November 24, 2024

Uzalishaji wa maua ulivyoshuka kwa kasi Tanzania

Ndani ya mwaka mmoja, umeshuka kwa zaidi ya asilimia 80 ukichochewa na baadhi ya nchi kufunga mipaka na kuzuia mikusanyiko ikiwemo sherehe.

  • Ndani ya mwaka mmoja, umeshuka kwa zaidi ya asilimia 80.
  • Hali hiyo imechochewa na baadhi ya nchi kufunga mipaka na kuzuia mikusanyiko ikiwemo sherehe.
  • Wadau washauri kuondolewa kwa maua ya plastiki yanayoingilia soko la maua ya shambani.

Dar es Salaam. Ni sherehe gani ambayo umehudhuria na ikakosa maua? Katika karne hii ya 21, karibu kila sherehe, utakutana na maua ya kila aina.

Kuanzia maua waridi, “mums”, “lilies” na maua mengine mengi, ni sehemu ya mapambo ambayo hutumika kupamba sherehe na wengine wakiyatoa kama zawadi kwa watu wanaowajali.

Hata hivyo, kwa mwaka 2020, uzalishaji wa maua umeshuka kwa kiwango kikubwa, hali inayohatarisha biashara hiyo ambayo kwa wengine ni chanzo cha mkono kwenda kinywani.

Kwa mujibu wa Kitabu Cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020 kilichotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), uzalishaji wa maua umeshuka hadi tani 1,710 mwaka 2020 kutoka tani 13,240 mwaka juzi.

Hilo ni sawa na angulo la asilimia 87.1 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Kupungua kwa uzalishaji wa maua mwaka jana kunaacha mwaswali mengi ikizingatiwa kuwa uzalishaji wa zao hilo umekuwa ukipanda kila mwaka tangu mwaka 2016. 

“Upungufu huo ulitokana na kushuka kwa uhitaji wa maua kwenye soko la dunia kulikosababishwa na athari za UVIKO-19,” imeeleza sehemu ya kitabu hicho.

Hata hivyo, wakulima hasa vijana wana nafasi ya kuongeza uzalishaji wa maua mwaka huu na wanaweza kufaidika na soko la ndani na kimataifa hasa katika nchi za Ulaya ambazo zina watumiaji wengi. 

Maua hutumika kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kutengeneza dawa, manukato, mapambo ya nyumbani na kupeana zawadi kwa wapendanao. 

Zao hilo la biashara hulimwa zaidi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Njombe na linaweza kulimwa nyumbani ikiwa kuna usimamizi mzuri. 

Mfanyabiashara wa maua jijini Dar es Salaam, Irene Albert ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa uzalishaji wa maua kwa mwaka jana unaweza kuwa umepungua kutokana na nchi nyingi kufunga mipaka yake na baadhi ya nchi kukataza mikusanyiko ikiwemo sherehe za aina yoyote.

“Ni wazi wakulima waliogopa kulima kwasababu sehemu za mauzo yao zilikuwa zimefungwa, hata Tanzania ilizuia sherehe. Endapo wangezalisha wangepata hasara hasa ikizingatiwa kuwa ua ni zao la muda mfupi, hauwezi kuliweka likakaa mwaka mzima au hata mwezi. Lina chanua, linanyauka,” Albert amesema.

Kwa mwaka 2021, Albert ameshauri watu kurudia tamaduni za kuwatumia wapenzi wao maua na kuachana na maua ya plastiki ambayo yameanza kuingilia soko.

“Watu wameanza kupenda maua ya  plastiki kwa sababu yanakaa kwa muda mrefu na mpambaji anaweza kuyatumia kwenye sherehe nyingi kwa sababu hayaharibiki. Tofauti na maua ya shambani ambayo hutumika mara moja, mbili kisha kutupwa,” amesema Albert.