October 6, 2024

Vibaka watajwa kusababisha vifo vya watu 20 mkutano wa dini Moshi

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema uchunguzi wa awali wa vifo vya watu 20 katika kongamano la Nabii na Mtume, Boniface Mwamposa mjini humo unaonyesha kuwa vimesababishwa na vibaka kuingilia na kuvuruga utaratibu wa ibada ya kukanyaga mafuta

  • Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema fununu zinaeleza kuwa vibaka hao waliingilia utaratibu wa kukanyaga mafuta ili kupora watu.
  • Watakiwa kujisalimisha la sivyo, damu ya waliokufa haitawaacha salama.
  • viongozi wa dini wakumbushwa kuhubiri maarifa ya upendo na amani na siyo kutumia matatizo ya watu kujipatia mali na utajiri.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema  uchunguzi wa awali wa vifo vya watu 20 katika kongamano la Nabii na Mtume, Boniface Mwamposa mjini humo unaonyesha kuwa vimesababishwa na vibaka kuingilia na kuvuruga utaratibu wa ibada ya kukanyaga mafuta kwa nia ya kuwapora watu vitu vyao. 

Vilio na simanzi vimetawala katika viwanja vya Mashujaa mjini Moshi mkoani humo leo wakati wa kuaga miili ya watu  waliokufa Jumamosi Februari Mosi, 2020 katika kongamano hilo.

Mghwira aliyekuwa akizungumza wakati akitoa salamu za Serikali wakati wa kuaga miili ya watu waliofariki, amesema kilichokosekana katika kongamano hilo ni utaratibu mzuri wa watu kukanyaga mafuta yanayosemakana kuwa ni ya baraka.

“Jana nimeenda kuona pale (uwanja wa Majengo) kulikuwa na hayo aina ya mabeseni mengi (ya mafuta), sasa sielewi kwanini watu walikwenda kuzongana katika lango moja. Malango yote yalikuwa na hayo mabeseni yenye mafuta. Kwa hiyo kilichotakiwa hapo ni utaratibu wa watu kujipanga,” amesema Mghwira. 

Amebainisha kuwa kuna fununu kuwa vibaka walipoona hakuna utaratibu, wao wakaingia na utaratibu wao wa kutaka kupora na kusababisha tatizo. 

“Watu wakaanza kukanyagana mpaka sasa tutaachia vyombo vya uchunguzi vitatuambia kwamba ni waumini walikanyagana au ni watu wengine walileta kukanyagana wakati wa kutoka nje,” amesisitiza Mghwira aliyekuwa akizungumza huku mvua ikinyesha uwanjani hapo.

Amewataka vijana walioingilia utaratibu wa ibada ya kukanyaga mafuta na kusababisha watu kukanyagana, wajitafakari na kujitokeza mbele ya umma kwa sababu damu za watu waliofariki hazitawaacha salama.

Waliofariki katika tukio hilo la kusikitisha ni watoto na watu wazima wanaotoka katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambapo baada ya kuagwa wanasafirishwa katika maeneo yao kwa ajili ya mazishi.

Sehemu ya uwanja wa Majengo mjini Moshi, mara baada ya kutokea kwa vifo vya watu 20 wakikanyagana kukanyaga mafuta ya upako. Picha|Mtandao.

Viongozi wa dini watakiwa kuimarisha amani

Katika hatua nyingine, Mghwira amewataka  viongozi wa dini kuwa chachu ya maarifa ya amani, upendo wa kweli na hali ya kujali watu huku wakifuata taratibu za kufanya mihadhara zilizowekwa kisheria.

“Jambo hili limetuogopesha, jambo hili limetutia hofu, lakini jambo hili halijatuvunja niwaombe watu wa Mungu, watu wote, viongozi tushikamane sana kwa ajili ya jambo hili. jambo hili liwe mwanzo wa kuimarisha mambo ya imani,” amesema. 

Mapema leo asubuhi Rais John Magufuli alitoa salamu za rambirambi kwa mara nyingine kwa wafiwa.

Katika mazungumzo yake na Rais Magufuli, Mghwira amesema mkuu huyo wa nchi amewataka viongozi wa dini na Serikali washughulikie mapungufu yaliyojitokeza na wasifunge shughuli za dini. 


Soma zaidi: 


Mpaka sasa Jeshi la Polisi linamshikilia Nabii Mwamposa ambaye anaongoza kanisa la Inuka Uangaze na watu wengine saba akiwemo Mchungaji wa kanisa la Calvari Assemblies of God,  Elia Mwambapa kwa mahojiano kuhusu tukio hilo.  

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya za Kilimanjaro, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amesema viongozi wa dini wanapaswa kujitafakari na wasitumie matatizo ya watu kujipatia utajiri na mali bali wawasaidie kumjua Mungu zaidi kwa mafundisho ya kweli.

“Ni kweli Wachungaji, wananchi wetu wanateseka sana, ni kweli wana mizigo mizito, wana matatizo ya ndoa, wana matatizo ya VICOBA, wana matatizo ya madeni lakini tusigeuze tabu zao kuwa ni mtaji wa kuwajipatia utajiri,” amesema Sabaya.