutio vya kifedha kwenye miradi ya upanuzi na bidhaa za msingi zisizo za mitaji,” inasomeka sehemu ya kitabu hicho ikieleza sababu za kushuka kwa usajili wa miradi ya uwekezaji. 

Hali hiyo imesababisha kupungua kwa thamani ya miradi iliyosajiliwa na kuathiri upatikanaji wa ajira mpya kwa Watanzania katika sekta mbalimbali za uzalishaji, kitabu hicho kinaeleza. 

“Thamani ya miradi iliyosajiliwa ilipungua kwa asilimia 44.4 kutoka dola za Marekani bilioni 5.07 mwaka 2017 hadi dola bilioni 2.82 mwaka 2018. 

“Aidha, miradi iliyosajiliwa mwaka 2018 ilitoa fursa za ajira 27,469 ikilinganishwa na fursa za ajira 30,728 mwaka 2017, sawa na upungufu wa asilimia 10.6,” kinaeleza kitabu hicho.


Zinazohusiana: 


Licha ya usajili miradi kupungua, wazawa ndiyo waliojitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa ya kuanzisha na kusajili miradi mipya ukilinganisha na wageni kutoka nje ya nchi. 

Kati ya miradi iliyosajiliwa mwaka 2018, miradi 132 au asilimia 61.3 ilikuwa ya Watanzania, wageni (69) na 14 ilikuwa ni ya ubia kati ya Watanzania na wageni. 

Hii ni tofauti na mwaka 2017 ambapo miradi mingi ilikuwa ni ya wageni wakiwa na  na miradi 168, Watanzania (miradi 84) huku miradi 85 ikifanywa kwa ubia. 

Hata hivyo, Sekta ya uzalishaji viwandani ndiyo iliyoongoza kusajili miradi mingi inayofikia 108 huku sekta ya huduma za biashara ikiongoza kwa kusajili miradi yenye thamani kubwa ya dola za Marekani bilioni 1.07 licha ya kusajili miradi 16 tu. 

Katika mgawanyiko wa miradi kimkoa, mkoa wa Dar es Salaam uliongoza kwa kuvutia miradi mingi ya uwekezaji ambapo miradi 109 ilisajiliwa kwa sababu ya kuwepo kwa mazingira wezeshi ya uwekezaji hasa miundombinu bora ikilinganishwa na mikoa mingine. 

Aidha, mkoa wa Pwani ulisajili miradi 37, Arusha miradi tisa, Kilimanjaro miradi (8) na Morogoro (8) huku mikoa ya Katavi, Kigoma, Lindi , Rukwa, Ruvuma, na Simiyu haikusajili mradi wowote mwaka jana.

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilisajili miradi 215 ikilinganishwa na miradi 345 mwaka 2017. Picha|Mtandao.

Serikali yachukua hatua

Juni 7 mwaka huu, Rais John Magufuli alipokutana wafanyabiashara Ikulu Jijini Dar es Salaam alieleza kuwa Serikali itazitatua changamoto zote za uwekezaji nchini ili kuweka mazingira mazuri ya uendeshaji biashara na kuongeza mapato ya Serikali.

Katika hotuba yake alianisha vikwazo vya biashara nchini ikiwemo rushwa, utitiri wa kodi na tozo, ukosefu wa mitaji na utitiri wa taasisi zinazosimamia biashara ambapo kuvipatia ufumbuzi. 

Hata katika hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali ya 2019/2020, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesisitiza kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kwa kujikita zaidi katika kushughulikia kero za kodi, tozo na ushuru wa forodha. 

“Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (BluePrint) ulioidhinishwa mwaka 2017/18 kwa kuanza kupitia mfumo wa tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Mamlaka za Udhibiti kwa lengo la kupunguza au kuzifuta baadhi ya tozo na ada, kupunguza na kuondoa muingiliano katika kutoza tozo hizo,” alisema Dk Mpango huku akitangaza kufuta tozo 54 kutoka kwa wizara na taasisi mbalimbali za Serikali.