October 8, 2024

Uzalishaji viwandani waipaisha Dar usajili miradi ya uwekezaji

Wakati Dar es Salaam ikiongoza orodha hiyo, mikoa ya Katavi, Kigoma, Lindi, Rukwa, Ruvuma, na Simiyu haikusajili mradi wowote mwaka 2018.

  • Ni baada ya kusajili zaidi ya nusu ya miradi iliyosajiliwa Tanzania mwaka 2018.
  • Mikoa inayofuata ni Pwani ambayo imesajili miradi 37 huku Arusha ikisajili miradi tisa.
  • Wakati Dar es Salaam ikiongoza orodha hiyo, mikoa ya Katavi, Kigoma, Lindi, Rukwa, Ruvuma, na Simiyu haikusajili mradi wowote mwaka 2018.

Dar es Salaam. Jiji la Dar es Salaam limeongoza kusajili miradi mingi ya uwekezaji kwa mwaka 2018 baada ya kusajili miradi 109 ambayo ni sawa na asilimia 50.6 ya miradi yote 215 iliyosajiliwa mwaka huo.

Hiyo ni sawa na kusema zaidi ya nusu ya miradi ya uwekezaji iliyopo Tanzania inapatikana katika jiji hilo linalokuwa kwa kasi barani Afrika.

Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2018, jiji hilo limesajili zaidi miradi inayohusisha uzalishaji viwandani inayofikia miradi 49 huku likiipiga mkumbo mikoa yote nchini.

Mkoa unaofuatia kwenye orodha hiyo ni Pwani ambao umesajili miradi 37 tu huku nao ukiongoza kusajili miradi mingi ya majengo ya biashara inayofikia mitano na miradi ya kilimo mitatu.

Wakati Dar es Salaam ikiongoza orodha hiyo, mikoa ya Katavi, Kigoma, Lindi, Rukwa, Ruvuma, na Simiyu haikusajili mradi wowote mwaka 2018.

Miradi mingine iliyoorodheshwa na  kitabu hicho ni pamoja na miradi ya utalii, kilimo, utangazaji, majengo ya biashara, miundombinu, nishati na miradi ya kifedha.

Miradi mingine ni miradi ya rasilimali watu, maliasili, miradi ya huduma, usafirishaji na madini.